Wednesday, October 10, 2012

Rais Mtaafu Mwinyi aibiwa milioni 37

 Apanda kizimbani kisutu kutoa ushahidi

Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi
RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi, ameibiwa sh milioni 37.4 na hivyo kulazimika kupanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutoa ushahidi wake linaripti gazeti la Tanzania Daima la Tanzania.


Kwa hatua hiyo, Mzee Mwinyi anafuata nyayo za Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliyepanda kizimbani hivi karibuni kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin.

Mzee Mwinyi ambaye alipanda kizimbani jana, anadai kuibiwa sh 37,440,000 na Abdallah Nassoro Mzombe (39) ambaye ni wakala wake.



Mbele ya Hakimu Mkazi, Genivitus Dudu, mshtakiwa huyo, mkazi wa Kinondoni Mkwajuni, anashtakiwa kwa makosa ya kumuibia Mzee Mwinyi kiasi hicho cha kodi ya pango ya nyumba mbili zinazomilikiwa na Rais huyo mstaafu.



Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ambayo Tanzania Daima Jumatano ina nakala yake, Mzombe anadaiwa kufanya makosa hayo kinyume na kifungu cha 258 na 273 (b) (e) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya Sura ya 16 ya mwaka 2002.
Siku hiyo ya Agosti 21, mwaka huu, ilidaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai 2012 huko Mikocheni, Mzombe akiwa wakala wa Rais huyo mstaafu, alimwibia sh 17,640,000 ambazo ni pato la kodi ya nyumba yake iliyoko eneo la Mikocheni, wilaya ya Kinondoni.

Iliendelea kudai kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho Mzombe alimwibia Rais Mwinyi kilikuwa ni kodi ya pango la nyumba namba 481, iliyoko kwenye ploti A huko Mikocheni ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013.
Aidha anadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, mwaka 2011 na Julai 10, mwaka huu huko Msasani Village wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa huyo alimwibia tena Rais huyo mstaafu sh 19,800,000 ambazo zilikuwa ni kodi ya nyumba namba 55 iliyoko kwenye Kitalu C .
Kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni kodi ya pango la nyumba hiyo la mwaka 2011/2012 na 2012/2013.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alikana mashtaka yote na yuko rumande hadi Oktoba 22 kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa.
Rais Mwinyi jana alitua katika mahakama hiyo huku akiongozwa na maofisa Usalama wa Taifa (TISS) kuja kutoa ushahidi katika kesi hiyo ya jinai Na. 201/2012 iliyofunguliwa na serikali dhidi ya wakala wa Mwinyi, Abdallah Nassoro Mzombe (39).
Kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, Mwinyi alihifadhiwa kwa muda kwenye chumba namba moja cha mahakama hiyo ili kutoa muda kwa wakili wa serikali, Charles Anindo, kumuandaa.
Waandishi wa habari waliokuwepo mahakamani hapo kwa ajili ya kuripoti kesi hiyo, walizuiliwa kuingia, jambo ambalo lililalamikiwa vikali na wana habari hao.
“Msiingie humu ndani haiwahusu,” alisema ofisa habari mmoja, akiwazuia waandishi kuingia ndani ya mahakama hiyo.
Mzee Mwinyi aliondoka katika viwanja vya mahakama hiyo majira ya saa 6:21 mchana na kisha kupanda gari aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili T 914 BJT.
Hati ya mashtaka ya kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Agosti 21 mwaka huu.
Mei 7 mwaka huu Rais Mkapa alifika mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Elvin Mugeta, kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, na Grace Martin. Mahalu aliachiwa huru katika kesi hiyo.