Wednesday, September 18, 2013

Serikal kutoa tamko leo Balozi wa China kuvaa kofia ya CCM

Balozi wa China Lu Youqing kulia anayeshutumiwa kukiuka mkataba wa Vienna

Serikali ya Tanzania leo itataoa tamko kuhusu itakavyolishughulia suala la Balozi wa China nchini Lu Youqing ambaye anadaiwa kuwa amekiuka mkataba wa kimataifa wa Vienna kwa kushiriki masuala ya siasa tofauti na majukumu yake.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndicho kilichoanza kumshutumu balozi huyo wa kusema kuwa amekiuka mkataba wa kimataifa wa Vienna kwa kuanza kushiriki kazi ya uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kama alivyoonekana akiwa mkoani Shinyanga.


Wakati CHADEMA ikitoa madai hayo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imekiri balozi huyo kuvunja mkataba huo unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia na kuahidi kuchukua hatua.

Septemba 12 mwaka huu, balozi huyo alihudhuria mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika uwanja wa Shycom mkoani Shinyanga na baadaye katika eneo la mnada wa Mhunze Jimbo la Kishapu.

Balozi Youquing alitambulishwa kwa wananchi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na kisha kuwahutubia akisema China imevutiwa na sera za CCM na hivyo itawekeza katika soko la pamba katika mkoa huo.

Ni katika mkutano huo, balozi huyo alicheza nyimbo za CCM za kubeza vyama vya upinzani huku akiwa amevalia kofia ya chama hicho.

Akizunguza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA, Ezekia Wenje, alisema balozi huyo amekiuka mkataba wa kimataifa wa Vienna kuhusu mambo ya kidiplomasia kifungu cha 41 (i).
Alisema kifungu hicho kinakataza mabalozi wa nchi kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Wenje alibainisha kuwa mkataba huo unataka kazi za balozi kuwa ni kuwakilisha nchi na si chama.
“Balozi wa China yuko hapa kuwakilisha China nchini Tanzania, si Chama cha Kikomunisti kwa CCM,” alisema.

Wenje aliongeza kuwa haamini kama huo ndio msimamo wa serikali ya China na pia CCM kwani Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, alinukuliwa akiwaonya mabalozi kuingilia mambo ya ndani ya nchi kwa nyakati tofauti wanapokuwa wameongea na vyama vya upinzani.

Alisema kuwa CHADEMA imeazimia kuiandikia barua serikali ya China ili kuweza kupata msimamo wake kwa tabia ya balozi huyu kuandamana na chama kimoja na kutumia vifaa vyake vya uenezi katika mikutano ya hadhara.

4 comments: