Sunday, January 13, 2013

Ndege ya ATCL yapasuka kioo angani, abiria wanasurika kufa



ABIRIA  25 waliokuwa wakisafiri na ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam wamenusurika kufa baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kupata ufa katika kioo cha mbele, hivyo kumfanya rubani abadili mwelekeo na kutua kwa dharura uwanja wa  ndege wa Kigoma.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni muda mfupi baada ya ndege hiyo aina ya Bombadia Dash 8 kuruka katika uwanja wa ndege wa Kigoma, ikiwa katika safari zake za kwanza, baada ya kusitishwa takriban miezi tisa iliyopita.

ATCL ilisitisha safari zake April 9, 2012 baada ya ndege yake aina ya Dash 8 kupata ajali katika kiwanja cha Kigoma, hivyo Shirika hilo kukosa ndege nyingine. Miezi miwili iliyopita shirika hilo lilinunua ndege mpya.

Kaimu Mkurugenzi wa ATCL, Kapteni Milton Lazaro alisema ilipata hitilafu hiyo dakika 15 tangu iliporuka, baada ya kioo cha mbele kupata ufa.“Ufa ule uliwatisha marubani na waliamua kutua kwa dharura kwa sababu kioo kingeweza kupasuka na kusababisha ajali mbaya na ndege kuanguka,” alisema Lazaro na kuongeza;

“Kawaida vioo vya ndege hupashwa moto ndege inapoondoka na endapo utatokea ufa wowote ni lazima irudi kiwanjani na kama ipo mbali na kiwanja inambidi rubani ateremke chini na kupunguza mwendo.”

Alisema kutokana na hali hiyo, wapo kwenye harakati ya kuifanyia matengenezo ndege hiyo na wakati wowote itarudi kwenye safari zake za kawaida.