Monday, January 14, 2013

Kenya yajitosa sakata la Dr. Ulimboka

Dr Ulimboka alipokuwa Hosptali ya Muhimbili baada ya kutekwa na kuteswa

SUALA la Joshua Mulundi anayetuhumiwa kumteka Dk Steven Ulimboka, katika Misitu ya Pande, limechukua sura mpya baada ya ubalozi wa Kenya nchini kuamua kumchunguza, ili kubaini kama kweli ni raia wake au la.

Balozi wa Kenya nchini, Mtindo Mutiso aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa amesikia taarifa za Mulundi akidai kuwa ni raia wa Kenya, lakini kama nchi, itahitaji kujiridhisha kabla haijajiingiza kumsaidia kwa lolote.

Mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa haijulikani yuko mahabusu gani baada ya kuhamishwa kutoka Gereza la Keko jijini Dar es Salaam kutokana na ufuatiliaji wa vyombo vya habari, amenukuliwa mara kadhaa na baadhi ya magezeti (siyo Mwananchi) kwamba hatendewi haki.



Pamoja na madai mengine, Mulundi amekuwa akitaka Ulimboka apelekwe mahabusu ili amtambue kama kweli alihusika kumteka, ili haki dhidi yake itendeke haraka.

Dk Ulimboka alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba muda kuzungumzia ukweli kuhusu tukio hilo bado na kwamba hajawahi kuitwa, ili akutanishwe na mtuhumiwa huyo.

Hata hivyo, uongozi wa Magereza nchini ulisema kwamba hauwezi kumsaidia mtuhumiwa huyo kwa lolote, badala yake ulimtaka aandike barua ya malalamiko na kumkabidhi mpelelezi wa kesi yake, ili ayafikishe mahakamani kwa hatua zaidi.

Juzi Balozi Mutiso alisema kwamba kutokana na suala hilo kuendelea kuwa na utata hasa kuhusu uraia wa mtuhumiwa huyo, aliamua kutuma ujumbe kwenda Gereza la Ukonga ambako alielezwa kwamba mtuhumiwa huyo anapatikana, lakini hakufanikiwa kumwona.
“Mimi nilituma kijana wangu leo pale gereza la Ukonga, lakini alipofika huko akaelezwa hayupo, eti afuatilie vizuri chanzo chake cha taarifa hizo mahali alipopelekwa. Nikaamua kukupigia simu (gazeti) ili tusaidiane kujua mahali alipo,” alisema Mutiso.

Mutiso alisema kutokana na hatua hiyo ameamua kufuatilia ili kujua madai ya mtuhumiwa huyo kuwa raia wa Kenya kabla hajajihusisha zaidi na suala hilo.
“Taratibu za kibalozi inapotokea jambo kama hilo, ni lazima awepo mtu au ndugu atakayemtambua kuwa

Mkenya, au kupata vyeti vyake vya uraia. Lakini hatujapatiwa vyeti hivyo. Kwa hivyo tunataka kuthibitisha kwanza kama ni Mkenya halafu tuhusike zaidi katika suala hulo,” alisema Mutiso.

Mutiso alisema leo atafanya uamuzi wa kufika mwenyewe katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ama kuandika barua ya kutaka uthibitisho wa uraia wa Mulundi.
“Jumatatu (leo) ndiyo nitawasiliana na wizara ili nifahamu kijana huyo yupo katika gereza gani,” alisema Mutiso.

Wiki iliyopita Kamishna Msaidizi na Msemaji Mkuu wa Magereza, Mtiga Omary alisema jeshi hilo haliwezi kumsaidia chochote, lakini ana haki kuandika barua kwa mpelelezi wa kesi hiyo.
“Siyo jukumu letu kumpeleka Dk Ulimboka akaonane huko, tunachoweza ni kumpatia nafasi ya kuandika barua ya maombi ya mpelelezi wa kesi hiyo ambaye pia ataipeleka Mahakamani,” alisema Mtiga.
Mtiga alikuwa akizungumzia taarifa zilizoandikwa kuhusu malalamiko ya mtuhumiwa huyo.

Mtuhumiwa huyo hivi karibuni aliiomba Mahakani ya Hakimu mkazi Kisutu imruhusu kuonana na Balozi wa Kenya, lakini mahakama ilikataa ombi hilo na kumtaka taratibu za kisheria.

Inadaiwa kwamba, mtuhumiwa huyo ameshafanikiwa kuandika barua kama sheria inavyoagiza na kufikisha ujumbe kwa viongozi mbalimbali wanaohusika akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi lakini hakuna dalili zozote anazoziona za kujua hatima ya kesi hiyo.

Source: Mwananchi

No comments: