Tuesday, October 16, 2012

Kikwete ziarani nchini Oman

Rais Jakaya Kikwete na Mfalme wa Oman Qaboos bin Said katika jumba la Kifalme nchini Oman


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika Taifa la Kifalme la Oman, ikiwa ni ziara ya kwanza ya Kiserikali kufanywa na Rais wa Tanzania katika nchi hiyo.

Rais Kikwete na ujumbe wake ameondoka mjini Dar es Salaam asubuhi ya Jumatatu, Oktoba 15, 2012, kwenda Oman kuanza ziara hiyo inayofanyika kwa mwaliko wa Kiongozi wa Ufalme wa Oman, Mfalme Qaboos bin Said, ambaye atakuwa mwenyeji wake kwa siku zote nne.


Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat, Rais Kikwete alilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mheshimiwa Yousef  bin Abdullah bin Alawi ambaye aliaandamana naye hadi Jumba la Muscat Gate ambako Rais alipokelewa na Mfalme Qaboos. Kutoka hapo walindamana hadi Kasri ya Kifalme ya Al Alam ambako alipokelewa rasmi kwa heshima zote za Kiserikali.

Shughuli kubwa ya jioni ya leo ya Mheshimiwa Rais itakuwa ni kufanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati ya Serikali za Tanzania na Ufalme wa Oman na pia kuhudhuria dhifa rasmi ambayo Mfalme Qaboos atamwandalia mgeni wake kwenye Kasri ya Al Alam.

Leo Jumanne, Oktoba 16, 2012, Rais Kikwete atatembelea Jumba la Makumbusho la Majeshi ya Ulinzi ya Oman, atafungua Mkutano wa Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman, atashuhudia utiaji saini makubaliano ya mikataba miwili kati ya nchi hizo mbili, ukiwamo ule wa kuundwa kwa Baraza la Biashara la Tanzania na Oman na ule wa Kuendeleza na Kulinda Uwekezaji katika nchi hizo mbili.

Jioni, Rais Kikwete atatunukiwa nishani ya juu kabisa ambayo Ufalme wa Oman hutoa kwa viongozi wa nchi za nje ya First Order Medal kwenye Chakula Maalum cha Usiku kitakachoandaliwa na Mfalme Qaboos kwa heshima ya Rais Kikwete.

Rais Kikwete na ujumbe wake pia utakutana na kuzungumza na Watanzania wanaoishi Oman katika mkutano utakaofanyika kwenye Hoteli ya Kifalme ya Al Bustan.
 
Hii itakuwa mara ya pili kwa Mheshimiwa Kikwete kutembelea Oman. Aliitembelea nchi hiyo mara ya kwanza mwaka 1998, wakati huo akiwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa