Monday, October 22, 2012

Sheik Farid aburutwa Kortini anyimwa dhamana

Sheikh Farid Hadi Ahmed
  Watuhumiwa saba kutoka Makundi mawili ya kidini hapa Zanzibar, leo wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kufanya mikutano na kupelekea ghasia zilizoleta uvunjifu wa amani na uhalibifu wa miundombinu ya barabara.
Waliofikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Mwanakwelekwe ni pamoja na Mwenyekiti wa Jumuia ya Maimamu Zanzibar Sheikhe Farid hadi Ahmed(41) na Mwenyekiti wa Kundi la Uamsho Sheikhe Mselem Ali Mselem(52).
Watuhumiwa hao pamoja na wenzao wengine watano, walisomewa mashtaka ya kufanya mikutano iliyopelekea fujo na uvunjifu wa amani kulikokwenda sambamba na uharibifu wa miundombinu ya barabara na uharibifu wa mazingira kama vile kukata miti na kuziba barabara.
Watuhumiwa wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni MUSSA JUMA ISSA, AZAN KHALID HAMDAN,
SULEIMAN JUMA SUIMANI, HASSAN BAKARI SULEIMAN na  KHAMISI ALI SULEIMANI ambao wote walikana mashitaka yao.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwereke Mh. Msaraka Ame Pinja, ilidaiwa na na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Bw. Maulidi Ame Mohammed, kuwa kuwa watuhumiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kufanya mkutano na kusababisha ghasia na vurugu hapo Septemba 27, mwaka huu.
Hakimu Msaraka amekataa kutoa dhamana kwa Watuhumiwa hao hadi Alhamisi Oktoba 25, mwaka huu atakapofikiria kuwapa ama kutowapa dhamana watuhumiwa hao kutokana na unyeti wa kesi inayowakabili.
Mbali ya watuhumiwa hao wenye wafuasi wengi, lakini kivutio kikubwa leo ilikuwa ilikuwa ni askari wa kutuliza Ghasia kinachojihusisha na masuala ya ulengaji wa shabaha na udunguaji ambacho ni maalumu kwa kupambana na vitendo vya ugaidi na majanga yasiotabirika.
Askari hao wakiongozwa na naibu Mkurugugenzi wa makosa ya Jinai hapa Zanzibar na Maafisa wengine wa Jeshi la Polisi, walionekana wakiwa wamesheheni vifaa maalum vya kujikinga na risasi za moto na milipuko huku wakiwa wamevalia kofia ngumu na miwani nyeusi zenye viona mbali.
Wengi wao wakiwa wameketi kwenye magari yao na wengine wakishika doria katika maeneo mbalimbali nje ya mahakama, wamewafanya watu waliofika mahakamani hapo kusikiliza kesi za ndugu zao kubaki nje sio kwa woga lakini wakiwashuhudia askari hao hadi watuhumiwa walipotoka na kupelekwa gerezani.
Baadhi ya wananchi walionekana wakiwauliza watu wengine siku ya kutajwa kwa kesi hiyo baada ya muda wao mwingi kuishia kuwatazama Polisi hao waliokuwa na silaha mbilimbli kwa kila mmoja mbali ya kuwa na mabom ya gesi ya kutoa machozi
Lakini pia kutojitokeza kwa watu wengi mahakamani hapo kunatokana na onyo la Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa aliyewataka wazazi na walezi kuwazuia watoto wao kujihusisha na makundi yanayopelekea vujo na vurugu.
Kamishna Mussa alisema Askari Polisi kwa kushirikiana na wenzao wa vikosi vingine vya Ulinzi na Usalama hapa Zanzibar, watahakikisha kuwa wanapambana na yeyote atakayejihusisha na fujo na kuharibu miundombinu ya barabara na mazingira.
Mji wa Zanzibar hivi sasa ni shwari na tulivu kana kwamba hakujatokea jambo lolote siku kadhaa zilizopita.