Sunday, May 26, 2013

Jeshi latuliza ghasia Mtwara


Hatimaye Soko Kuu la Mjini Mtwara limefunguliwa baada ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kutwaa jukumu la kulilinda ili wananchi wapate huduma muhimu za chakula.
Mkuu wa vikosi vya aridhini wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali SM Kijuu amewahakikishia ulinzi wafanyabiashara hao, baada ya kukutana na uongozi wa Chama cha Wafanyabiashara Sokoni (Wabisoco) jana asubuhi, kufuatia wafanyabishara hao kudai kuendelea kusitisha biashara zao kwa kuhofia usalama.
Katibu wa Wabisoco, Saidi Namata ameliambia Mwananchi Jumapili kuwa wafanyabiashara hao wamekubaliana kufungua biashara zao, baada ya makubaliano ya kulinda eneo hilo na askari wa JWTZ.

“Sisi wafanyabiashara tulikuwa tayari kuendelea kusitisha huduma kutokana na hali ya usalama kuwa mbaya, alipokuja kiongozi wa jeshi na kutuhakikishia kuwa dhamana ya ulinzi itakuwa chini yao tulikubaliana,” alisema Namata
Alisisitiza: “Kama ulinzi ungekuwa mikononi mwa polisi, katu tusingefungua. Polisi wenyewe ndiyo hawa wanaovunja maduka na kuiba, kwa kuwa dhamana hii imebebwa na wanajeshi hatuna shaka, tunaomba wafanyabiashara wengine wafungue biashara zao.”
Tangu juzi magari ya matangazo yamekuwa yakipita mjini Mtwara na kuwatangazia wananchi kuendelea na kazi zao kama kawaida kwa kuwa ulinzi umeimarika, huku askari wa JKT na JWTZ waliosheheni silaha wakizunguka mitaani.
Pinda awasili Mtwara
Wakati tukiewnda mitamboni Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewasili Mtwara jana jioni na kukutana na viongozi wa mkoa.
Bungeni Dodoma
Suala la mgawanyo wa rasilimali za taifa jana liliendelea kutikisa Bunge, baada ya baadhi yao kueleza kuwa ni haki kwa maeneo yanakotoka rasilimali hizo kunufaika kwanza kabla ya maeneo mengine.
Wakati wabunge hao wakieleza hayo, wengine wamesisitiza kuwa kwa kuwa nchi ni moja Tanzania, rasilimali zote ni mali ya Watanzania wote.
Wabunge wanaotaka rasilimali zinufaishe kwanza maeneo zinakotoka. Wanasema pamoja na ukweli kwamba Tanzania ni moja, watu hao wana haki ya msingi kupata huduma hizo kwanza kuliko wengine.
Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige alisema anashangaa kwa nini fomula ya rasilimali kuyaendeleza maeneo iliyopatikana, inatumika kwenye Idara ya Wanyamapori na haitumiki katika sekta ya nishati na madini.

Source: Mwananchi