Tuesday, October 2, 2012

Ni pundua pinduka uchaguzi wa CCM

Baada ya Lowassa kushinda awazodoa wapinzani wake

Sumaye hoi safiri ya Ikulu huenda ikaota mbawa


Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ameibuka na ushindi mkubwa na kutangazwa kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana wilayani Monduli, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, aliibuka na ushindi wa asilimia 93.3 dhidi ya wapinzani wake wawili Dk. Salash Toure na Nanai Konina.

Lowassa alipata kura 709, Konina kura 44 na Dk. Toure kura saba.

Awali wakati Lowassa akiomba kura kwa wajumbe wamchague, mgombea mwenzake wa nafasi hiyo, Dk.  Toure, alijikuta katika wakati mgumu kutokana na kuzomewa na wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya.

Hatua hiyo ya kuzomewa kila alipozungumza ilimfanya Dk. Toure kutangaza kujitoa kwenye kinyanyang’anyiro hicho.

Lowassa aliyeanza kujinadi kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia afya njema na pia kwa chama chake kumteua kuwania nafasi hiyo hali ambayo inaonyesha kuwa wana imani naye.


“Mtu anaweza akawauliza kwa nini ninagombea nafasi hii sasa kwa jeuri na uhakika mnaweza kumjibu kwamba sasa Monduli tuna amani tuliyoitengeneza kwa uhakika,” alisema.

Lowassa alifafanua kuwa katika suala la maendeleo, Wilaya  ya Monduli hakukuwa na barabara ya lami iliyokuwa ikifika hadi Monduli badala yake iliishia eneo la Kosovo katika barabara kuu itokayo Arusha kwenda Karatu, lakini hivi sasa ipo.

Kuhusu huduma ya maji, alisema sasa hivi maeneo mengi yanapata huduma hiyo ingawa yapo maeneo machache ambayo upo mkakati wa kuyapatia maji.

Akizungumzia kuhusu huduma za afya, alisema zipo Sh. milioni 850 katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ambazo zitatumika kujenga hospitali na zahanati katika kata 10.

Lowassa alisema katika elimu zimejengwa kwa shule nyingi za msingi na sekondari hivyo watoto wengi wa jimbo hilo wanaenda shule tofauti na ilivyokuwa awali.

Baada ya dakika tatu za kujinadi kumalizika, Mkurugenzi wa Uchaguzi huo, Athumani Sheshe, alimtaka mgombea kuwaomba kura, lakini wajumbe kwa pamoja walipaza sauti zao wakisema hana haja ya kuomba kura kwani atapewa zote.

Aidha, Sheshe alipowataka wajumbe kama kuna mtu mwenye swali la kumuuliza mgombea, walijibu kwa pamoja kwamba hawana swali lolote la kumuuliza.

No comments: