Saturday, July 6, 2013

Miss Temeke ni Sylona Nyameyo


Miss Temeke Sylona Nyameyo alikaa akiwa pamoja na mshindi wa pili Marietha Boniface (Kushoto)  na mshindi wa tatu Latifa Mohamed (Kulia)


Washiriki wakijipanga jukwaani
Miss Temeke Sylona Nyameyo katikati na mshindi wa pili Marietha Boniface (Kushoto) na mshindi wa tatu Latifa Mohamed (Kulia)





MREMBO Sylona Nyameyo juzi usiku alifanikiwa kutwaa taji la Redd’s Miss Temeke lililofanyika katika Ukumbi wa TCC Changombe, jijini Dar es Salaam.

Sylona aliye mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akisomea mambo ya sheria alifanikiwa kuwashinda warembo wengine na kufanikiwa kujitwalia taji hilo.

Katika shindano hilo lililokuwa na upinzani mkali, ulioambatana na burudani za kumwaga, ilishuhudiwa nafasi ya pili ikienda kwa Marietha Boniface, ambaye naye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUCHS).

Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Latifa Mohammed ambaye amemaliza kidato cha sita mwaka huu, hivyo warembo hao kujihakikishia nafasi ya kuingia katika fainali za Redd’s Miss Tanzania.

Ushindani ulionekana dhahiri katika shindano hilo, ambapo warembo walikuwa wakichuana mno, huku mashabiki waliojitokeza hapo wakijikuta wakishangilia muda wote.

Akizungumza mara baada ya kuvikwa taji hilo, Sylona alisema amefurahishwa mno na matokeo hayo na atahakikisha hawaangushi wakazi wa Temeke katika shindano la Redd’s Miss Tanzania.

“Nilijua toka mwanzo lazima niwashinde, maana nilijiamini na niliona nina vigezo vyote, sasa ni wakati wa kwenda kupambana katika Redd’s Miss Tanzania ili kurudisha heshima ya Temeke,” alisema.


Shindano la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

No comments: