Saturday, January 26, 2013

Hali ya Manumba bado tete, apelekwa Afrika Kusini

Robert Manumba

HATIMAYE Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba amesafirishwa kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee ambako Manumba alikuwa amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) tangu Januari 13, mwaka huu, amethibitisha kusafirishwa kwa kiongozi huyo wa Polisi.
“Ni kweli amesafirishwa jana (juzi),kwenda Afrika Kusini, akiwa katika hali ya kuridhisha, ila sijajua bado jina la hospitali aliyopelekwa,”alisema Dk Dharsee.



Awali  akizungumza kabla ya kusafirishwa Manumba, Dk Dharsee alieleza kuwa hali ya kiongozi huyo sasa inatia matumaini kwani ameweza kujitingisha baadhi ya viungo vya mwili wake, tofauti na awali alipofikishwa hospitalini hapo.
“Anaendelea vizuri, licha ya kwamba yupo ICU, lakini anatia matumaini kwa sababu kwa sasa naweza kusema amepata ufahamu, kwani anaonyesha kuwa ana maumivu,hata uso wake sasa umebadilika tofauti na awali alipokuwa hajitambui,” alisema Dk Dharsee.

Awali Dk Dharsee alithibitisha kuwa Manumba anasumbuliwa na malaria kali baada ya kumfanyia uchunguzi na kukutwa na wadudu 500 wa ugonjwa huo hatari, hali ambayo ilisababisha apoteze fahamu na figo zake zote mbili kushindwa kufanya kazi.

Kwa upande wa Mganga Mkuu Mwelekezi wa Polisi, Dk Ahmed Makata aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu jana kuwa, kusafirishwa kwa Manumba kumefanikiwa baada ya afya yake kuimarika vyema tofauti na ilivyokuwa awali.
“Mimi kwa sasa nipo Tanga, lakini imewezekana kumsafirisha kwa kuwa afya yake imeimarika, yaani presha, mzunguko wake wa damu kwa kifupi ni kwamba imewezekana kwa sababu yupo vyema sasa tofauti na awali, ambapo ilishindikana kumsafirisha,”alisema Dk Makata.

Msemaji wa Polisi, Advera Senzo alipohojiwa kuhusu kusafirishwa kwa Manumba, alithibitisha, lakini hakuwa tayari kueleza amesafirishwa wakati gani, ndege iliyomsafirisha, wala hospitali aliyopelekwa.
“Taarifa ninayokupa ni hii, amesafirishwa jana (juzi) kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi basi hayo mengine mimi sikwambii kwa sasa, lakini amefika salama,” alisema Senso.

Tangu alipolazwa katika Hospitali ya Aga Khan chumba cha ICU, akiwa hajitambui huku akipumua kwa msaada wa mashine, viongozi mbalimbali wakiwamo wa Serikali walimtembelea ili kumjulia hali.

Miongoni mwa viongozi waliomtembelea ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete na mkewe mama Salma Kikwete, Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mke wake mama Tunu Pinda.

Source: Mwananchi

No comments: