Friday, January 25, 2013

Dhamana ya Lulu bado ni Kizungumkuti




MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imesogeza mbele tarehe ya usikilizwaji wa maombi ya dhamana ya msanii wa fani ya maigizo, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia.

Lulu aliwasilisha mahakamani hapo maombi ya dhamana, kupitia kwa jopo la mawakili wake linaloongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama, Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Peter Kibatala na Fulgence Masawe wa Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).



Maombi hayo yalikuwa yamepangwa kusikilizwa leo na Jaji Zainabu Mruke, lakini yamesogezwa mbele hadi Jumatatu, Januari 28, 2013.

Hata hivyo taarifa ya Mahakama (notice) ya kusogezwa mbele kwa usikilizwaji wa maombi hayo, kwenda kwa mawakili wa pande zote haikueleza sababu, lakini pengine hiyo ni kwa sababu leo ni Sikukuu ya Maulid.

Lulu anakabiliwa na mashtaka ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa msanii maarufu wa fani hiyo nchini, Steven Kanumba, kinyume cha kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu.

Awali kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali ukiwamo upelelezi, huku akikabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia kinyume cha kifungu cha 196.

Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa upelelezi, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alimbadilishia mashtaka na kuwa ya kuua bila kukusudia, na Desemba 21, 2012, alisomewa maelezo ya kesi yakiwamo maelezo ya mashahidi watakaotoa ushahidi.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, kesi hiyo ilihamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndio ina uwezo wa kusikiliza mashtaka yanayomkabili. Tayari kesi hiyo imeshasajiliwa Mahakama Kuu kuwa shauri la jinai la kuua bila kukusudia, lenye namba ya usajili 125 la mwaka 2012.

Kutokana na mabadiliko hayo ya mashtaka, sasa mshtakiwa kupitia kwa mawakili wake hao, amewasilisha maombi ya dhamana chini ya hati ya dharura wakiomba yasikilizwe na kuamuriwa mapema kwa madai kuwa mshtakiwa amekaa rumande kwa muda wa miezi saba na kwamba kosa lake linadhaminika.

Kwa mujibu wa hati ya maombi iliyoambatanishwa na hati ya kiapo cha wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba mahakama iamuru mshtakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo mahakama itaona yanafaa.

Hati hiyo ya maombi ya dhamana inasema, “Kwamba tunaomba Mahakama hii Tukufu impe dhamana mshtakiwa akiwa na au bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, iliyoko katika mahakama hii tukufu.”