Monday, November 15, 2010

Raia wa Sudan Kusini wasajiliwa kushiriki kura ya maoni



Baada ya kucheleweshwa kwa muda, hatimaye wapiga kura kutoka Sudan Kusini wanaanza kujiandikisha kushiriki kura ya maoni ya hapo mwakani.

Wapigaji kura wataamua iwapo Sudan Kusini itajitenga na Sudan Kaskazini na kujitawala kama taifa huru au la.

Shughuli nzima ya kujiandikisha inatarajiwa kuchukua siku 17, kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za kura ya maoni.

Kura hii ni mojawapo ya maafikiano ya mpango wa amani wa mwaka 2005 uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenye vya zaidi ya miongo miwili.

Kumekuwa na hali ya wasiwasi nchini humo baada ya kuzuka tofauti kati ya Sudan Kusini na Sudan Kaskazini juu ya utaratibu wa kufanyika kura hii lakini makundi hayo yanaarifiwa kuafikiana mwafaka wa kutatua tofauti zao.

Chini ya mwafaka huu suala la eneo linalozozaniwa la Abyei litatatuliwa na Rais wa Sudan na mwenzake wa eneo linalojisimamia la Sudan Kusini.

Imeafikiwa pia kwamba iwapo Sudan Kusini itaamua kujitawala kama taifa huru mipaka kati ya nchi hizo mbili zisifungwe na masuala ya uraia yakubaliwe kati ya mataifa hayo mawili.

Tangazo hili huenda likasaidia pakubwa kupunguza uhasama kati ya pande hizo mbili ambao umedhihirika kabla ya kura hiyo kufanyika Januari mwakani.

Hata hivyo kuna hofu iwapo shughuli hiyo itakamilika katika siku kumi na saba zilizotengewa.

Sudan Kusini inakisiwa kuwa na wapigaji kura milioni tano na ni dhahiri kwamba raia hao watapiga kura ya uhuru wa taifa lao kujitenga.

No comments: