Friday, November 9, 2012

Kashfa ya Akaunti Uswis Zitto ataka Mawaziri Wakuu Wastaafu wachunguzwe

Zitto Kabwe
Mbunge wa Kigoma kaskazini Zitto Kabwe amewasilisha hoja binafsi  kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza Serikali kuchukua hatua dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.
ambapo amewataja watu wenye nyazifa za juu na Mawaziri Wakuu wastaafu wanapaswa kuchungwa kuhusu kashfa hiyo.

Bila ya kuwataja kwa majina, mbunge huyo aliwataja watu hao kwa nyadhifa kuwa ni watu wote walioshika nyadhifa za uwaziri mkuu katika kipindi cha 2003 hadi 2010, walioshika nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini katika kipindi hicho na waliokuwa makatibu wakuu Wizara ya Nishati na Madini.

Baada ya kuwasilisha hoja hiyo mjadala mkali uliibuka bungeni jana kufuatia Mbunge huyo kuwalipua vigogo hao akitaka wachunguzwe kwa makosa ya kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi.



Wengine ni mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi, wakuu wa majeshi, wanasheria wa Serikali, makamishna wa nishati, walioshika wadhifa wa Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010.
Kutokana na hilo, Zitto aliitaka Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria bungeni wakati wa Mkutano wa 11 wa Bunge wa Aprili mwakani.

“Mbali na hilo napendekeza kuwa iwe ni marufuku kwa kiongozi yeyote wa umma au mume au mke wake au mtoto wake kuwa na akaunti nje ya nchi isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano,” alisema Zitto.


Pia Zitto alitaka Serikali kuwasiliana na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha ‘Assets Recovery Unit’ ili mabilioni ya fedha na mali ambazo zimetoroshwa nje ya nchi kwenda Uswisi, Dubai, Mauritus na maeneo mengine ziweze kurejeshwa.
Aliwataka Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya nchi waeleze wamezipata wapi na Takukuru wachukue hatua za kisheria  dhidi ya watu wote wanaomiliki fedha hizo kinyume cha sheria.
Zitto alisema katika mkutano wa Bunge la 11 na baada ya taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu raia wa Tanzania wenye kumiliki fedha za kigeni kwenye benki na mali nje ya Tanzania ilete taarifa ya hatua ilizochukua ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya nchi.
Alipendekeza kwamba Serikali katika bajeti ya mwaka 2013/14 ianzishe kodi maalumu ya asilimia 0.5 ya thamani ya fedha zilizotoroshwa ili kuweka rekodi za uhakiki fedha za ndani na zinazotoka nje.
Mbunge huyo alisema mazungumzo yake na wachunguzi wake binafsi kiwango cha fedha kinachomilikiwa na Watanzania Uswisi peke yake ni takriban mara 20 ya kiwango kilichotangazwa na benki  ya taifa ya nchi hiyo.
Alisema fedha hizo ni sehemu tu ya fedha ambazo Watanzania wamezificha katika benki mbalimbali  za nje.

Alitoa mfano wa Benki ya UBS peke yake iliyopo katika nchi hiyo ina maofisa 240 ambao wanashughulikia  wateja wa Tanzania  na kila ofisa mmoja husimamia mteja mmoja mwenye kiwango kisichopungua dola za Marekani 10 milioni.

Zitto alisema Benki Kuu ya Uswisi ilitangaza kuwa jumla ya dola za Marekani 196 milioni zilikuwa zimehifadhiwa  kwenye akaunti za benki za nchi hiyo.
Alisema kuwa pamoja na Mkurugenzi wa Takukuru kukaririwa akisema kuwa ataiandikia Serikali ya Uswisi barua kuomba kurejeshwa kwa fedha hizo , lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.

Majibu ya AG
Akichangia hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema Serikali imeanza kuzifanyia uchunguzi tuhuma hizo.
Alisema kwamba siyo kwamba Serikali imelala bali inaendelea na uchunguzi na kwamba vyombo vya usalama na Takukuru wanalifanyia kazi suala hilo.
 Mbunge wa Simanjiro (CCM),  Christopher Ole Sendeka alisema hata kama ni Rais aliyeko madarakani au waziri mkuu ama kiongozi yeyote atajwe bungeni ili Bunge limwondolee kinga aburutwe  mahakamani.

Alimtaka Zitto kuwataja kwa majina watu hao ili wachukuliwe hatua.
Kwa upande wake, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliwataja marehemu Daudi Balali, Andrew Chenge na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja kwamba walihusika na tuhuma za ufisadi wa Tan Gold hivyo Bunge linapaswa kuchukua hatua. “Si fahari kwa Serikali kuwa na watendaji ambao siyo waaminifu,” alisema.
Aliwataka wabunge kuwa pamoja na hasa upande wa CCM kwa kuwa ni wengi waunge mkono hoja ya Zitto ili dhambi isije ikawadondokea.
Alisema mapendekezo ya Jaji Werema ni ya kuua hoja na si kuiboresha.
Naye Mbunge wa Kisesa (CCM),  Luhaga Mpina alitaka watu walioficha fedha nje ya nchi watajwe kwa majina ili wananchi wawafahamu.

Mpina ambaye aliwahi kuwasilisha hoja nyingine ya kuwapo mabilioni yaliyofichwa nje ya nchi na  baadhi ya Watanzania, alisema yeye haogopi kitu chochote na kwamba waliochota fedha wachukuliwe hatua.

Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema  wapo Watanzania wanaotoa fedha nyingi kwenye uchaguzi na kutoa misaada mbalimbali kiasi cha kuiharibu nchi, hao peke yake wanatosha kudhihirisha kwamba ni mafisadi walioficha fedha nje.
Alisema Bunge lisigawanyike kama ilivyotokea katika Bunge la Tisa kwenye masuala ya Dowans , Richmond na Epa ambapo kila wabunge wakisimama viongozi wa Serikali wanatoa vikwazo kuzuia juhudi zao na akaapa katika mabilioni ya Uswisi hawatalala.

Wiki iliyopita wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kuhusu mabilioni ya fedha yaliyofichwa nje ya nchi, Freeman Mbowe, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Serikali imeanza kulifanyia uchunguzi wa kina suala hilo ili kujua ukweli wake na hatua za kuchukua.

Waziri Mkuu alisema mara baada ya uchunguzi huo kukamilika Serikali itatoa taarifa kamili.

Taarifa kutoka Benki Kuu ya Uswisi inaonyesha kuwa baadhi ya  fedha hizo zimewekwa katika akaunti za vigogo hao na kampuni za mafuta na gesi zilizopo nchini.
Zitto akihutubia mkutano wa hadhara Rombo mkoani Kilimanjaro Oktoba 26 mwaka huu, alimlipua Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah akidai kuwa bosi huyo ameandika barua Uswisi, akieleza kwamba Tanzania haina masilahi na mabilioni ya fedha yaliyofichwa katika benki za nchi hiyo.
Hata hivyo, Dk Hoseah alikanusha akisema kuwa tuhuma hizo hazina ukweli wowote.

source: Gazeti la Mwananchi

No comments: