Sunday, February 3, 2013

Kimewaka Bungeni! Wapinzaji watoka Nje ya Bunge

 Maajabu Waziri wa Elimu hana Mtaala ashindwa kuwasilisha Bungeni





Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa
HOJA binafsi ya mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia, imeibua mapya bungeni mjini Dodoma, baada ya Kambi ya Upinzani kukutana kwa dharura, kupinga kufifishwa hoja hiyo na Naibu Spika, Job Ndugai, wakidai anataka kuizima.

Juzi Mbatia aliwasilisha bungeni Hoja Binafsi kuhusu udhaifu wa elimu Tanzania, akitaka mfumo mzima unaosimamia elimu nchini ufumuliwe.

Baada ya majadiliano marefu kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mitalaa, sera na
mihutasari ya elimu, hoja mbalimbali zilitolewa, baadhi ya wabunge wakitaka Kamati ya Bunge, huku wengine wakitaka iundwe tume huru ya kufuatilia suala hilo.

Mjadala huo uliendelea jana asubuhi kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kusimama na kutetea mfumo wa elimu uliopo na mtalaa, kabla ya wabunge kuchangia na Mbatia kuhitimisha.



Akiwasilisha hoja yake, Mbatia aling’ang’ania kupatiwa mtalaa wa masomo ya elimu kwa shule za msingi na sekondari, jambo ambalo, Waziri Kawamba alijibu kuwa ulikuwapo ingawa hakuwa nao bungeni.
Baada ya majibu ya Dk Kawambwa, Mbatia aliomba hoja yake iahirishwe hadi mtalaa utakapowasilishwa bungeni.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisimama na kusema akihoji: “Katika kikao kilichopita, hata katika Hansard, tulisema mtalaa utawasilishwa katika kikao hiki, sasa wasiwasi wa mbunge (Mbatia) ni nini? Hata siku ya mwisho ya Bunge tutaleta.”

Baada ya kauli hiyo, Naibu Spika, Job Ndugai alipiga kura kwa kuuliza wanaotaka hoja imalizike na baada ya majibu, aliruhusu Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla kuwasilisha Hoja Binafsi kuhusu ajira kwa vijana na kilimo.

Hata hivyo, baada ya kumruhusu Dk Kigwangalla, wabunge wa upinzani walitoka nje ya Bunge na kufanya mkutano wa dharura uliochukua dakika 38 katika Ukumbi wa Pius Msekwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa kikao hicho, Tundu Lissu aliwaeleza sababu za wao kutoka nje ya Bunge na hatua za kuchukua.

“Tumewaita kuzungumzia sababu za kutoka nje na hatua za kuchukua. Kama mlivyosikia, Mbatia alisema kuwa hakuna mitalaa wala hakujawahi kuwa na mitalaa tangu mwaka 1961 na kama ipo atajiuzulu. Alipomtaka Waziri ampe japo nakala, waziri alikataa,” alisema Lissu na kuongeza:

“Sasa tunachosema ni kwamba, Waziri Kawambwa amelidanganya Bunge na tutapeleka taarifa ya kikao chetu katika Kamati ya Bunge ya Mamlaka ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, kumtaka ajiuzulu kwa kulidanganya Bunge, ikishindikana tutapeleka kwa Mamlaka zilizomteua.”
Alisisitiza: “Na hapa ikishindikana pia kumwajibisha, tutapiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.”
Hata hivyo, Lissu akiwa pamoja na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema na Mbatia meza kuu, alisema kuwa tangu kuanza kwa vikao vya Bunge, Spika Anne Makinda na naibu wake Ndugai, wameonyesha nia ya kufifisha hoja za upinzani.

Alisema: “Tulitaka kujadili hoja ya suala la gesi ya Mtwara, lakini Spika akazima, akasema itaundwa tume, baadaye akasema tume hakuna baada ya Waziri Mkuu kwenda, tangu Mbatia kuwasilisha hoja yake, inaonekana waziwazi wanataka kuizima.”

Lissu aliongeza: “Kanuni ziko wazi, maspika wamekula kiapo kufanya kazi bila upendeleo, lakini hapa hawatendi haki, sasa sisi kama Kambi ya Upinzani, vilevile tutaandaa hoja kwa lengo la kumwondoa spika na naibu wake.”

Alisema kuwa ingawa mjadala huo wa hoja ya Mbatia unaonekana kutaka kuzimwa, Kambi ya Upinzani haitakubali uzimwe kwa hila, badala yake itahakikisha suala la mitalaa linajadiliwa kwa mujibu wa kanuni.

“Kuna haja ya kuzifanyia marekebisho kanuni mbalimbali za Bunge, ambazo zinampa madaraka makubwa Spika,” alisema Lissu ambaye ni mnadhimu wa kambi ya upinzani.

Akizungumzia hoja yake, Mbatia alisema kuwa wanachokipigania ni kwa faida ya Watanzania wote kuwa lengo ni kupata elimu endelevu kwa kuwa mitalaa iliyopo ni kama sumu wanayowalisha watoto.
“Kila siku wanamdanganya Rais kuwa kuna mitalaa, sasa haipo, kwa nini wasiwajibishwe

wanaosema uongo?...Wanawalinda mafisadi wanaotaka kuchakachua fedha za rada Sh66 bilioni kwa kuchapisha vitabu vibovu, tunataka CAG aende Wizara ya Elimu, kuna madudu,” alisema Mbatia.

Akizungumza baadaye jana, Naibu Spika, Ndugai alisema: “Kama kuna tatizo, Rais, Makamu wa Rais na sisi Spika na Naibu, kila mbunge ana haki ya kutupigia kura ya kutokuwa na imani nasi na ni jambo la kawaida sana. Lakini, uamuzi wa mwisho unatolewa na wabunge wenyewe.”

Source: Mwananchi

No comments: