Tuesday, November 23, 2010
Rais Sambi wa Comoro atembelea Tanzania
TANZANIA na Comoro zimekubaliana kuhusu umuhimu wa kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri vya majini kati ya nchi hizo mbili kufuatia tukio la karibuni la uharamia na utekaji nyara wa meli moja iliyokuwa inafanya safari kati ya nchi hizo
Aidha, Comoro imewasilisha rasmi pongezi zake kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kufuatia ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu, 2010.
Hayo yalijitokeza wakati Rais Kikwete alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mheshimiwa Ahmed Abdallah Sambi (mwenye kanzu kulia), Ikulu, Dar es Jumatatu ya Novemba 22, 2010.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili wamekubaliana kuhusu umuhimu wa kuimarisha usalama wa vyombo vya majini vinavyosafiri kati ya nchi hizo mbili, iwe ni vya kubeba bidhaa na mali ama kusafirisha watu.
Viongozi hao wawili wamejadili hali ya usalama kwenye eneo la maji linalounganisha nchi hizo mbili kufuatia tukio la karibu ambako meli moja ya Comoro, MV Aly Zoufecar iliyokuwa inasafiri kutoka Moroni kuja Dar es Salaam, ilitekwa nyara na maharamia Oktoba 31, 2010.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Comoro inasema kuwa ilikuwa na mabaharia tisa, akiwamo Mtanzania mmoja, na abiria 22 wakiwemo Watanzania 14.
Rais Sambi pia amemwelezea Rais Kikwete kuhusu hatua ambazo zinachukuliwa na nchi yake kuhakikisha kuwa meli hiyo inaachiwa huru na abiria wote wanaokolewa wakiwa salama.
Rais Kikwete amesikiliza baadhi ya mapendekezo ya jinsi ya kupambana na hali hiyo na ameahidi kuangalia hatua zinazofaa kuchukuliwa kuimarisha usalama wa vyombo vinavyosafiri katika eneo hilo.
Kuhusu ushindi mkubwa wa Rais Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, Rais Sambi amesema kuwa Watanzania wamechagua amani na utulivu na uongozi bora wa Rais Kikwete.
Rais Sambi amemweleza Rais Kikwete hali ya kisiasi ilivyo katika Visiwa vya Comoro, kufuatia uchaguzi wa Novemba 7, mwaka huu, na akaongeza katika nyanja ya siasa na nyanja nyingine Comoro itaendelea kujifunza kutoka Tanzania na pia kupata msaada wa uzoefu kutoka nchini.
Rais Kikwete ameshukuru kwa pongezi za Comoro na kuahidi kuwa Tanzania itaimarisha zaidi ushirikiano kati yake na Comoro. “Hili la kuimarisha uhusiana na ushirikiano nakubaliana nalo. Comoro ni nchi jirani, nchi rafiki na kwa kweli wako Wacomoro wengi wanaoishi kwa amani na kuendesha shughuli zao katika Tanzania.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment