Sunday, February 17, 2013

Pengo anaweza kuwa Papa baada ya Papa Benedict


Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo


Papa Benedict wa XVI
Kuna uwezekano Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akachaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa kanisa hilo duniani anayejulikana kama Baba Mtakatifu au Papa.

Kardinali Pengo anatajwa kuweza kuchaguliwa kuwa Papa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo nafasi yake ya ukardinali, inayomweka kwenye mazingira ya kuwa mmoja wa watakaomchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki duniani, ambapo kwa mujibu wa sheria za kanisa hilo yeyote mwenye cheo hicho, anaweza kuchaguliwa kuwa Papa.


Wakizungumza katika mahojiano waumini wa kanisa hilo nchini, wakiwamo walei, mapadri na maaskofu walimtabiria Kardinali Pengo kushika nafasi hiyo ya juu katika Kanisa Katoliki.

Walisema kuwa kuna sababu za msingi zinazowezesha Kardinali Pengo kutwaa nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake katika kazi mbalimbali pamoja na uongozi wa kanisa akishika nafasi mbalimbali kitaifa na kimataifa.

Kwa sasa Kardinali Pengo ni mjumbe pekee kutoka Afrika kwenye Kamati ya Uenezi wa Imani Duniani, ambayo kwa jina la kilatini inajulikana kama Propaganda Fidei.

Kamati hiyo ambayo ina wajumbe tisa kutoka duniani kote ilikuwa ikiongozwa na Kardinali Joseph Ratzinger, ambaye ndiye Papa anayestaafu kwa sasa.

Akitoa maoni yake aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Joseph Selasini alisema kuwa kila nchi duniani ina nafasi ya kutoa Papa Tanzania pia ikiwemo.

Alisema kuwa Kardinali Pengo anaweza kupata nafasi hiyo kwani sheria ya Kanisa Katoliki inasema kuwa kardinali yeyote kutoka duniani kote ni moja ya watu watakaopigiwa kura hivyo kuweza kuwa Papa.

Alisema: “Kwa kawaida nafasi hiyo inawakutanisha makardinali wote duniani, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki mjini Roma. Hapo kila mmoja anakaa kwenye chumba chake na kupigia kura jina analolijua yeye.”

Alisema kuwa uchaguzi wa Papa hauna kampeni tofauti na uchaguzi wa kisiasa na kwamba Papa anaweza kupatikana ikiwa mmoja wa makadinali atakuwa amepata theluthi mbili ya kura zitakazopigwa na ikiwa tofauti na kiwango hicho cha kura uchaguzi unaweza kurudiwa.

Akizungumzia zaidi kuhusu nafasi ya Kardinali Pengo alisema kuwa anaweza akapata nafasi hiyo kwani hata yeye ni mmoja ya washiriki wa nafasi hiyo mwenye uzoefu mkubwa wa kuongoza kanisa.

“Yeye ni Mwafrika pekee ambaye ni mjumbe wa wajumbe wa Kamati ya Uenezi wa Imani ya Kanisa Katoliki hilo kati ya wajumbe tisa duniani,” alisema Selasini.

Naye Padri Nicolaus Masamba alisema: “Kila kitu ni mipango ya Mungu na kwamba Mungu akipenda Kardinali Pengo atakuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani.

Aliongeza: “Sisi tunamwombea Mungu kwani kila Kardinali kutoka duniani kote anaweza kuchaguliwa kuwa Papa, sasa kwa jambo hilo, Mungu ndiye anapanga yote, ngoja tusubiri tuone itakavyokuwa.”

Morogoro
Waumini wa kanisa hilo mkoani Morogoro wamekuwa na maoni tofauti juu ya mchakato wa uchaguzi wa Papa mpya na jinsi wanavyomtazamia Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuwa na uwezekano wa kushika nafasi hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti waumini hao walisema kuwa uchaguzi wa safari hii utakuwa wa kihistoria kwa kuwa utakuwa wa 266 ukifanyika baada ya Papa Benedict XVI, kutangaza kujiuzulu wadhifa huo ifikapo Februari 28.

Mmoja wa waumini hao, Bonventure Mtalimbo, alisema kuwa uchaguzi wa Papa hufanywa na makadinali kwa msaada wa Roho Mtakatifu akieleza kuwa yeyote kati ya makadinali 117 watakaopiga kura anaweza kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Alisema kuwa utaratibu uliowekwa wa kumchagua Papa unampa fursa kardinali yeyote kuchaguliwa kushika wadhifa huo na kumtaja Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuwa anaweza pia kuchaguliwa kwa vile ana sifa na ndiyo maana aliteuliwa kuwa kardinali.

Mtalimbo alisema kuwa Kardinali Pengo ni mtu mwenye misimamo kama ilivyokuwa kwa Papa Benedict XVI, ambaye bado anaiishi misingi, sheria na mapokeo ya Kanisa Katoliki bila kupenda kupindisha mambo.

Alisema kwa kuwa, inawezekana kabisa jina la Kardinali Pengo likapendekezwa na walio wengi kwa mujibu wa mapenzi ya Roho Mtakatifu na atakuwa Papa wa kwanza Mwafrika mweusi kushika nafasi hiyo.

Hata hivyo, Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbinga, Johm Ndimbo alipotakiwa kutoa maoni kuhusu suala hilo kwa njia ya simu aligoma kuzungumza chochote akimtaka mwandishi aende ofisini kwake akiwa na vitambulisho vyake ili aweze kujiridhisha.

Kwa upande wake Padri Rogers Haule kutoka Parokia ya Ifinga Songea Vijijini alisema: “Kardinali Pengo ni kiongozi mkubwa aliyefanikiwa kuongoza waumini wa taifa hili, anaweza pia kuongoza waumini wa dunia nzima.”

Source: Mwananchi

No comments: