Wednesday, October 10, 2012

Ripoti kamili ya mwandishi aliyeuawa hii hapa


Dr. Emmanuel Nchimbi Waziri wa Mambo ya Ndani


TAARIFA YA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MWANDISHI WA HABARI WA
CHANNEL TEN BW. DAUD MWANGOSI
1.0 UTANGULIZI
Mnamo tarehe 03 Septemba mwaka 2012, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe.
Dkt. Emmanuel Nchimbi (MB) aliteua Kamati ya watu watano kufanya uchunguzi
kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel
Ten, marehemu Daud Mwangosi, kilichotokea tarehe 02 Septemba 2012, katika Kijiji
cha Nyololo,Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa. Kituo cha kazi cha marehemu Daud
Mwangosi kilikuwa mkoa wa Iringa ambapo pia alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya
Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Iringa (IPC).

Wajumbe wa Kamati hiyo ni:
Jaji (Mst.) Steven Ihema - Mwenyekiti
Bibi Pili Mtambalike - Mjumbe
Kanali (Dkt. Eng) Wema Wilson Wekwe - Mjumbe
Bwana Theophil Makunga - Mjumbe
Naibu Kamishna wa Polisi Issaya Juma. Mngulu - Katibu
Sekretarieti ya Kamati ni:
Bi. Edith T. Assenga - Wizara ya Mambo ya Ndani
Bwana Nasoro H. Msumi - Wizara ya Mambo ya Ndani
1
2.0 HADIDU ZA REJEA
Kamati ilipewa Hadidu za rejea zifuatazo:
 Uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo,Wilaya ya
Mufindi, Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba, 2012 na kuwepo kwa uvunjifu
wa amani.

 Kama yalikuwepo makubaliano au maelekezo kuhusu mikutano ya hadhara au
maandamano nchini katika kipindi cha Sensa.
 Mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu iliyosababisha kifo cha
Marehemu Daud Mwangosi na wengine kuumizwa, na uwiano wa nguvu hiyo
na tukio.
 Madai ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari
Mkoa wa Iringa na chanzo cha uhasama huo. Aidha kuna madai ya kuwepo
kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao Jeshi la Polisi limepanga
kuwashughulikia.
 Uwepo wa Sheria, Kanuni au Taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la Polisi
kuzuia mikusanyiko inayoitishwa na Vyama vya Siasa na Mamlaka ya Rufaa
endapo vyama hivyo havitaridhika na amri hizo.
 Hali ya Mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa nchini katika
Utendaji kazi wao na Utii wa Sheria.
3.0 MUDA WA UCHUNGUZI
Kamati ilipewa muda wa siku 19 kuanzia tarehe 11 Septemba 2012 iwe imekamilisha
uchunguzi na kuwasilisha Ripoti yake ifikapo tarehe 02 Oktoba 2012.
2
4.0 NJIA ZILIZOTUMIKA KUFANYA UCHUNGUZI:
4.1 Mahojiano na watu mbalimbali waliokuwepo kwenye tukio.
4.2 Kupitia nyaraka na vielelezo mbalimbali.
4.3 Kutembelea eneo la tukio.
4.4 Majadiliano na vikundi mbalimbali (viongozi wa dini ngazi ya kijiji na wilaya
hadi ya mkoa; viongozi wa vyama vya siasa kwenye ngazi ya kijiji, wilaya, mkoa na
Taifa, viongozi wa serikali ngazi ya kijiji, wilaya, mkoa, Taifa) na wanakijiji wa
Nyololo.
5.0 UCHUNGUZI
Kamati ya Uchunguzi ilifanya mahojiano na watu mbalimbali ikiwa pamoja na
watendaji wa serikali hususan Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya wilaya Mufindi na
mkoa wa Iringa viongozi wa Jeshi la Polisi viongozi wa vyama vya Siasa, Viongozi wa
Madhehebu ya Dini, Waandishi wa Habari na wananchi wa kawaida (ngazi ya Kijiji,
Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa).
3
6.0. YALIYOJITOKEZA
Baada ya Kamati kukutana na makundi ya watu mbalimbali katika Mkoa wa Iringa na
Viongozi wa Vyama vya Siasa wa kitaifa jijini Dar es Salaam, mambo kadhaa
yalijitokeza na baadhi yao ni:
 Hofu ya kutoweka kwa amani miongoni mwa viongozi na wananchi hasa
katika mikutano na maandamano ya siasa ambayo yameanza kuota mizizi ya
uvunjifu wa amani na mengine kusababisha mauaji. Viongozi na wananchi
wengi waliotoa maoni yao mbele ya Kamati wameonyesha hofu kuwa hali
hiyo isipodhibitiwa mapema inaweza kulipeleka pabaya Taifa letu.
 Kuna walakini wa mahusiano kati ya waandishi wa habari na Jeshi la Polisi
mkoani Iringa.
 Uwepo wa utashi wa makusudi/dhati kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa
kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya vyama.
 Umuhimu wa Ushirikiano na mahusiano baina ya vyombo vya serikali, vyama
vya siasa, wanahabari na wananchi kwa ujumla badala kuonyeshana ubabe
ambao umetufikisha hapo.
 Haja ya kufanya mabadiliko ya kisheria katika mfumo wa usimamizi na
utendaji wa masuala ya siasa nchini
 Haja ya kuwa na mabadiliko ya kimfumo katika Jeshi la Polisi badala ya ulioko
sasa ambao kwa maoni ya baadhi ya watu waliozungumza na Kamati ni wa
kitaifa zaidi na kuacha serikali za mitaa bila ya wajibu wa kulinda usalama wa
raia na mali zao.
 Kwamba nguvu kubwa inatumika na vyombo vya dola/usalama dhidi ya raia
na hivyo kupunguza imani ya jamii kwa vyombo hivyo.
4
 Kupungua kwa maadili/uzalendo miongoni mwa Watanzania kuanzia viongozi
hadi wananchi hususan kwenye shughuli za kisiasa.
 Haja ya kusisitiza elimu ya uraia kwa jamii kuanzia kwa watoto hadi kwa watu
wazima hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi ili kujenga umoja wa
kitaifa.
 Kuwepo kwa mikutano na maandamano ya vyama vya siasa yasiyokuwa na
kikomo.
 Muonekano wa Jeshi la Polisi mbele ya jamii.
5
7.0. MATOKEO YA UCHUNGUZI KUTOKANA NA HADIDU ZA REJEA
7.1 Kuhusu “Uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la
Nyololo, Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba 2012 na
kuwepo uvunjifu wa amani”, uchunguzi wa Kamati umebaini yafuatayo:
Tarehe 30 Agosti 2012 CHADEMA iliandika barua, Ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya
Mufindi kutoa taarifa kuhusu ratiba ya mikutano ishirini na sita (26) kwenye majimbo
ya Mufindi Kusini na Kaskazini tarehe 02-03 Septemba 2012. Awali ratiba ya
mikutano hiyo ilikubaliwa, lakini baadaye siku hiyo ya tarehe 01 Septemba 2012
mikutano hiyo ilisitishwa kwa barua Kumb. Na MFG/A.24/9/54 kutokana na
kuongezwa siku za zoezi la Sensa ya watu na Makazi hadi tarehe 08 Septemba 2012.
CHADEMA walikataa kusitisha ratiba ya mikutano hiyo kama inavyothibitishwa na
Justin Leornard Mpotwa Katibu wa Wilaya ya Mufindi kwa barua yake Kumb. Na
CDM/M4/002/Vol.01/2012 ya tarehe 01 Septemba 2012 kuwa “pia tunaomba
ieleweke bayana kwamba kisheria shughuli zetu hazina mwingiliano na wala
kuhusiana na program iliyoongezwa ya Sensa. Kwa barua hii tunakuarifu kuwa
mikutano tuliyokutaarifu kuifanya kuanzia kesho tarehe 02 septemba 2012
itaendelea kama ilivyopangwa - CHADEMA VEMA”.
Aidha kuwepo kwa zuio la mikutano ya Siasa ya CHADEMA Mkoani Iringa wakati wa
zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linathibitishwa na Amri ya Utendaji (Operation
Order) ya Kamanda wa Polisi Mkoa (SACP Michael Kamuhanda) ya tarehe 01
Septemba 2012. Amri ya Utendaji ambayo ni amri halali ilitolewa ili “kuzuia shughuli
za Siasa (mikutano na maandamano) kipindi cha zoezi la kitaifa la Sensa kuanzia
tarehe 25 Agosti 2012 hadi 08 Septemba 2012”. Uhalali wa Amri/Zuio hili
ulithibitishwa pia na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini katika barua yake Kumb Na. DA.
112/ 123/ 01/ 34 ya tarehe 28/08/2010 na wakati wa mahojiano na Kamati ya
uchunguzi tarehe 22 Septemba 2012.
Licha ya zuio/amri hii Viongozi wa CHADEMA walikataa kutii amri hiyo. Kutokana na
taarifa hizi, Kamati ya Uchunguzi inathibitisha kwamba hapakuwepo na uhalali wa
mkusanyiko/mkutano ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo, Wilaya ya Mufindi,
Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba 2012. Kuhusu kuwepo kwa uvunjifu wa amani
6
Kijijini Nyololo tarehe 02 Septemba 2012 Kamati ya Uchunguzi ilibaini mambo
yafuatayo:
 Tukio la kuuawa kwa Daud Mwangosi jioni ya tarehe 02 Septemba 2012
lilitokea baada ya Operesheni ya Jeshi la Polisi kumalizika. Hii ni kwa mujibu
wa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia Mkoa wa Iringa na Joseph Senga Mpiga picha/Mwandishi
Tanzania Daima.
 Kitendo cha kutotii amri halali ya Kamanda wa Polisi kuagiza wafuasi wa
CHADEMA watawanyike kutoka kwenye eneo la ofisi ya Kata ya CHADEMA
ilikuwa chanzo cha vurugu.
Uamuzi wa CHADEMA kung’ang’ana kukusanyika isivyo halali eneo la Nyololo
ikizingatiwa kuwepo kwa ujumbe wa SMS kutoka kwa Dkt. Slaa, Katibu wa
CHADEMA uliosema, “IGP nasubiri simu yako. Wajulishe Polisi wako waandae risasi za
kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha
kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya Den Hague. Ni afadhali tufe
kuliko manyanyaso haya”. Dr. Slaa. : ujumbe huu ukiashiria umwagaji wa damu ni
ushaidi tosha kuwepo kwa uvunjifu wa amani. CHADEMA ndiyo Chanzo cha vurugu na
uvunjifu wa amani Kijijini Nyololo tarehe 02 Septemba 2012.
7.2 Kama yalikuwepo makubaliano kuhusu mikutano ya hadhara au
maandamano nchini katika kipindi cha Sensa.
Katika kuzungumzia hoja hii tukianzia na Uongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa
ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi Taifa, Kamati ya Uchunguzi ilithibitisha kuwepo kwa
maagizo ya kusimamisha mikutano/maandamano ya Vyama vya Siasa wakati wa
kipindi cha Sensa ya Watu na Makazi yaliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini, na kuongezwa muda wa Sensa hadi tarehe 08 Septemba 2012 na Kamishna wa
Sensa hapo tarehe 01 Septemba 2012.
Aidha hoja hii imethibitika kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa barua
yake yenye Kumb Na DA. 112/ 01/ 34 ya terehe 28 Agosti 2012 kwenda kwa
Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa akiwasihi kusimamisha shughuli zote za
7
mikutano na maandamano ya Vyama vyao kwa kipindi chote cha Sensa ya Watu na
Makazi. Aidha kwa mujibu wa Gazeti la Serikali Na 29 VOL 93 ya tarehe 20 Julai 2012,
Mhe. Rais, JAKAYA MRISHO KIKWETE kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu
namba 14 cha Sheria ya Takwimu sura 351 alielekeza kwamba Sensa ya Watu na
Makazi itafanyika kuanzia tarehe 26 mwezi wa nane, mpaka tarehe 08 mwezi wa tisa
mwaka 2012.
Kamishna wa Sensa aliratibu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kumalizika ifikapo
tarehe 01 Septemba 2012. Hata hivyo kutokana na tathmini aliyofanya, kazi hiyo
ilikuwa imekamilika kwa asilimia 95%. Hivyo tarehe 01 Septemba 2012 alitoa taarifa kwa
Vyombo vya Habari kwamba ili kila mwananchi apate nafasi ya kuhesabiwa watu
watakaokuwa wamesalia ambao ni chini ya 5% wanaombwa kutoa ushirikiano ili zoezi
hili likamilike. Hivyo, wale wote mmoja mmoja waliobakia wataendelea kuandikishwa
hadi tarehe 08 Septemba 2012.
Kwa upande wake Inspekta Jenerali wa Polisi kwa ujumbe wa simu Kumb Na S8.7/
2/ A/ VOL XIV/ 59 ya tarehe 28/08/2012, pia simu yake Kumb Na C.28/ B/ 44 ya
terehe 01/ 09/ 2012 aliwaelekeza Makamanda wa Polisi wa Mikoa kutoruhusu
mikutano na maandamano wakati huu wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi mpaka
litakapokamilika tarehe 08 Septemba 2012.
Kimsingi Kamati ya uchunguzi imethibitisha kwamba maelekezo kwa Vyama vya
Siasa kutoendesha shughuli za mikutano ya hadhara au maandamano yalitolewa kwa
mujibu wa Sheria.
7.3 Mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu
iliyosababisha, kifo cha marehemu Daud Mwangosi na wengine kuumizwa,
na uwiano wa nguvu hiyo na tukio.
Hoja kuwa Polisi walitumia nguvu kubwa katika kudhibiti mkutano wa CHADEMA
iliungwa mkono na Viongozi wa Serikali ya Kijiji, Viongozi wa dini na Viongozi wa
siasa Kijijini Wilayani na Mkoani pamoja na Waandishi wa Habari. Hata hivyo Kamati za
Ulinzi na Usalama Wilaya na Mkoa na Viongozi wa Jeshi la Polisi waliona nguvu hizo ni
za mazingira ya hali ilivyokuwa.
8
Uchunguzi wa suala hili umebaini kwamba tarehe 02 Septemba 2012 muda wa saa
10 za jioni huko eneo la Sokoni, Kijiji cha Nyololo kulikuwepo na mkutano usio halali
ulioandaliwa na viongozi wa CHADEMA. Upo ukweli kwamba uongozi wa Polisi ulitoa
ilani kuamuru wafuasi wa CHADEMA waliokuwepo mkutanoni hapo waondoke la
sivyo nguvu itatumika. Walikaidi amri hiyo na ilipoagizwa viongozi wakamatwe
ndipo walianza kurusha mawe kwa Askari Polisi. Baadhi ya Askari walijeruhiwa,
akiwamo G 9934 PC Mgaka alivunjwa mkono wa kulia. Pia kofia (helmet) tatu
ziliharibiwa. Kutokana na hali hiyo amri ya kupiga mabomu ya machozi na ya
kishindo ilitolewa, kwa mujibu wa Kifungu 77 hadi 79 cha Kanuni za Adhabu, Sura ya
16 - R.E 2002. Operesheni hii ilimalizika baada ya kukamatwa viongozi na wafuasi
wa CHADEMA jumla yao saba.
Baada ya zoezi hilo kukamilika Askari Polisi walioshiriki kwenye Operesheni
waliamriwa kuingia katika magari tayari kwa kuondoka. Wakati Askari wakipanda
kwenye magari kishindo kikubwa kilitokea umbali wa zaidi ya mita 100 kutoka
sehemu ambayo operesheni ilikuwa inafanyika na iligundulika kwamba kishindo kile
kimesababisha kifo cha Mwandishi wa Habari Daud Mwangosi.
Upelelezi wa awali pamoja na picha za mnato unaonyesha kwamba marehemu
alikuwa amemkumbatia Mkuu wa Polisi Kituo cha Mafinga ASP Assel Mwampamba na
huku akiwa amezungukwa na Askari Polisi wasiopungua sita ambao licha ya
kumzunguka marehemu Daud Mwangosi kuna madai yaliyotolewa na mwandishi wa
Habari Joseph Senga kwamba, Askari Polisi hao walikuwa wanamshambulia
marehemu kwa kumpiga, ndipo askari mmoja aliyetambuliwa kuwa ni G 2573 PC
Pasificus Cleophace Simon alifyatua Bomu la kishindo na kusababisha kifo cha Daud
Mwangosi.
9
Tukio hili linaweza kugawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza ni
wileamapamebas(mni ya kutawanya watu na ya pili ni ile ya mauaji ya Daud
Picha Namba 15: Askari Polisi wakimpiga Marehemu Daud Mwangosi, huku
OCS M wenye kifimbo) akijaribu kuwazuia.
Mwangosi. Katika tukio la kwanza idadi ya Askari walioshiriki ni Sekisheni
Tukio hili linaweza kugawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza ni lile ya
Operesheni ya kutawanya watu na ya pili ni ile ya mauaji ya Daud Mwangosi. Katika
tukio la kwanza idadi ya Askari walioshiriki ni Sekisheni tatu ambapo ni askari
wasiozidi thelathini. Kwa maelezo yaliyotolewa na Mwandishi wa Habari mbele ya
Kamati, Bw Joseph Senga anaeleza kuwa watu walishatawanyika na hali kutulia
mara baada ya Operesheni hii kukamilika na Polisi kujiandaa kuondoka kwenye eneo
la tukio. Tukio la mauaji ya Daud Mwangosi lilisababishwa na kupigwa bomu la
kishindo.
Maswali ya kujiuliza katika tukio la mauaji ni Je, kulikuwepo na uwiano unaolingana na
tukio hili?, Je Palikuwa na uhalali wa kutumia Bomu la kishindo?, na Je, utumiaji wa
Bomu hilo ulikuwa na umuhimu?
10
Kulingana na tukio lenyewe majibu ya maswali hayo ni kama ifuatavyo:
 Hapakuwa na uwiano wa Bomu na tukio la mauaji, kwa vile utaratibu
wa matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45
na umbali mita 80 mpaka mita 100.
 Hapakuwa na uhalali wa kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la
ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia.
 Hapakuwepo umuhimu wa kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata
ingekuwa ukamataji tayari Askari Polisi wapatao sita walikuwepo eneo
la tukio.
Kwa misingi hiyo Kamati imeona kwamba nguvu iliyotumika mwanzo hadi kumaliza
Operesheni haikuwa kubwa. Kuhusu tukio la kuuawa Bw. Daud Mwangosi na
kuumizwa baadhi ya Askari Polisi halikustahili kabisa.
7.4 Madai ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa
Mkoa wa Iringa na chanzo cha uhasama huo. Aidha madai ya kuwepo kwa
orodha ya waandishi watatu (3) ambao Jeshi la Polisi limepanga
kuwashughulikia.
Katika kupata ukweli wa jambo hili, Kamati ilikutana na wanachama wa Klabu ya
Waandishi wa Habari Iringa na pia iliwahoji Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa,
Michael Kamuhanda, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Nyigesa Ramadhani Wankyo na
Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia mkoani Iringa Said Abdallah Mnunka.
Pia, wakati Kamati inakutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ilileta suala la
mahusiano kati ya Polisi na waandishi wa habari na watendaji wakuu wa serikali wa
mkoa wa Iringa.
Katika mkutano na waandishi wa habari, ilionekana kuwa katika thathmini yao
uhusiano kati yao na Polisi hapo mkoani ni mbaya sana. Walieleza matukio kadhaa ya
kunyanyaswa waandishi wa habari wakati wapo kazini, ikiwamo kupigwa, kutishiwa
kuharibiwa na kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na hata kutishiwa maisha ili wasiripoti
mambo ambayo Polisi wana maslahi nayo.
Kwa mfano, mwandishi wa habari wa Star TV, Oliver Moto alieleza Kamati kuwa:
“Waandishi wa habari hawana mahusiano mazuri na Jeshi la Polisi, na hata
11
wanapofika ofisi za Polisi huwa hawapewi ushirikiano. Kutokana na uhusiano mbaya
wanahabari walifanya maandamano tarehe 06 Machi 2012 kupinga unyanyasaji
wanaofanyiwa na Jeshi la Polisi hapa Iringa”.
Mwandishi mwingine wa habari Zulfa Shomari ambaye anaandikia gazeti la
Mwananchi alieleza kuwa kuna matukio kadhaa ambayo Polisi wamewazuia
waandishi kufanya kazi zao mojawapo ni lile ambalo Polisi walikataza kupigwa picha
tukio la kukamatwa kwa pembe za ndovu.
Kamati pia iielezwa na mwandishi wa habari wa ITV, Bw. Laurian Mkumbata mkasa wa
kuvunjwa kamera yake na OCD Iringa kwenye tukio moja. Ilibidi OCD alipe kamera
hiyo kwa maagizo ya RPC.
Pia walisema kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa hivi sasa ana mawasiliano duni sana na
waandishi wa habari na juhudi za wengi wao kumfuata ili athibitishe tukio
zimekuwa zikishindwa kwani ameweka maagizo getini kuwa mtu yeyote ambae
anataka kumuona ni lazima aeleze anataka kumuona kwa sababu gani ndipo
aruhusiwe kuingia. Kwa sababu hii waandishi wa habari wengi wamekata mguu
kwenda ofisini kwake.
Mwandishi mmoja wa Ebony FM Bw. Raymond Francis, aliiambia Kamati kuwa yeye
binafsi alitishiwa kuuawa na baada ya kuandaa kipindi kuhusiana na watu
wanaoshukiwa kufanya biashara haramu ya madawa ya kulevya ambao
wanahusiana na baadhi ya Polisi wasio waadilifu.
Mwandishi wa Habari Greyson Mgoi wa gazeti la Kwanza Jamii aliiambia Kamati
kunatukio la kuanguka kwa lori la mafuta eneo la Ifunda karibu na Mafinga ambapo
waliwakuta wananchi na polisi wakichota mafuta kutoka kwenye hilo gari. Alisema
kuwa waliamua kupiga picha tukio hilo lakini Polisi waliwakamata na kuwalazimisha
wafute hizo picha walizopiga. Kwa kuogopa shari walikubali kuzifuta na
wakaruhusiwa kuendelea na safari yao.
Waandishi wa Habari hata hivyo walibainisha kuwa uhusiano wao na Polisi hapo
mkoani ulikuwa mzuri sana kipindi cha uongozi wa RPC Advocate Nyombi. Walisema
kuwa wakati wa RPC Nyombi, alikuwa na utaratibu wa kukutana na waandishi wa
habari na pia alikuwa anafikiwa na waandishi wa habari kwa urahisi kwa simu au
12
ofisini kwake. Walisema lakini ulianza kuharibika alipohama na nafasi yake
kuchukuliwa na RPC Mangara na kuwa mbaya zaidi alipokuja Kamuhanda. Walidai
kuwa Polisi wa Iringa si waadilifu na wamekuwa wakijiona kama miungu watu.
Waandishi walieleza Kamati, kitu kilichowaudhi sana ni yale majibu yaliyotolewa na
RPC baada ya mauaji ya Daud Mwangosi ambayo yalionekana yalikuwa ni ya
kupanga ili ukweli usijulikane. Walisema kama si picha zilizotolewa na waandishi wa
habari waliokuwepo kwenye tukio, hawadhani kama umma wa Watanzania
wangepata ukweli wa tukio hilo.
Walisema tarehe 06 Machi 2012, walifanya maandamano ili kupinga manyanyaso ya
Polisi wa mkoani Iringa yaliyopokelewa na Mkuu wa Mkoa. Waandishi wa Habari
mkoani Iringa pia walionyesha masikitiko yao kuwa tangu kutokee kwa mauji ya
Daud Mwangosi, hawajapokea pole kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na watendaji wake wa
juu hata kama ni ya “kinafiki”.
Kwa upande wa pili, yaani Jeshi la Polisi, Kamati ilipata taswira tofauti. RPC
Kamuhanda alisema kuwa yeye anaona mahusiano ya Polisi na waandishi wa habari
kwa ujumla ni mzuri na yeye binafsi amekuwa akikutana na waandishi wa habari
takriban kila siku asubuhi saa nne kuwapa habari. Pia aliiambia Kamati kuwa
waandishi wa habari walishiriki kikamilifu katika kuripoti michuano ya mpira ya
Kikombe cha Kamuhanda yaliyofanyika mjini Iringa.
Msimamo huo pia ulichukuliwa na viongozi wa juu wa kiutawala akiwemo Mkuu wa
Mkoa Dkt. Christine Ishengoma, Katibu Tawala wa Mkoa Bibi Getrude Mpaka ambao
walisema kuwa hapakuwa na uhasama wowote kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na
Waandishi wa Habari. Wote wawili walisema kuwa walimfahamu marehemu Daud
Mwangosi na aliteuliwa katika kamati kadhaa za kimkoa ikiwa ni pamoja na ile ya
kuandaa Sensa ya Watu na Makazi Mkoani, Kamati ya Masuala ya Katiba ya Mkoa na
Kamati ya Kukuza Utalii ya Mkoa.
Kuhusiana na hisia kuwa Mkuu wa Mkoa na watendaji wake hawakujumuika na
waandishi katika msiba wa Daud Mwangosi, Dkt. Ishengoma alisema si kweli
hawajatoa rambirambi zao kwa kifo cha Mwangosi lakini alitoa pole kwa waandishi
wakati ameenda na IGP Mwema kijijini Nyololo na pia kupitia radio katika kipindi
kilichotayarishwa na mwandishi wa habari Francis Godwin.
13
Baada ya kuongea na pande hizo mbili, Kamati imebaini kwamba kuna walakini wa
mahusiano kati ya waandishi wa habari na baadhi ya askari polisi mkoani Iringa.
Kuhusu madai ya kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao jeshi la polisi
limepanga kuwashughulikia.
Kwenye tukio la Nyololo ambapo mwandishi wa habari Daud Mwangosi aliuawa,
mwandishi wa habari mwengine Godfrey Mushi alipigwa na Polisi na inasemekana
kujeruhiwa vibaya na baadaye kukamatwa na Polisi.
Kwa mujibu wa Joseph Senga mpiga picha/mwandishi wa habari wa gazeti la
Tanzania Daima ambaye alikuwepo kwenye tukio na kupiga picha, alimuona
marehemu akipita nyuma ya gari moja la Polisi ambalo lilikuwa na baadhi ya
wanachama wa CHADEMA. Punde tu alimwona mtu amezungurukwa na askari
akipigwa lakini hakujua ni nani na yeye aliendelea kupiga picha tukio hilo mpaka nae
alipokamatwa na Polisi watatu ambao walimwuliza kama nae anataka aende
kuungana na mtu anayepigwa pale.
Senga alisema wakati kipigo kinaendelea, kuna askari mmoja mwenye nyota tatu
(OCS Mwampamba) aliteremka kutoka kwenye gari na kwenda pale ambapo yule
mtu aliyekuwa anapigwa huku akiwaambia “mwachieni, mwachieni, namfahamu
mimi huyo ni mwandishi wa habari!”
Senga alisema mara alisikia kishindo kikubwa na wale askari ambao walikuwa
wanamshikilia walikimbia ndipo yeye akaendelea kupiga picha sasa za marehemu
Daud Mwangosi ambaye alikuwa amekwisha sambaratishwa na bomu. Alieleza kuwa
alimsikia yule askari ambaye alikuja kumsaidia marehemu Mwangosi akisema
“afande wameniuwa”, “afande wameniuwa”, akimwambia RPC ambaye alikuwa
karibu nae kwani nae aliumizwa vibaya katika mlipuko huo. Senga aliiambia Kamati
wale wote ambao walikuwa wame mzunguka marehemu kama wanavyoonekana
kwenye picha alizopiga walikuwepo wakati anapigwa.
Maelezo ya Bw. Senga yanatofautiana sana na yale yaliyotolewa na RPC na OC FFU
kuwa Marehemu alimvamia OCS Mwampamba na kuwa wale askari huenda
walidhania kuwa mkubwa wao alikuwa amevamiwa ndipo walipoamua kwenda
14
kumsaidia. OCS Mwampamba mwenyewe wakati akihojiwa na Kamati ilipokuwa
Mafinga alisema hakumbuki kitu.
Hata hivyo, kwa maelezo ya Bw. Senga, ambayo yanakubaliana na yale ya RPC na
OC-FFU, kitendo cha kupigwa na mauaji ya marehemu Daud Mwangosi kilitokea
baada ya kuisha ile operesheni ya kusambaratisha mkutano wa CHADEMA na
hapakuwa na mabishano yeyote au purukushani iliyotokea kabla ya marehemu
kuzungukwa na kuanza kupigwa.
Kwa minajili hii basi Kamati imeshindwa kubaini baada ya kumalizika operesheni na
askari Polisi kuanza kuondoka, kwa nini Mwangosi alishambuliwa kwa kipigo kabla ya
kulipuliwa na bomu la kishindo?
Kwa nini kuna maelezo yanayokinzana kati ya Bw. Senga ambaye alikuwa karibu
sana na tukio na yale ya RPC na OC-FFU ambao katika maelezo yao kwa Kamati
walisema kuwa wao walikuwa mbali kidogo na tukio kwa hiyo hawakuweza kuona kwa
dhahiri kilichotokea. Maelezeo ambayo yalirudiwa na viongozi wa juu wa Polisi ikiwa ni
pamoja na Kamishna wa Upelelezi (DCI) Robert Manumba na Inspekta Jenerali wa
Polisi, Said Mwema katika mahojiano na Kamati.
Uchunguzi wa Kamati haukuweza kupata ushahidi wa kubainisha kama kupigwa kwa
waandishi hao kulitokana na njama yeyote ya Polisi kuwashughulikia au ilitokea
kwenye purukushani ya vurugu zilizotokea baada ya FFU kuamriwa kutawanya
wanachama wa CHADEMA.
Pia Kamati haikupata ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa mauaji ya Daud
Mwangosi yalikuwa ni ya kupangwa.
Kutokana na maelezo ya hapo juu, Kamati inapendekeza yafuatayo:-
 Taasisi za habari zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari,
hususan Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri wafanye utaratibu
unaostahiki za upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi la Polisi na
uongozi wa mkoa wa Iringa. Hii itasaidia kurejesha uhusiano mzuri kati ya
vyombo hivyo muhimu katika mkoa;
 Waandishi wa habari wapewe mafunzo ya jinsi ya kuripoti matukio ya
hatari/ghasia;
15
 Waandishi wa habari wavae vivazi maalum vya kuwatambulisha wakiwa
katika matukio hasa kwenye maeneo hatarishi;
 Waandishi wa habari wafanye kazi kwa weledi, uadilifu, uwazi na
wasijibainishe na vyama vya siasa;
 Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Daud Mwangosi kabla
hajauawa wachukuliwe hatua stahiki za kisheria;
 Kamati ya Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari
iliyoanzishwa mwaka 2008 ifufuliwe. Na kamati hizo ziteremke hadi kwenye
ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.
 Viongozi wa polisi wanapotoa taarifa za tukio, ziwe zimefanyiwa utafiti wa
kina ili zisipotoshe jamii.
7.5 Uwepo wa Sheria, Kanuni au Taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la
Polisi kuzuia mikusanyiko inayoitishwa na Vyama vya Siasa na Mamlaka ya
Rufaa ambapo Vyama hivyo havitaridhika na amri hiyo.
Sheria Namba 5 ya 1992 kama ilivyorekebishwa na Sheria Namba 7 ya 2009
inaratibu mahusiano ya kiutendaji kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa. Kwa
mujibu wa Sheria hii Jeshi la Polisi limepewa madaraka ya kutoa zuio kwa maandishi
na kuweka bayana sababu za kuzuia mikutano au maandamano. Zuio aina hii ni
halali kwa mujibu wa Sheria na ni sherti Chama cha Siasa kiheshimu na kutii. Fungu
la 11 vifungu vidogo Na 1, 4, 5, 6, 7 na 8 ya Sheria ya Vyama vya Siasa likisomwa
pamoja na mafungu Namba 43, 44, 45 na 46 ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Auxiliary
Forces Act Sura 322 vitatumika kusimamia uendeshaji mikutano ya Vyama vya Siasa
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na kwamba Vyama vya Siasa
vinatakiwa kutoa taarifa na siyo kuomba idhini, Jeshi la Polisi limepewa uwezo na
madaraka juu ya mikutano hiyo kuhusu kuzuia au kuruhusu na au kutoa maelekezo
stahiki, kama vile kupendekeza, na kushauri eneo mbadala na tarehe tofauti ya
kufanya mikutano/maandamano. Aidha kutotii amri/zuio ya Jeshi la Polisi ni kosa la
Jinai kwa mujibu wa Fungu la 74 la Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura 16 RE.
Vilevile kwa mujibu wa Fungu la 43 (6) ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Auxiliary
Forces Act, Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye Mamlaka ya Rufaa dhidi ya amri/zuio
linatolewa na Jeshi la Polisi.
16
Pamoja na kuwepo kwa Sheria hizi mbili bado kuna mapungufu katika uendeshaji na
usimamizi wa shughuli za Siasa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Kwa mfano
pamoja na madaraka aliyonayo Msajili wa Vyama vya Siasa ya kukifuta Chama cha Siasa
kwenye rejesta ya usajili kwa mujibu wa Fungu la 19 na 20 ya Sheria ya Vyama vya
Siasa, kusimamisha utoaji wa ruzuku na matumizi yake, uratibu wa shughuli za
vyama hivyo hauko mikononi mwake.
Wadau wanashauri umuhimu wa kuimarisha uhusiano katika shughuli za utendaji kati
ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi ili kudumisha utulivu na amani
na utii wa sheria bila shuruti kwa upande mmoja na kukuza mfumo wa Demokrasia
ya Vyama Vingi vya Siasa kwa upande mwingine.
7.6 Hali ya mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa nchini
katika utendaji kazi wao na Utii wa Sheria.
Kamati ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Daud
Mwangosi katika kupata majibu kwa hadidu hii ya rejea, ilizungumza na viongozi wa
vyama vya siasa kutoka ngazi za Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa
na Viongozi wa kitaifa jijini Dar es Salaam na viongozi wa dini kutoka ngazi za Kijiji cha
Nyololo, Wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa.
Kwa ujumla, kila kiongozi wa chama cha siasa wa ngazi zote ambaye Kamati
imezungumza naye kuhusu hadidu hii ya rejea, ameelezea umuhimu wa Jeshi la
Polisi katika kulinda usalama wa raia na mali zao na wangependa jeshi hilo liachwe huru
katika kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa na wanasiasa ili lifanye kazi zake
kwa weledi na uadilifu.
Hata hivyo taswira iliyojitokeza ni kwamba kuna mgawanyiko wa mtizamo kuhusu
jinsi Jeshi la Polisi linavyoshughulikia mikutano/maandamano ya Vyama vya Siasa.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wanaamini kuwa Jeshi la Polisi
linakipendelea Chama cha Mapinduzi na kubinya vyama vya upinzani, huku viongozi
wa CCM kutoka ngazi ya kijiji hadi Taifa wakilisifia Jeshi hilo kuwa linafanya kazi
yake vizuri na kwa weledi mkubwa.
Mgawanyiko wa taswira kuhusu madai kuwa Jeshi la Polisi kuipendelea CCM hauko
tu kati ya vyama vya upinzani na CCM bali pia kwa viongozi wa dini kuanzia ngazi za
17
kijiji, wilaya hadi mkoani Iringa kwa maelezo kuwa hawajasikia hata siku moja mtu
anauawa na Polisi kwenye mkutano wa CCM. Mwandishi mmoja alitoa udadisi wake
kuwa huwa wanapata shida sana kuandika habari za mikutano ya CHADEMA
kutokana na jinsi Polisi wanavyojipanga kwenye mikutano ya chama hicho.
Kudhihirisha umuhimu wa Jeshi la Polisi katika jamii, hata wale wanaolituhumu kuwa
linakipendelea CCM, katika kutoa maoni yao kuhusu hatua za kuchukuliwa askari
wanaoharibu sifa ya Jeshi hilo, wanapendekeza kuwa askari wahusika wachukuliwe
hatua na kuomba Jeshi hilo liendeshwe kwa weledi hasa inapotokea askari
akalazimika kutumia silaha kukabiliana na fujo isifikie kuua.
Kwa mfano, Mchungaji Peter Katanga wa Revival Baptist Church, alishauri chombo cha
Polisi kisitumike kufanya mauaji, au kisitumike na mtu, watu, au kikundi chochote
kufanya matendo yasiyo mazuri kwa jamii kwa sababu chombo hicho kipo kwa ajili ya
kulinda usalama wa raia wote na mali zao.
Viongozi wa siasa wengine bila kujali itikadi zao, wameonekana kukerwa sana na
tabia ya watu kuuawa wakati Jeshi la Polisi linatuliza ghasia na hii ikiachiwa iendelee
inaweza kuleta uvunjifu wa amani katika nchi. Kwa mfano, Mchungaji wa Kanisa la
EFATA Nyololo, Mkombozi Kiliwa alishauri Polisi watumie njia zinazofaa kukabiliana na
wanaovunja sheria na si kuua.
Pia Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyololo, Obby Kimbale, alielezea kutokukubaliana
kwake na kitendo cha mauaji ya Daud Mwangosi, alipendekeza elimu ya uraia
itolewe kwa jamii nzima vikiwemo vyombo vya dola, viongozi wa serikali, wanasiasa na
wananchi kwa ujumla wao ili kila mtu kwa nafasi yake akaelewa namna ya kutimiza
wajibu wake ndani ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Kwa upande mwingine, wengi waliotoa maoni yao juu ya mahusiano ya Polisi na
vyama vya siasa, pamoja na kulaumu Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa katika
kukabiliana na wafuasi wa CHADEMA, pia waliwalaumu viongozi wa chama hicho,
kwa kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi hatimaye kusababisha Polisi kutumia nguvu
kiasi hicho.
Kitendo cha kuuawa kwa Mwandishi wa Habari, Daud Mwangosi na tabia ya kutokea
mauaji katika mikutano ya CHADEMA kimeonekana kuwakera viongozi wengi wa
18
vyama vya siasa kwani wanaamini kuwa Polisi huwa wanatumia nguvu kubwa kupita
kiasi ‘wanapotuliza ghasia’ katika mikutano ya CHADEMA.
Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa, Zakaria Mwansasu alielezea sababu ya matukio ya
namna hii kuwa ni kutokana na mmomonyoko aliouita mkubwa wa maadili hasa
katika vyama vya siasa na akashauri viongozi wa vyama vya siasa wakapewa elimu
ya uraia.
Maoni mengi ya viongozi wa vyama vya siasa yamejikita zaidi katika hofu ya nchi
kuingia kwenye vurugu na kutoka kwenye kisiwa cha amani na hivyo kutoa uashauri
kwa viongozi wa vyama vya siasa na Jeshi la Polisi kuweka mbele maslahi ya taifa.
Mchungaji Yokonia Koko wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), alielezea
ukosefu wa maadili kwa baadhi ya askari Polisi kuwa umetokana na jeshi hilo kuajiri
vijana ambao hawana maadili na kwamba watuhumiwa wa mauaji kwenye matukio
yanayolihusisha Jeshi la Polisi wakati wa kuzuia fujo katika mikutano/maandamano
ya vyama vya siasa wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa askari wengine.
Kasi ya CHADEMA kuendesha mikutano katika sehemu mbalimbali nchini kwa ajili ya
kujiimarisha kichama, imepokewa kwa hisia tofauti na vyama vingine vya siasa.
Wakati kuna makundi ya watu katika jamii wakidhani kuwa hiyo ni haki yao kama
chama cha siasa kinachotaka kukua na kukubalika kisiasa, wengine wanaiona
mikutano hiyo ya hadhara ya CHADEMA kama ni kuwapunguzia muda wa kufanya
shughuli zao za maendeleo hasa baada ya kipindi cha uchaguzi kumalizika.
Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama, alishauri kufanyiwa marekebisho kwenye
sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992 itakayoweka wazi shughuli za
vyama vya siasa baada ya Uchaguzi Mkuu. Alisisitiza kuwa shughuli za siasa baada
ya Uchaguzi Mkuu zihamie bungeni kwa wanasiasa kuhoji mipango ya maendeleo ya
serikali na matumizi ya rasilimali za nchi na wananchi waachwe wachape kazi zao za
maendeleo.
Kuhusu Jeshi la Polisi, Mukama alisema mfumo uliopo wa Jeshi hilo unalifanya
lionekane la kitaifa zaidi na kushauri libadilishwe kimuundo ili liweze kutandaa hadi
serikali za mitaa kuongeza nguvu katika mpango wa ulinzi shirikishi ulioanzishwa na
Jeshi hilo.
19
Mwanasiasa John Shibuda alizungumzia mahusiano kati ya vyama vya siasa na Jeshi la
Polisi kwa kutoa lawama kwa vyama vya siasa kuwa havitoi malezi kwa
wanachama wake ambayo yatawafanya wawe waadilifu, wazalendo, waaminifu na
watiifu wa sheria.
Alisema vyama vya siasa havina mfumo wa kujihakiki, kujikosoa na kujiwajibisha na
akapendekeza kuanzishwa kwa mfumo huo kisheria ambao utawajibisha vyama vya
siasa kwa matendo ya viongozi au wanachama wao.
Shibuda alifafanua kwamba sheria anayopendekeza iwe na nguvu ya kutoa adhabu
kwa chama cha siasa na kwa kiongozi au mwanachama ambaye atathibitika kuwa
ndiyo chanzo cha uvunjifu wa amani.
Kuhusu Jeshi la Polisi mwanasiasa huyo alipendekeza kufanyike kwa marekebisho ya
utendaji ili wakuu wa wilaya na mikoa waondolewe nguvu za kiutawala ambazo
huwafanya wakati mwingine kutoa maagizo ya kisiasa kwa Jeshi la Polisi na
hatimaye kulifanya Jeshi hilo lionekane linatekeleza maslahi ya wanasiasa badala ya
kuwa chombo cha kulinda amani.
Kwa ujumla Kamati kutokana na maelezo mbalimbali ya Viongozi wa Vyama vya Siasa
na Jeshi la Polisi, imeona kuwa kuna mahusiano hafifu kati ya baadhi ya Vyama vya
Siasa na Jeshi la Polisi.
Kwa kuwa taasisi zote hizi ni wadau muhimu wa amani na utulivu nchini, Kamati
inapendekeza:
 Kuwe na jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na
Vyama vya Siasa ili kila upande ujue wajibu wake na wa taasisi nyingine
katika kudumisha amani ya nchi na utamaduni wa kuheshimu sheria zilizopo
na kupunguza migongano.
 Kuhusu madai kwamba mauaji yanayotokea nchini yaundiwe Tume, Kamati
imeona kuwa zipo sheria zinazotoa mamlaka ya kutafiti au kuchunguza
endapo kuna mashaka ya kifo hicho.
 Muundo uliopo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya kisheria ili kuziba mianya
inayotoa nafasi kwa wanasiasa kulitumia Jeshi hilo kwa manufaa ya kisiasa.
20
 Nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kiutendaji ziangaliwe upya ili
zisitumike na mhusika kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.
 Kwa kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwa ndiye mlinzi wa usalama wa raia na
mali zao, siasa za ubabe kwa vyama vya siasa ziepukwe kwa kuwa zinaleta
msuguano usio wa lazima na Jeshi la Polisi
21
8.0. MAONI NA MAPENDEKEZO:
Kutokana na uchunguzi uliofanyika kupitia mahojiano na Viongozi wa kada
mbalimbali, kuanzia ngazi ya Kijiji, Wilaya, Mkoa hadi Taifa, Kamati ina maoni na
mapendekezo yafuatayo:
MAONI:
 Kuhusu madai kwamba mauaji yanayotokea nchini yaundiwe tume, Kamati
imeona kuwa zipo sheria zinazotoa mamlaka ya kutafiti au kuchunguza
endapo kuna mashaka ya kifo hicho.
 Nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kiutendaji ziangaliwe upya ili
zisitumike na mhusika kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.
 Kwa kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwa ndiye mlinzi wa usalama wa raia na
mali zao, siasa za ubabe kwa vyama vya siasa ziepukwe kwa kuwa zinaleta
msuguano usio wa lazima na Jeshi la Polisi
 Kuhusu operesheni ya uzuiaji wa mkutano wa CHADEMA usio halali Kijijini
Nyololo tarehe 02 Septemba 2012, Jeshi la Polisi lilitekeleza wajibu wake
ipasavyo na kutumia nguvu sahihi. Operesheni iliyoandaliwa na kufanyika
ilikamilika kwa kuwatawanya watu waliofika kwenye mkutano, kukamata
baadhi ya Viongozi na wafuasi wa CHADEMA na hali ya utulivu ilirejea kwenye
eneo husika.
MAPENDEKEZO
 Mauaji ya mwandishi wa habari Daud Mwangosi yalitokea baada ya
operesheni kumalizika, na amri ya kuondoka kwa askari eneo la tukio
kutolewa na Viongozi wa operesheni hiyo
 Jamii wakiwemo Viongozi waelimishwe umuhimu wa utii wa sheria, kanuni na
taratibu ili kudumisha amani na utulivu hapa nchini. Viongozi wengi
walionyesha hofu ya kuliingiza Taifa kwenye machafuko makubwa na uvunjifu
22
wa amani iwapo jamii haitazingatia umuhimu wa kutii sheria, kanuni, taratibu na
amri halali za Mamlaka.
 Msajili wa Vyama vya siasa afafanue majukumu ya vikundi vya Ulinzi vya
Vyama vya Siasa kama vile Green Guard, Red Brigade, Blue Guard.
 Iwepo programu mahususi ya Elimu ya Uraia nchini ili kujenga uzalendo na
kukuza maadili ndani ya jamii wakiwemo viongozi wa kada mbalimbali. Hivi
sasa jamii inashuhudia kutoweka kwa uzalendo na kuwepo kwa mmomonyoko
wa maadili ndani ya jamii.
Njia zifuatazo zitumike:
- Elimu ya uraia iimarishwe katika mitaala ya elimu kuanzia Shule za msingi
hadi Vyuo Vikuu.
- Uamuzi wa kurudisha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana
utekelezwe mapema.
- Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Tasnia ya Habari na Taasisi
zisizokuwa za Serikali zishiriki kikamilifu katika uenezi wa Elimu ya Uraia
nchini.
- Kuhimiza uzingatiaji wa weledi katika utendaji kazi kwa mujibu wa taaluma
na miongozo inayotolewa kuleta ufanisi. Aidha elimu endelevu sehemu za
kazi itiliwe mkazo.
 Kufanya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya 1992 ili kuweka
wazi shughuli za Vyama vya Siasa baada ya Uchaguzi Mkuu. Lengo ni kuwa
Shughuli za Siasa zihamie Bungeni kujadili na kuhoji mipango ya Serikali na
matumizi ya rasilimali za nchi. Kwa kufanya hivyo wananchi watapata nafasi
kufanya kazi za maendeleo.
 Kuboresha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, hususan uanzishwaji
wa ofisi ngazi ya Mkoa na Wilaya ili kuratibu ushirikiano/mahusiano baina ya
serikali (Jeshi la Polisi) na Vyama vya Siasa. Lengo ni kukuza mahusiano na
kuondoa mgongano.
 Utaratibu wa kufanya mikutano mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na
Vyama vya Siasa, Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari uimarishwe ili
kujenga mahusiano mazuri na kupata ufumbuzi wa haraka kwa matatizo
yaliyojitokeza.
23
 Jeshi la Polisi nchini ni chombo muhimu katika ulinzi na usalama wa raia na
mali zao. Muundo uliopo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya Kisheria ili kuziba
mianya inayotoa nafasi kwa wanasiasa kulitumia Jeshi hilo kwa manufaa ya
Kisiasa. Aidha mipango ya kuboresha utendaji kazi kitaaluma iliyopo hivi sasa
upewe msukumo stahiki hususan rasilimali watu na fedha.
 Wananchi wahamasishwe kushirikiana na Polisi Jamii na Ulinzi shirikishi. Polisi
ishirikiane na Serikali za mitaa kufanikisha malengo hayo.
 Jeshi la Polisi liimarishwe ili litekeleze majukumu yake kikamilifu na kujenga
mahusiano sahihi kati yake na Jamii, Vyama vya Siasa, Tasnia ya Habari na
Asasi zisizo za Kiserikali.
 Taasisi za habari zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari,
hususan Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri wafanye utaratibu
unaostahiki wa upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi la Polisi na
uongozi wa mkoa wa Iringa. Hii itasaidia kurejesha uhusiano mzuri kati ya
vyombo hivyo muhimu katika mkoa.
 Waandishi wa habari wapewe mafunzo ya jinsi ya kuripoti matukio ya
hatari/ghasia.
 Waandishi wa habari wavae vivazi maalum vya kuwatambulisha wakiwa
katika matukio hasa kwenye maeneo hatarishi.
 Waandishi wa habari wafanye kazi kwa weledi, uadilifu, uwazi na
wasijibainishe na vyama vya siasa.
 Kamati ya Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari
iliyoanzishwa mwaka 2008 ifufuliwe. Na kamati hizo ziteremke hadi kwenye
ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.
 Viongozi wa Polisi wanapotoa taarifa za tukio, ziwe zimefanyiwa utafiti wa
kina ili zisipotoshe jamii.
 Kuwe na jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na
Vyama vya Siasa ili kila upande ujue wajibu wake na wa taasisi nyingine
katika kudumisha amani ya nchi na utamaduni wa kuheshimu sheria zilizopo
na kupunguza migongano.
24
9.0. CHANGAMOTO
Changamoto zilizojitokeza katika Uchunguzi zimegawanyika katika mtiririko ufuatao:-
9.1 Jeshi la Polisi:
- Ukosefu wa Mafunzo endelevu.
- Ukosefu wa Uvumilivu katika utekelezaji wa Majukumu. -
Uelewa mdogo wa Elimu ya Uraia.
- Mmomonyoko wa Maadili.
- Kukosekana kwa uzalendo.
- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu
9.2 Vyama vya Siasa:
- Kukosekana kwa uvumilivu katika kuendesha shughuli za Siasa. -
Kukosekana kwa Elimu ya Uraia
- Uelewa mdogo wa baadhi ya Viongozi wa Vyama kuhusu uendeshaji wa
Vyama vya Siasa.
- Ukosefu wa Sera/Mwongozo kwa Vyama vya Siasa kuendesha shughuli za
Kisiasa baada ya uchaguzi mkuu.
- Kukosekana kwa Jukwaa linalokutanisha mara kwa mara Vyama vya Siasa
na Jeshi la Polisi
- Mmomonyoko wa Maadili.
- Suala la Uzalendo.
- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu
25
9.3 Jamii:
- Elimu ya Uraia.
- Mmomonyoko wa Maadili.
- Kukosekana kwa uzalendo.
- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu.
26
10 HITIMISHO
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake aliwahi kusema
kuwa, “ili nchi iendelee inahitaji vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na
uongozi bora. Watanzania kila mtu mahali pake, tunahitaji kuwa na siasa safi yenye
kujenga ustawi, tija, mshikamano, amani, maendeleo na afya kwa taifa letu”.
Utulivu na amani kwa ajili ya mustakabali wa taifa, imekuwa ni kauli mbiu ya
viongozi mbalimbali ambao Kamati hii imepata fursa ya kuzungumzia juu ya hali ya
siasa na mahusiano yaliyopo baina ya Serikali, (Jeshi la Polisi, Kamati za Ulinzi na
Usalama wilaya na mkoa), vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi.
Wananchi na Viongozi wanataka kuona shughuli za siasa ya vyama vingi
inaendeshwa kwa hoja zenye tija badala ya vurugu na utengano. Njia mojawapo ya
kukabiliana na hali hii inayojitokeza ni kujenga uzalendo, maadili mema, na
mshikamano ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani na utulivu.
Kamati hii inashauri na kupendekeza kuwa maoni haya yazingatiwe na kutekelezwa.
Aidha Kamati imefaidika sana kupata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali
kuanzia kijiji hadi taifa na walitoa ushirikiano wa dhati katika kutoa mchango wao wa
mawazo. Kamati inapenda kutoa shukrani za dhati kwa Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi Mhe. Dkt Emmanuel Nchimbi (Mb) kwa imani yake kwa wajumbe wa Kamati
ya Uchuguzi.
27

No comments: