Sunday, October 21, 2012

Sofia Simba Mbunge miaka mingine 5, Ashinda UWT

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsi na Watoto, Sofia Simba

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba  amekuwa Waziri wa kwanza kuwa na uhakika wa kuingia Bungeni baada ya Bunge hili kumalizika baada ya jana kushinda Uenyekiti wa UWT ndani ya Chama Chama Mapindiuzi

Sofia Simba amejihakikishia kuwa Mbunge wa viti Maalum kwa kipindi kingine cha miaka 5 kwani ndani utaratibu wa CCM Mwenyekiti wa UWT moja kwa moja huingia bungeni katika zile nafasi za wabunge wa viti maalum kwa upande wa Wanawake.

Katika uchaguzi huo Sofia Simba alimbwaga hasimu wake Anne Kilango  kwa idadi kubwa ya kura katika uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) linaripoti  gazeti la Mwanachi.

Hii ni mara ya pili kwa Simba kumshinda Kilango katika kuwania nafasi ya uenyekiti wa UWT, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2008, ambapo Simba aliibuka mshindi.
Katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma ambao ulisimamiwa na  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka


Hata hivyo, uchaguzi huo ulinusurika kuingia dosari baada ya mbunge wa Afrika Mashariki Shyrose Bhanj, kuchafua hali ya hewa ambapo yeye na mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Simba nusura wapigane.
Katika tukio hilo, Shyrose na Simba huenda wangepigana kutokana na kila mmoja kutaka kuonyesha ubabe kwa mwenzake.
Hali hiyo ilitokea baada ya Bhanj kuelekeza tuhuma za moja kwa moja kwa Simba kuwa katika kipindi chake cha uongozi, hakusimama katika majukwaa kuisaidia CCM hata siku moja.
Kauli hiyo ilionekana kumkwaza Simba, aliyekuwa jukwaani akijieleza na baada ya kushuka alikwenda moja kwa moja mahali alipokuwa ameketi Bhanj na kumnyooshea kidole akisema: “Huniwezi wewe!”
Kauli hiyo ilimkasirisha Bhanj na kufanya ahamaki. Aligeuka na kuuliza: “What! Uko na mimi?”
Ilikuwa kama sinema, kwani awali, Bhanj alitoka katika kiti alichoketi na kwenda kukaa mbele, alipokuwa ameketi Sophia Simba, ili aweze kupata nafasi ya kuuliza maswali.
Awali Bhanj alimuuliza mgombea Anne Kilango Malecela akitaka kujua kilichomsukuma kugombea uenyekiti wa UWT.
Hata hivyo, swali hilo lilikataliwa na aliyeongoza mkutano huo akiwa msimamizi wa uchaguzi huo, Profesa Anna Tibaijuka akisema halikuwa na mashiko.
Hata hivyo, Bhanj aliomba nafasi tena, kabla ya kuipata ya kumuuliza Simba, Tibaijuka aliwaelekeza kuwa, aulize swali na siyo kutoa hotuba.
“Mheshimiwa mjumbe, naomba uulize swali siyo kutoa hotuba,  tafadhali naomba apewe nafasi ya kuuliza swali maana naamini pia mgombea wetu ni mahiri atalijibu tu,” alisema Tibaijuka, kauli iliyotafsiriwa na baadhi ya wajumbe kuwa ni ya kumbeba Simba.
Akijibu swali hilo Simba alisema: “Huyu mjumbe, hajui kabisa kampeni za chini, hizo kelele za wajumbe zinaonyesha kuwa nilikuwa nafanya kazi kikamilifu, ndiyo maana hata yeye amekuwa ni Mbunge wa Afrika Mashariki kupitia sisi wanawake.”
Majibu ya Simba yalilipua kelele kutoka kwa wajumbe ambao moja kwa moja walianza kumshangilia licha kuwa awali ilikatazwa kufanya hivyo.
Baada ya kumaliza kujieleza na kuomba kura, ndipo Simba alishuka kuelekea mahali alipoketi na Bhanj alisimama akitaka kumpisha, lakini ghafla Simba akamnyooshea kidole na kumweleza kuwa hatamuweza.
Ndipo wakaanza kujibizana na kusababisha mkutano huo kusimama kwa muda, huku wapambe waliodaiwa kuwa wa Sophia Simba wakionekana kukerwa zaidi na kutaka kumpiga Bhanj, aliyesaidiwa na watu wa usalama kuondolewa eneo hilo.
Hata hivyo, Profesa Tibaijuka alizuia watu wa usalama wasimtoe nje Bhanj kwa sababu ni mjumbe halali wa mkutano huo.

Simba ajieleza
Akijieleza katika mkutano huo wa uchaguzi,  Simba aliwataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UWT kutochagua watu aliodai kuwa, wakiwa bungeni wanabwatuka ovyo na kuikosoa CCM kana kwamba yuko upande wa upinzani.
“Wajumbe wa kata, wilaya na mikoa mmekuwa mkifuatilia habari za Bunge kila wakati, nadhani mnaona, mimi ni Serikali siwezi kubwatuka ovyo. Lakini kuna watu wanabwatuka na kusema patachimbika, huku wakikikosoa chama. Hawafai hao,” alisisitiza Simba.
Miongoni mwa wagombea watatu wa nafasi ya Mwenyekiti wa UWT Taifa, wawili ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni Simba na Kilango Malecela na ambao wamekuwa wakisigana katika kampeni, huku Maryrose Majinge akionekana kutotajwa.
Kauli ya Simba ilionekana wazi kumwelekea Kilango, ambaye mara zote amekuwa akijipambanua kuwa mpambanaji wa ufisadi na kuonekana kama mtetezi wa wanyonge.
Tofauti na maelekezo ya mwenyekiti wa muda na msimamizi wa uchaguzi huo, kauli hiyo ya Simba iliibua kelele za kuzomea na kushangilia wakiimba Simba, Simba, Simba.
Simba alikanusha kuwa, suala la ukomo wa Viti Maalumu halijafika kwa nafasi za udiwani bali lipo kwa wabunge na kwamba litajadiliwa kwenye maoni ya Katiba Mpya.
Nje ya ukumbi wa mikutano, Simba alisimama mlangoni akiomba kura kwa kila mjumbe aliyekuwa akiingia ukumbini.
Kilango ajinadi na Biblia mkononi
Tofauti na hasimu wake, mgombea Anna Kilango Malecela alifika katika ukumbi wa mikutano akiwa katika gari moja na mumewe  Malecela na kuingia moja kwa moja ukumbini.
Mara baada ya kushuka katika gari, wanandoa hao walikumbatiana na kisha Malecela alionyesha ishara ya mkono ili mkewe aingie ndani ya ukumbi naye alitekeleza.
Akiwa ndani ya ukumbi, Kilango alipita kila kiti na kuwaomba wajumbe kura huku akiwa amebeba Biblia mkononi.
Haikujulikana ni kwa nini Kilango alitumia staili hiyo ya kuwa na Biblia, lakini baadhi ya wajumbe walitafsiri kuwa ilikuwa ni kuonyesha kuwa anamtegemea Mungu kwa kila kitu.
Katika hotuba yake ya kuomba kura, alisema kuwa, atahakikisha kuwa UWT inawezeshwa kiuchumi pamoja na kuwasaidia watendaji wa ngazi za wilaya kuishi na wenza wao.
Kilango aliwaeleza wajumbe namna alivyo na mvuto na ubavu wa kupambana na upinzani, hasa katika kipindi cha uchaguzi wa mwaka 2015, akipewa nafasi hiyo anaweza kusambaratisha ngome zote za upinzani.
Alitoa mfano wa kiwanda cha kusindika tangawizi alichojenga katika Jimbo lake la Same Mashariki kuwa, alipopewa nafasi ya ubunge alihakikisha kuwa anafanikisha mambo mengi.
Kilango aliahidi kuongeza kipato cha watendaji wa nafasi mbalimbali ndani ya UWT, ili waweze kuwa na kipato cha kuwatosha.
Maryrose Majinge
Kwa upande wake, Majinge alifika katika mkutano na kuingia moja kwa moja ndani ya ukumbi na kuanza kuomba kura kwa wajumbe mmoja, mmoja waliokuwa wakiingia ndani ya ukumbi.
Katika hotuba yake mgombea huyo aliwataka wajumbe kuchagua viongozi wenye ushawishi na si watu wa mavazi.
“Nina uwezo wa kushawishi, nina elimu ya kutosha kuongoza na ninatosha kimaadili pia. Ninaomba mnichague, maana uongozi siyo mavazi ya kanga na vitenge wala nyimbo,’’alisema Majinge.
 Nje ya ukumbi
Njeya ukumbi wa mkutano huo mkuu wa UWT, kambi mbili zilikuwa zikitambiana kwa nyimbo za mafumbo na ushangiliaji.
Wapambe wengi waliokuwa wanaume waliokuwa wamevalia mabango ya picha ya Simba huku wakiimba; “Simba lazima aungurume leo Dodoma.”
Kwa upande wa wapambe wa Kilango walikuwa wakiimba; “Tunataka mabadiliko, tunataka mabadiliko.”
Hata hivyo kundi la Kilango lilionekana kuwa ni dogo.
Rushwa nje nje
Uchaguzi huo uligubikwa na viashiria vyote vya rushwa ingawa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilionekana kuweka mitego yake kila kona.
Hata hivyo, kulikuwa na mbinu za hali ya juu ambapo baadhi ya wajumbe walikuwa wakichukulia pesa kwa wauza nguo pamoja na vibanda vya mama lishe, ambao jana ilikuwa siku ya mavuno kwao.
“Mimi nimeelekezwa majina ya watu, kwa hiyo wakifika katika eneo hili wanajitambulisha na ninawapa elfu ishirini. Lakini lazima na mimi nihakikishe kuwa nabakiwa na pesa, maana wengine nawapa hata elfu kumi na wengine naona hawaji kabisa,” alisema mmoja wa wauza vyakula nje ya ukumbi huo.
Mama huyo alisema kuwa hakujua pesa alizokuwa akitoa zilikuwa ni za upande wa mgombea gani, lakini alikubali kuzishika kwa kuwa watu hao walinunua pia chakula chake chote.
Mamalishe huyo alisema baadhi ya wapambe waliokuwa wamesimama mahali pa wazi kuonyesha ishara ya wajumbe wanaostahili kupewa posho hizo.
Alibainisha hayo baada ya mwandishi wa habari hizi kumaliza kula chakula na alipotakiwa kulipa ndipo mama huyo alipobaini kuwa hakuwa miongoni mwa wapambe na akakataa kuzungumza zaidi.
Awali akifungua Mkutano huo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Mohamed Gharib Bilali, aliwataka wajumbe kuchagua viongozi waadilifu.
Dk Bilali alisema iwe mwiko kuwachagua watu waliotoa rushwa kwa ajili ya kununua uongozi ma kutahadharisha kuwa jambo hilo linaweza kuwa ni shubiri kwa CCM.