Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda |
Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ametaka Katiba Mpya impunguzie Rais madaraka hasa katika nafasi ya uteuzi.
Kauli hiyo ya Pinda inapingana na ile iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kuhusu Katiba Mpya ambaye aliiambia Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba madaraka ya Rais yasiguswe akisema kama atanyang’anywa, atashindwa kuongoza nchi.
Balozi Sefue alisema nafasi ya Rais inapaswa kuwa imara na yenye uwezo wa kuwaunganisha Watanzania wote.
“Asilimia kubwa ya Watanzania, wamekuwa
wakipendekeza Rais apunguziwe madaraka aliyonayo, jambo ambalo linaweza
kuleta hatari mbeleni, suala hili linatupasa kuwa nalo makini,” alisema
Balozi Sefue na kuongeza:
“Tusiwe wepesi wa kutamka maneno bila ya
kutafakari hasara na faida zake, tunapaswa kutambua taifa letu lenye
miaka 51 ya Uhuru bado maskini, kuna mataifa yenye miaka 200 hadi 400,
lakini kamwe hayathubutu kumpunguzia Rais madaraka.”
Hata hivyo, jana Pinda aliiambia tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba: “Kuna haja ya kumpunguzia Rais madaraka kwani amekuwa na mzigo mkubwa wa kuongoza Serikali. Kitu kikubwa ambacho ningependa kiangaliwe kwenye Katiba Mpya kwa upande wa madaraka ya Rais ni katika uteuzi wa viongozi mbalimbali.”
“Nimetaka Katiba Mpya impunguzie mzigo Rais kwani
amekuwa na kazi nyingi sasa ni vyema angepunguziwa mzigo huo hasa katika
masuala ya uteuzi wa viongozi.”
Pinda alitoa mfano kwamba katika kazi ya uteuzi wa viongozi, Makamu wa Rais anaweza kumsaidia kazi hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine ambavyo Katiba itaviainisha.
Pinda alitoa mfano kwamba katika kazi ya uteuzi wa viongozi, Makamu wa Rais anaweza kumsaidia kazi hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine ambavyo Katiba itaviainisha.
Mbali na hayo, Pinda alitaka pia Katiba Mpya izuie wabunge kuwa mawaziri na Serikali za Mitaa ziwekewe mfumo sahihi wa kujiendesha na kuwe na tume itakayoshughulikia masuala ya Muungano, lakini akataka Muungano ubaki wa Serikali mbili.
Jaji Lubuva
Hata hivyo, akitoa maoni yake mbele ya tume hiyo jana, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema kwamba muundo wa Muungano unapaswa kuangaliwa upya kikatiba, ili kuondoa malalamiko yaliyopo kwa muda mrefu.
Alisema suala la dola kwa nchi zilizoungana yaani Tanganyika na Zanzibar linapaswa kutambuliwa ili kila nchi iwe na mamlaka yake kamili.
“Kwa hali ilivyo sasa dola haiko Tanganyika wala
Zanzibar, bali iko kwa Tanzania yote. Jambo hili linaleta manung’uniko
mengi kwani Zanzibar kama ilivyo kwa Bara inahitaji kuwa na dola kamili.
Napendekeza mfumo wa Muungano ufuate matakwa ya wananchi kutoka kila upande, pia Katiba iainishe mambo ya Muungano ili kuondoa malalamiko kutoka kila upande,” alisema Jaji Lubuva.
Pia alisema Bunge linapaswa kuendelea na wajibu wake wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali na siyo kufanya kazi za wizara.
Alisema kwa hali ilivyo sasa, Kamati za Bunge zimekuwa zikitoa maagizo na uamuzi kwa mambo mbalimbali kitu alichosema kuwa siyo sawa kwani hayo ni majukumu ya Serikali.
Jaji Lubuva alisema kitendo hicho kinaweza kudhoofisha utendaji wa Serikali, pia hakizingatii mgawanyo wa madaraka kwa mihimili ya dola.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment