Saturday, June 8, 2013

Mauaji ya kutisha Sengerema

Mbunge wa Sengerema William Ngeleja

Hofu kubwa na simanzi imewakumba wakazi wa mji wa Sengerema akiwemo Mbunge wa jimbo hilo, William Ngeleja, baada ya Jeshi la Polisi wilayani humo kwa kushirikiana na wananchi kugundua makaburi mawili  yaliyozikwa watu wawili wakiwa wamejeruhiwa vibaya na kuvunjwa shingo.

Miili ya watu hao ilipatikana ikiwa imefukiwa katika makaburi mawili tofauti yenye urefu wa kina cha futi mbili ikiwa imeharibika vibaya, katika kitongoji cha Mnadani kata ya Nyampurukano na kusababisha watu walioshuhudia kuangua kilio na wengine kuzirai.


Kabla ya miili hiyo kugundulika, inadaiwa kuwa walikuwa wametoweka katika mazingira ya kutatanisha, huku mmoja ambaye mwili wake ulitambuliwa akidaiwa aliondoka na mganga wa kienyeji siku kumi zilizopita.

Akisimulia Tukio hilo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Sengerema, Ngeleja, juzi usiku, mjane wa marehemu Anna Enos (35) huku akibubujikwa na machozi na kusababisha Mbunge huyo naye kutokwa  machozi na baadhi ya wana ndugu  kuzirai, alidai kuwa mganga wa kienyeji ndiye aliyemchukua mume wake usiku wa saa mbili lakini toka siku hiyo hakurejea hadi mwili wake ulipogunduliwa ukiwa umezikwa.

Tukio hilo la kusikitisha liligundulika  juzi jioni baada ya mke wa marehemu kuamua kutoa taarifa posli na kwa uongozi wa kitongoji kufuatia mume wake kutorejea nyumbani kwa zaidi ya siku 10 baada ya kuchukuliwa na  mganga wa kienyeji.

Baada ya kutoa taarifa hiyo, mtuhumiwa alitiwa mbaroni na wanakijiji na kuanza kupewa kipigo kabla ya kunusuriwa na polisi.

Kisha wanakijiji hao walikwenda makaburini na kuanza kufukua makaburi waliyotilisha mashaka na ndipo walipofanikiwa kuipata miili hiyo imefukiwa.

Hofu imetanda katika mji wa Sengerema kufuatia matukio ya mauaji ya kikatili na ya utekeaj nyara watoto wa kike na wahusika wakitoa masharti ya kupewa fedha ili wawaachie.

Katika matukio hayo, wasichana watatau waliotekwa katika matukio mawili wanadaiwa kubakwa na kuumizwa vibaya kabla ya mtekaji kupatiwa Sh. 80,000 kwa njia ya M-Pesa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ernest Mangu, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja mwili wa aliyetambuliwa kuwa ni Robert Herman (54) mkazi wa kitongoji cha Mnadani aliyeacha watoto 10 na mjane mmoja.

Alisema mwili wa pili ulikuwa haujatambuliwa na kwamba upelelezi wa polisi unaendelea na tayari timu ya makahero imetumwa kufanya kazi hiyo toka jana.

Akitoa salaam za rambi rambi kwa familia na wanakijiji hao, Ngeleja aliwaomba wananachi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa polisi ili kuwezesha waliohusika wote kukamatwa kwani bila hivyo hali hiyo inaweza kuendelea.


Source: Nipashe
 

No comments: