Thursday, November 1, 2012

Mbunge Mussa Azzan Zungu mbaroni kwa rushwa



Mussa Azzan Zungu
MMOJA wa Wenyeviti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu pamoja na makada wengine wa CCM, juzi usiku walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Dodoma kwa tuhuma za rushwa

Habari zilizopatikana mjini Dodoma juzi usiku zinasema, Zungu alikamatwa saa 4.30 katika moja ya vituo vya mafuta akidaiwa kujaribu kutoa rushwa ya Sh100,000 kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmari, jana alikiri kuwakamata baadhi ya watu wakijihusisha na vitendo vya rushwa akiwamo Zungu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mmari alidai kuwa vijana wake walimtia nguvuni Zungu juzi saa tatu usiku katika Hoteli ya Golden Crown akiwa na wapambe wake wakiendelea kugawa fedha kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wazazi.

Alisema taarifa za Zungu kudaiwa kugawa fedha hizo walizipata juzi mchana na kuanza kufuatilia nyendo zake ambazo zilionyesha kuwa na dalili zote za rushwa.

“Tuliweka mitego yetu kila mahali ndipo tukabahatika kukutana naye katika eneo la hoteli hiyo akiwa na magari mawili, moja ikiwa ni teksi ya kawaida na nyingine ikiwa ni Prado ambayo ndiyo ilisadikiwa kubeba pesa,” alisema Mmari.

Kamanda huyo alidai kuwa kiasi cha fedha kilichokuwa kikitolewa na Zungu kilikuwa Sh100,000 kwa kila mjumbe ili kumshawishi ampigie kura.

Hata hivyo, alisema hawakuweza kumkamata moja kwa moja akitoa na hata fedha hizo hawakuzikamata kwani maofisa wa Takukuru walizingira gari dogo wakati fedha hizo zinasadikiwa zilikuwa katika Prado ambalo baada ya vurugu hizo lilitokomea kusikojulikana.

Akizungumzia madai hayo Zungu alisema: “Kwanza niseme kuwa si kweli kwamba nimekamatwa nikitoa rushwa, nilikuwa katika kituo kimoja cha mafuta wakaja watu ambao walisema wana shaka na gari langu.”
Aliendelea: “Samahani, halikuwa gari langu, bali ilikuwa ni teksi, mimi nikawaruhusu, wakaingia wakafanya ukaguzi na waliporidhika wakaniachia nikaondoka.”

Chanzo Mtando wa gazeti la Mwananchi.

No comments: