Katibu
wa Jumuiya ya Madaktari,Dk Edwin Chitage akitoa tamko la Jumuia hiyo
kwa Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam la kutokuwa na imani na
Tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza tukio la kupigwa kwa
Mwenyekiti wao Dk Stephen Ulimboka.
TUKIO
la kutekwa nyara, kupigwa na kujeruhiwa vibaya, kisha kutupwa katika
Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kiongozi wa
Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka, limechochea kasi ya
mgomo baada ya madaktari bingwa kutangaza kujitosa rasmi kwenye mgogoro
huo.Awali madaktari hao hawakushiriki mgomo huo, lakini jana walieleza
kwa nyakati tofauti kuwa, wameamua kuungana na wenzao kutokana na unyama
aliofanyiwa kiongozi wao akiwa katika harakati za kutetea na kupigania
haki zao.
Madaktari hao wa hospitali za Muhimbili, Moi, KCMC,
Mbeya, Bugando na Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, jana walitangaza
rasmi kuwa wameingia kwenye mgomo huo kushinikiza pamoja na mambo
mengine, Serikali kutoa tamko kuhusu utata wa tukio hilo.
Tukio
hilo la aina yake kutokea nchini, limeathiri upatikanaji wa huduma zote
za matibabu katika hospitali hizo, huku madaktari katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili na Moi, wakielekeza nguvu zao kunusuru maisha ya
mwenzao aliyeumizwa.
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin
Chitage, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mgomo huo utaendelea hadi
hapo Serikali itakapotekeleza madai yao.
"Tunaitaka Serikali
kuacha vitisho kwa madaktari nchini, tunaitaka itambue kwamba mgogoro
huu hauwezi kumalizwa kwa njia yoyote vikiwemo vitisho bali ni kwa kukaa
meza ya majadiliano na kukubaliana na madaktari," alisema Dk Chitega na
kuongeza:
"Ninawashukuru madaktari wote nchi nzima, wauguzi na
wafanyakazi wa sekta ya afya kwa ujumla wao kwa kusitisha huduma baada
ya kupigwa mwenzetu. Tunaomba mshikamano huu uendelee," alisema Dk
Chitega.
Gazeti hili lilishuhudia wagonjwa wakiwa wamekaa katika
makundi bila kujua la kufanya, huku wengine wakiamua kuondoka na kwenda
hospitali binafsi.
Waliliambia Mwananchi kwamba kitendo
alichofanyiwa Dk Ulimboka ni cha kinyama na kuungana na madaktari hao
kuitaka Serikali kutatua mgogoro huo haraka.
Wagonjwa waliofika
katika eneo hili pia walielezwa bayana na maofisa wa Moi kwamba huduma
zimesitishwa kutokana na madaktari kugoma.
Ocean Road
Madaktari
bingwa katika Taasisi ya Ocean Road nao waligoma kutoa huduma hatua
iliyozua taharuki kwa wagonjwa waliofika kwa ajili ya matibabu.
Gazeti hili lilishuhudia ofisi za madaktari hao zikiwa zimefungwa na hata zile ambazo zilikuwa wazi, madaktari hawakuwapo.
Mmoja
wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Joyce Dachi, alisema kuwa,
wagonjwa wengi wamekuwa wakiandikishwa mapokezi, lakini wanachukua muda
mrefu kumuona daktari.
Mgomo huo pia umeendelea katika
Hospitali ya Amana wilayani Ilala huku uongozi wa hospitali hiyo ambao
uligoma kuzungumza na vyombo vya habari, ukihaha kunusuru hali hiyo.
Katika Hospitali za Temeke na Mwananyamala huduma ziliendelea kutolewa kama kawaida.
Mbeya
Katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ,madaktari bingwa ambao awali
hawakugoma jana waliingia kwenye mgomo na kusababisha wagonjwa katika
hospitali hiyo hususan kitengo cha wazazi, kusota bila matibabu.
Habari kutoka katika hospitali hiyo zilieleza kuwa hivi sasa madaktari bingwa wanatoa huduma kwa kujuana.
Mmoja
wa madaktari hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema kitendo
alichofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya yao kimewakatisha tamaa.
Alisema
kuwa, hali hiyo sasa imehamia hadi katika Kituo cha Wazazi cha Meta na
kufafanua kuwa hali ni mbaya, tayari wajawazito wametakiwa kuhamia
katika Hospitali ya Mkoa ambayo imefurika wagonjwa.
Mkurugenzi wa
Hospitali hiyo ya Rufaa, Dk Eliuter Samky hakuweza kuzungumzia tukio
hilo jana kutokana na kile kilichoelezwa na katibu wake muhtasi kwamba
ana kazi nyingi.
Mwanza
Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya
Bugando (BMC) mkoani Mwanza nao wamegoma, huku kiongozi wa Kamati Ndogo
ya hospitali hiyo inayoshughulikia migomo, akikataa kuzungumzia hali
hiyo.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu baada ya
kutoonekana katika maeneo ya hospitali, mmoja wa viongozi wa Kamati
hiyo, Dk Geogre Adrian, alisema kwa sasa hawezi kulitolea ufafanuzi
suala hilo na kwamba kufanya hivyo, ni kwenda kinyume na maagizo
aliyopewa na Kamati Kuu.
Akizungumzia huduma katika hospitali hiyo alisema kuwa hajui lolote kwa kuwa hawajagusa maeneo ya kazi kwani wapo kwenye mgomo.
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia huduma katika hospitali yake, hakupatikana.
Watimuliwa
Jana
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Charles Majinge alitoa tangazo la
kuwataka madaktari waliopo mafunzoni ‘Interns’ katika hospitali hiyo
kurejea kazini na kama watakiuka agizo hilo, watakuwa wamejifukuzisha
wenyewe.
Manyara
Mkoani Manyara, madaktari kumi katika
Hospitali ya Haydom Wilaya ya Mbulu wamegoma tangu juzi.Idadi ya
wagonjwa katika hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), inaongezeka siku hadi siku.
Wakizungumza
na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotaka kutajwa majina yao,
madaktari hao ambao wanafanya mafunzo ya vitendo katika hospitali hiyo,
wamesema kuwa hawatatibu wagonjwa mpaka madai yao yatekelezwe.
Mkuu
wa Wilaya ya Mbulu, Anatory Choya, alithibitisha kutokea kwa mgomo huo
na kufafanua kwamba wanaendelea kufanya mazungumzo ili kupata ufumbuzi.
Choya alisema kuwa madaktari wanaoendelea na kazi, wameelemewa kutokana na wagonjwa kuwa wengi.
Alisema kati ya madaktari 11 wanaosoma kwa vitendo hospitalini hapo, mmoja tu anayesomeshwa na hospitali hiyo, ndiye hajagoma.
KCMC
Hali
katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro imezidi kuwa tete
na kuwafanya ndugu kuwahamishia wagonjwa wao katika hospitali binafsi.
Mwananchi lilitembelea wodi za hospitali hiyo na kukuta vitanda vikiwa wazi.
Wakizungumza
na gazeti hili, baadhi ya madaktari ambao wapo kwenye mgomo kwa sharti
la kutotajwa majina, walisema hawako tayari kurudi kazini kwa kuhofia
usalama wa maisha yao.
Dodoma
Wagonjwa katika Hospitali ya
Mkoa wa Dodoma jana walijikuta wakipata taabu baada ya madaktari wa
hospitali hiyo kusitisha huduma kwa takriban saa sita kuanzia asubuhi.
Muda wa mchana utoaji huduma katika hospitali hiyo uliendelea ingawa kwa kusuasua.
Tofauti na siku zote, jana chumba cha daktari kilichokuwa wazi ni kimoja tu hali iliyosababisha msongamano mkubwa.
Arusha
Mjini
Arusha, madaktari wameendelea na mgomo katika Hospitali ya Mkoa ya
Mount Meru na kusababisha kudorora huduma huku wagonjwa kadhaa
wakiondolewa hospitalini hapo.
Mgomo huo, ulianza saa 1 asubuhi
hadi saa 6:00 mchana, ambapo madaktari na wauguzi,waligoma kutoa huduma
wakitaka kujua hatima ya Dk Ulimboka. Walitaka pia kuzungumza na uongozi
wa hospitali hiyo na waandishi wa habari, kuhusu mgogoro wao.
Askari anyimwa huduma
Askari
wa Usalama Barabarani ambaye jina lake halikufahamika mara moja ambaye
alipata ajali jana, alijikuta akishindwa kuhudumiwa katika hospitali ya
Mount Meru na kuondolewa kutokana na mgomo huo.
Askari huyo,
aliyevaa sare, alifikishwa hospitalini hapo saa 5:00 asubuhi akiwa
kwenye teksi, lakini wauguzi waliokuwa zamu walishauri apelekwe sehemu
nyingine.
Hata hivyo, uongozi wa hospitali ya mkoa, ukiongozwa na
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Omar Chande, jana ulifanya kazi ya ziada ya
kuwabembeleza madaktari hao, kurejea kazini, kusubiri uamuzi wa
Serikali.
Mgomo, Dk Ulimboka
vyateka Bunge
Mgomo
wa madaktari na kutekwa kisha kupigwa Dk Ulimboka jana vilitawala
mjadala wa Bunge hadi pale Spika Anne Makinda alipotoa mwongozo kwamba
suala hilo lisijadiliwe kwani liko mahakamani.
Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda alilazimika kutoa ufafanuzi wa hoja yake aliyoitoa juzi
pale alipokuwa akizungumzia mgomo wa madaktari na kuhitimisha kwamba
Serikali ilikuwa inajiandaa kutoa kauli na msimamo wake hivyo “liwalo na
liwe’.
Pinda alilazimika kutoa maelezo kutokana na swali
aliloulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
aliyetaka kufahamu maana ya kauli ya Waziri Mkuu ambayo aliita kuwa ni
nzito na iliyozua mjadala mkali nchini.
Kadhalika, Mbowe alitaka
kufahamu hatua ambazo Serikali imechukua kuhakikisha kwamba wananchi
wanaendelea kupata huduma za tiba kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba
madaktari katika hospitali kadhaa walikuwa wakiendelea na mgomo.
Kadhalika
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alimuuliza Pinda
kwamba haoni kwamba ni busara kujiuzulu wadhifa wake kutokana na ahadi
yake kwamba mgomo wa madaktari usingetokea, lakini ahadi hiyo imeshindwa
kutekelezeka.
Akimjibu Mbowe, Pinda alikiri kutoa kauli hiyo
ndani ya Bunge juzi na kusema alifanya hivyo akiamini kuwa jambo hilo
lilikuwa mahakamani na akasema asingeweza kusema jambo lolote kwa kuwa
hana tabia ya kuwa na utovu wa nidhamu wa kuingilia mambo ya mahakamani.
Hata
hivyo, alijitetea kuwa kabla ya kutoa kauli hiyo bungeni juzi, hakuwa
na taarifa kuhusu tukio la kupigwa kwa Ulimboka na akasema kuwa, kauli
yake haihusiani kabisa na Serikali kuhusika katika jambo hilo kwa namna
yoyote ile.
Waziri Mkuu alisema tayari amekwishaagiza vyombo
husika kufanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu ya haraka ili wahusika
waweze kuchukuliwa hatua stahiki mara moja.
“Kwanza namtakia
afya njema ndugu Ulimboka, na mimi nataka Watanzania waamini kuwa
tulikuwa katika mazungumzo mazuri na madaktari chini yake Ulimboka hivyo
tukio hilo ambalo limetokea katika mazingira magumu limetushtua kweli,
kama ni Serikali basi ingekuwa ni Serikali ya ajabu kweli,’’alisema
Pinda.
Kuhusu namna ya kusaidia Watanzania wasiathirike na mgomo
huo, alisema tayari Serikali imeshaagiza madaktari kutoka wizarani
kutumika na kuwaomba waliostaafu kutoa huduma katika kipindi hicho
kigumu.
Mkakati mwingine ni pamoja na kutumia hospitali za Jeshi
ikiwamo Lugalo waanze kutoa huduma hizo wakati Serikali inaendelea
kuzungumza kwa utaratibu na madaktari.
Lissu aliuliza swali la
nyongeza kumtaka Pinda kuachia ngazi hali iliyosababisha mvutano kwani
Waziri Mkuu alikosoa uulizaji wa swali hilo kuwa halikustahili.
Baada
ya kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John
Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala la madaktari akitaka
taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ambayo ilifanyia kazi
suala la mgomo wa madaktari ijadiliwe bungeni.
Hata hivyo, Spika
Makinda alisema ripoti hiyo haiwezi kujadiliwa kwani tayari Serikali
ilishakabidhiwa kwa ajili ya kuifanyia kazi na kwamba mapendekezo ya
Bunge kupitia ripoti hiyo yamefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa. |
No comments:
Post a Comment