Sunday, September 1, 2013

Viongozi waeleza walivyosaidiwa na Marehemu Askofu Kulola





Makamu wa Rais Dr Mohamed Ghalib Bilal aliongoza maelfu ya waombolezaji kwenye ibada hiyo. Hapo anatoa salamu za serikali
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Ghalib Bilal jana aliongoza maelfu ya waombolezaji kwa ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania(EAGT), Dk Moses Kulola (83)  iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa la EAGT Temeke jijini Dar es Salaam.
Akitoa salamu za serikali Makamu wa Rais Dk. Bilal alisema Tanzania na kanisa limeondokewa na mmoja ya viongozi muhimu wa kanisa na taifa kwa ujumla.
Alisema Marehemu Kulola alikuwa mstari wa mbele kuhubiri neno na kuwa na mchango katika kudumisha amani na kuondoa maovu miongoni mwa raia.
Hata hivyo ibada hiyo ilichukua sura mpya baada ya viongozi kadhaa wa Serikali nchini, kufunguka na kutoa siri za mafanikio yao kwa maombi yake ikiwemo kupata uwaziri.
Viongozi hao ni pamoja na Paul Kimiti ambaye alikiri mbele ya maelfu ya waombolezaji kwamba maombi ya Askofu huyo, yalimpa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupata uwaziri mara mbili.

Paul Kimiti
“Nakumbuka aliniombea tena ofisini kwangu wakati huo nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, mbele ya bendera za taifa nilipiga magoti mbele ya mtumishi wa Mungu alikuwa anatembea na Yesu, kweli kila goti litapigwa kwa Yesu, kwa maombi yake nilifanikiwa kuwa waziri kwa vipindi viwili, ilibaki nusra niupate na uwaziri Mkuu,” alisema Kimiti akifuatiwa na kelele za kushangiliwa.
Kimiti amewahi kuwa Waziri wa Ajira na Maendeleo ya Vijana na Waziri wa Kilimo na Biashara, kati ya mwaka 1995 na mwaka 2000.
Kwa upande wake, Mchungaji Getruda Rwakatare ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, alisema Askofu Kulola alikuwa ni baba yake wa kiroho na kwamba alimtambua baada ya ndoa yake kuwa na mgogoro.
DK. Getrude Rwakatare
“ Alinifariji sana, aliniombea nakumbuka kuna wakati nilimweleza jinsi mateso yalivyoendelea katika ndoa yangu, aliniambia kama mume wako anakupiga au kukutesa tambua hakutesi wewe bali Yesu aliye ndani yako, maneno yale yalinitia nguvu nikabadilika nikawa mtumishi wa Mungu hadi leo naye akawa ananiita nabii Debora,” alisema Mchungaji Rwakatare.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso akiwasilisha rambirambi ya Sh 2,000,000, alisema kuwa jeshi hilo limepoteza kamanda wa kiroho na kimwili ambaye walikuwa wanamtumia kutokana na mahubiri yake katika kuzuia matukio ya uhalifu ikiwemo ya kikatili ya kukata viungo vya albino.
Makamu wa Askofu wa EAGT, Asumwisye Mwaisabila akitoa salamu zake kwenye ibada hiyo, aliwataka viongozi wote wa makanisa ya kiroho kumaliza tofauti zaoili kumuenzi Askofu Kulola ambaye alikuwa na upendo wa pekee.