Friday, November 2, 2012

Mbunge aliyenaswa akitoa rushwa kashinda uchaguzi

Mussa Zungu (kushoto) akizungumza na Waziri Mkuu Mizengo Pinda

 Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM) ambaye usiku wa kuamkia juzi, alipatwa na mkasa wa kukamatwa na Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kujihusisha kwa rushwa ameshinda nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuuu NEC kupitia Jumuiya ya Wazazi.

Zungu alikamatwa Jumanne usiku kwa tuhuma za kugawa rushwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu ili wampigie kura, tuhuma ambazo hata hivyo alizikanusha.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo usiku wa kuamkia jana, Wassira alisema Zungu alipata kura 402 akishika nafasi ya pili, nyuma ya Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima aliyeongoza kundi hilo kwa kupata kura 531.



Mshindi mwingine ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza aliyepata kura 448, wakati kutoka Zanzibar walioshinda ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima na Fatma Abeid Haji.

Katika uchaguzi huo, kiongozi wa wasimamizi wake ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira alimtangaza Abdallah Majura Bulembo kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi.

Bulembo alipata kura  677 na kuwashinda kwa mbali wapinzani wake ambao ni Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata aliyepata kura 192 na  Kapteni Mstaafu, John Barongo aliyeambulia kura 42.

Hata hivyo, wakati akitoa shukrani kwa wajumbe kwa kumchagua, Bulembo alieleza kutofurahishwa na washindani wake kukataa kusaini matokeo ya kura hizo na kukiita kitendo hicho kuwa siyo cha kiungwana.

Wakati akitoa lawama hizo, Barongo na Mlata hawakuwapo ukumbini na hata walipoitwa kwa ajili ya kuzungumza baada ya matokeo kutangazwa, hawakutoke

Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Dogo Idd Mabrouk alifanikiwa kuitetea katika uchaguzi wa duru ya pili kwa kura 417 na kuwashinda  wagombea wenzake  Ally Issa Ally na Hassan Rajab Khatibu .

Nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu Tanzania Bara walioshinda ni Dk Godbertha Kinyondo, Saumu Mohamed Bendera, Deogratias Rutta, Masudi Bwire na Juliana Chintika.

Nafasi ya uwakilishi wa Mkutano Mkuu katika Jumuiya ya Wanawake (UWT) aliyeshinda ni Godlever Kamala na uwakilishi katika Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) aliyeshinda ni William Malecela.

Kikwete akemea
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amesisitiza kuwa chama hicho lazima kichukue hatua za kutokomeza vitendo vya rushwa katika chaguzi zake.

Mbali na hilo, Rais Kikwete amewataka viongozi wapya wa Jumuiya ya Wazazi kuthibitisha kwa vitendo kwa nini jumuiya hiyo isifutwe kutokana na kushindwa kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.

Akifunga mkutano wa Jumuiya hiyo jana, Kikwete alisema: “Sisi ni watu wazima na tumekuwa tukiendekeza tabia hii na wengine mpo hapa, unapewa shilingi 30,000, unapewa Sh70,000, hii ni hatari kwani athari zake haziishii ndani ya chama pekee bali katika jamii yetu nzima.”

Kuhusu jumuiya hiyo, alisema chama hakiwezi kuendelea kuibeba kwani kumekuwa na malalamiko kwamba haina tija na badala yake imegeuka mzigo kwa CCM.

Rais Kikwete alisema katika vikao vyote vya Nec kumekuwa na hoja inayotaka Jumuiya ya Wazazi ifutwe lakini yeye akiwa mwenyekiti amekuwa akijitahidi sana kuikingia kifua.

Alizungumzia kwa undani ubadhirifu wa mali za Jumuiya hiyo zikiwamo fedha na kuuzwa kwa baadhi ya majengo ya kihistoria, kwamba ni suala linalomkera hivyo kuwaagiza viongozi wapya kulifanyia kazi.

Alitoa mfano wa majengo ya kilichokuwa chuo cha wapigania uhuru wa chama cha ukombozi wa Msumbiji, Frelimo kilichopo Kaole  Bagamoyo kwamba yameuzwa na kubadilishwa matumizi yake.

“Pale waliwahi kufundisha akina Mzee Chissano (Joachim) na Mzee Geubuza (Armando), sasa leo wazee hao wakija hapa kwetu wakasema wanataka kuona chuo chao, utawaambia nini?”alihoji Kikwete.

Kuhusu shule zinazomilikiwa na jumuiya hiyo, Rais Kikwete alisema: “Shule zenu zimekuwa ndiyo mzizi wa fitina, kusikia taarifa za ubadhirifu wa fedha za shule limekuwa ni jambo la kawaida, shule zenu nyingi hazifanyi vizuri na hazitoi elimu bora,” alisema.