Friday, January 18, 2013

Manumba hali ni tete ICU, Kikwete aenda kumwona

Rais Jakaya Kikwete akisindikizwa na IGP Said Mwema kwenda kumwona Robert Manumba hosptali ya Agha Khan alikolazwa
 HALI ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DCI), Robert Manumba bado ni tete na jana Rais Jakaya Kikwete alikwenda tena ikiwa ni mara ya pili mfululizo katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam alikolazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), kumjulia hali.

Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine waliofika hospitalini hapo kumjulia hali DCI Manumba ni Mke wa Rais, Salma, Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP, Said Mwema na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni. Pia walikuwapo ndugu, jamaa na marafiki ambao walikusanyika hospitalini hapo takriban siku nzima jana wakifuatilia afya yake.


Rais Kikwete alifika hospitalini hapo jana saa 11:15 na alitumia takriban dakika 10 tu kwani alitoka saa 11:26 huku akionekana mnyonge na alielekea kwenye gari lake na kuagana na IGP Mwema na Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee kisha kuondoka.

Juzi, Rais Kikwete alikwenda hospitalini hapo mara baada ya kumsindikiza Uwanja wa Ndege mgeni wake Rais wa Benin,Thomas Boni Yayi aliyekuwa nchini kwa ziara ya siku moja.
Jana, Mke wa Rais alikuwa wa kwanza kufika hopitalini hapo saa 10:20 na aliondoka saa 10:45 muda mfupi kabla ya Rais Kikwete kufika.

Habari zilizopatikana jana zilieleza kwamba kutokana na afya yake kuwa mbaya, wageni wengi wakiwamo viongozi waandamizi, walizuiwa kuingia kumwona.

Uongozi wa Aga Khan watoa tamko
Jana mchana, uongozi Aga Khan ulitoa taarifa rasmi kuzungumzia afya ya kiongozi huyo wa Polisi huku ukieleza kuwa kimsingi siyo nzuri na bado anahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.

“Uongozi wa Hospitali ya Aga Khan ungependa kuujulisha umma kwamba Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, DCI Robert Manumba bado yupo hospitalini Aga Khan ambako anaendelea kupatiwa matibabu. Hali yake bado inahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Juzi, Dk Dharsee alisema Manumba alifikishwa katika hospitali hiyo akisumbuliwa na malaria huku hali yake ikiwa mbaya na hajitambui.

Msemaji wa familia atoa mafumbo
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana, msemaji wa familia ya DCI Manumba, James Kilaba alisema: “Maisha ndivyo yalivyo, huwezi kuzua ugonjwa na huwezi kubadili uhalisia wa mambo. Sisi kama familia, tunaamini Mungu yuko na ndugu yetu na ndiye atatenda yake na naomba Watanzania wamuombee.”

Hata hivyo, alikataa kuzungumzia ugonjwa wake zaidi ya kusema kuwa alipelekwa Jumanne iliyopita hospitalini hapo kwa ajili ya vipimo zaidi.

Source: Mwananchi (Picha na Habari)

No comments: