Taasisi binafsi ya Bill na Melinda Gates itaendelea kuisaidia Tanzania katika masuala mbalimbali ya Utafiti katika sekta za afya na kilimo.
“Tuko tayari kuendelea kuisaidia Tanzania kama mtatupa vipaumbele vyenu” Mwenyekiti mwenza wa Taasisi ya Bill na Melinda Gates, Bw. Bill Gates amemwambia Rais Kikwete leo mchana alipofika Ikulu kumsalimia Rais.
Rais Kikwete amemshukuru Bw. Bill Gates na Mkewe Melinda kwa msaada wao mkubwa ambao wamekuwa wakiipatia Tanzania kwa ujumla.
Bw. Bill Gates na Mkewe Melinda wapo nchini kwa ajili ya ziara ya binafsi ya kifamilia ambapo wametembelea mbuga za Serengeti na pia shughuli za kikazi ambapo wanatembelea na kukagua miradi yao mbalimbali iliyopo nchini.
Tayari wametembelea Kituo cha Utafiti na Mafunzo katika Hospitali ya Bagamoyo, ambacho ni sehemu ya Kituo cha Utafiti cha Ifakara kilichoko Morogoro na Kituo cha Serikali cha Utafiti wa Kilimo cha Mikocheni (MARI) ambapo Taasisi ya Bill na Melinda inatoa msaada.
Katika utafiti wake kituo cha Bagamoyo kinatafuta kinga ya malaria wakati kituo cha Mikocheni kinafanya utafiti kutafuta chanzo cha ugonjwa katika zao la muhogo.
Wakati huo huo Rais Kikwete anaondoka mchana huu kwenda Malabo, Equatorial Guinea kuhudhuria kikao cha kila mwaka cha Wakuu wa Nchi za Afrika, chini ya uenyekiti wa Rais Teodoro Obiango Nguema Mbasogo. Mada kuu ya kikao cha mwaka huu ni uwezeshaji wa vijana kwa ajili ya maendeleo.
Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nchini Julai 2, ambapo Julai 3 atakuwa mgeni rasmi kwenye Siku ya Washirika wa Tumbaku mkoani Kagera.
Tarehe 4 Julai, Rais ataongoza sherehe za ufunguzi rasmi wa barabara ya Mwandiga-Manyovu, uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Uvinza na pia atazindua ujenzi wa daraja la Malagarasi.
No comments:
Post a Comment