Thursday, December 20, 2012

Kaboyonga azikwa Kikwete ahudhuria Mazishi


Waombolezaji wakiubeba mwili wa Marehemu Siraji Kaboyonga

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete asubuhi ya leo ameungana na mamia ya waombolezaji kumzika aliyepata kuwa Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Hayati Siraji Juma Kaboyonga.

Marehemu Kaboyonga ambaye amezikwa kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam, alifariki dunia usiku wa Jumanne ya wiki hii kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ugonjwa wa moyo akiwa na umri wa miaka 63.

Miongoni mwa waombolezaji walioshiriki mazishi ya leo ya Marehemu Kaboyonga, ambaye mpaka kifo chake alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), alikuwa Rais wa Awamu ya Pili ya Uongozi wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi.

Marehemu Kaboyonga alikuwa Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi kati ya 2005 na 2010 na katika salamu zake za rambirambi jana, Rais Kikwete alimwelezea marehemu kama mtumishi wa umma wa mfano wa kuigwa ambaye uwezo wake wa uongozi ulijionyesha dhahiri wakati wa kipindi chake cha ubunge na kwenye nafasi nyingine za umma alizopata kuzishikilia katika maisha yake.


No comments: