Pinda awaambia viongozi
WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda amesema kuna haja ya kuweka utaratibu maalum wa kuwapima viongozi wa serikali ili kuona kama wanatekeleza kwa vitendo kauli ya Kilimo Kwanza.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Agosti 5, 2011) wakati akizindua maonesho na mashindano maalum ya mifugo katika Viwanja vya Nzuguni nje kidogo ya mji wa Dodoma ambako maonesho ya Nane Nane yanaendelea.
Mizengo Pinda |
WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda amesema kuna haja ya kuweka utaratibu maalum wa kuwapima viongozi wa serikali ili kuona kama wanatekeleza kwa vitendo kauli ya Kilimo Kwanza.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Agosti 5, 2011) wakati akizindua maonesho na mashindano maalum ya mifugo katika Viwanja vya Nzuguni nje kidogo ya mji wa Dodoma ambako maonesho ya Nane Nane yanaendelea.
“Kiongozi ni lazima uonyeshe kuwa wewe mwenyewe umedhamiria kweli kuwasaidia wananchi kuondokana na umaskini kwa kuonyesha mfano… utawezaje RC au DC kuwakaripia wanancnhi kuwa mbuzi wake wamekonda wakati wewe mwenyewe hata mbuzi mmoja huna?” alihoji.
“Unakuta DC anamkemea mwananchi… hili banda lako chafu sana! Utaanzaje kusema hivyo wakati wewe mwenyewe hata banda la kufugia hujajenga… Ni lazima tuanze sasa, tuwe viongozi kwa mfano! Lazima tutafute mbinu ya kuulizana, hata kama ni fomu kiongozi ajaze kuwa na kiasi gani cha mifugo…” aliongeza.
Alisema wananchi wanahitaji mahali pa kuangalia na kujifunza kutoka kwa mtu anayewaongoza na kwamba hakuna njia nyingine isipokuwa kwa viongozi kutoa mfano huo.
Akizungumzia kuhusu mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la Taifa, Waziri Mkuu alisema kuna tatizo la msingi katika sekta hiyo kwa mchango wake umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka katika miaka minne iliyopita.
“Mchango wa Mifugo kwenye Pato la Taifa bado ni mdogo sana kwa sababu ya kutumia ufugaji wa jadi ukiwemo ufugaji wa ng’ombe na kuku. Ukiangalia mwaka 2007 mchango wa sekta ya mifugo ulikuwa asilimia 4.7; mwaka 2008 asilimia 4.6; mwaka 2009 asilimia 4.0 na mwaka jana asilimia 3.8,” alisema.
“Mtiririko huu unaonyesha kwamba lipo tatizo la msingi katika sekta ya mifugo. Takwimu hizi zinaashiria kwamba ni lazima sasa tufanye mapinduzi ya ufugaji katika sekta hii na tuachane na ufugaji wa kizamani ambao tunauita ni ufugaji wa jadi,” alisema.
Alisema takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2011, zinaonesha kuwa idadi ya mifugo nchini inafikia ng’ombe milioni 21.3, mbuzi milioni 15.2 na kondoo milioni 6.4. pia, wapo kuku wa asili milioni 35 na kuku wa kisasa milioni 23 na nguruwe milioni 1.9.
“Idadi hii kubwa haiendani na mchango wa sekta hii katika uchumi wa nchi yetu... Endapo jitihada zitafanyika na kuinua sekta hii iongeze mchango katika pato la taifa, ni dhahiri kuwa hata pato la mfugaji pia litaongezeka,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alitoa changamoto kwa Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo kuhakikisha kuwa maonesho ya hayo ya mifugo yanafanyika kila mwaka na kwamba Dodoma ndiyo iwe makao makuu ya maonyeshao ya kitaifa ya mifugo. “Wenzetu Kenya wanafanya maonesho kama haya kila mwaka... Tunamshukuru Rais Jakaya Kikwete ambaye aliagiza maonesho haya yafanyike sambamba na wiki hii ya Nane Nane,” alisema.
Alisema maonesho hayo yajumishe mifugo ya aina mbalimbali pamoja na ufugaji wa nyuki na kwamba kama yatafanyika vizuri, ni dhahiri kuwa yatachangia kuhamasisha, kukuza na kuendeleza ufugaji bora hapa nchini.
Katika uzinduzi huo, ng’ombe sita wa maziwa wenye kilo kati ya 290 na kilo 720 ambao wanafungwa na wakulima wadogo na taasisi za hapa nchini walishindanishwa. Vilevile, ng’ombe sita wa nyama wenye kilo kati ya 337 na kilo 858 ambao wanafungwa na wakulima wadogo na taasisi za kilimo walipitishwa mbele ya mgeni rasmi na majaji.
Washindi wa maonesho hayo wanatarajiwa kupewa zawadi zao siku ya kilele cha sherehe za Nane nane jumatatu ijayo. Washiriki wa mashindani hayo walitoka kanda za kati, nyanda za juu kusini na kanda ya kaskazini.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri wa Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo, Dk. Mathayo David, Waziri wa Nchi (OWM – TAMISEMI), Bw. George Mkuchika, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Msekela, Mwenyekiti wa TASO Taifa, Bw. Engelbert Moyo, makatibu tawala wa Singida na Dodoma baadhi ya wakuu wa wilaya za mikoa hiyo na watendaji wa halmashauri za wilaya na manispaa.
No comments:
Post a Comment