Thursday, December 2, 2010

Kikwete aomboleza kifo cha mtoto wa Aboud Jumbe


Dk. Suleiman Aboud Jumbe Mwinyi, mtoto wa kwanza wa Mheshimiwa Jumbe, alifariki dunia mchana wa juzi, Jumatatu, Novemba 29, 2010, katika Hoteli ya MDS Lodge iliyoko Sarita Vihar mjini New Delhi, India, ambako alikuwa amempeleka baba yake kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya Apollo.

Kwa mujibu wa habari kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini India, Dk. Suleiman A. Jumbe Mwinyi alikutwa na mauti chumbani mwa hoteli alimokuwa amefikia, na mwili wa daktari huyo utawasili Zanzibar kesho, Alhamisi, Desemba 2, 2010, kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia (ET) tayari kwa mazishi.

Katika salamu zake, Mheshimiwa Kikwete amemwambia Mheshimiwa Jumbe: “Nashindwa kuelezea kiasi cha majozi na huzuni niliopata baada ya kutaarifiwa kuhusu kifo cha ghafla cha mwanao, Dk. Suleiman Aboud Jumbe Mwinyi, na msiba huo mkubwa uliokufika”.

Ameongeza Rais Kikwete: “Napenda kutuma rambirambi za dhati ya moyo wangu kwako kufuatia msiba huu mkubwa. Napenda kukuthibitishia kuwa mimi na wenzangu katika Serikali tuko nawe katika msimba huu mkubwa na katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi makubwa sana.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Nakuomba pia kwa kupitia kwako uwasilishe salamu zangu za rambirambi na wenzangu katika Serikali kwa familia yako yote na kwa jamaa na marafiki ambao kwa namna moja ama nyingine wameguswa na msiba huu”.

Amemalizia: ”Tunajua kuwa mnapitia kipindi kigumu. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awapeni nguvu, subira na uvumilivu wa kubeba majonzi ya kipindi hiki kwa sababu yote ni mapenzi yake.”