Friday, February 15, 2013

Wachachamaa Bunge kutoonyeshwa moja kwa moja



Siku moja baada ya Ofisi ya Bunge kutangaza kutoonyeshwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kutokana na baadhi ya wabunge kukiuka kanuni, mjadala mzito umeibuka baada ya kupinga kitendo hicho kwa kusema ni kuwanyima wananchi uhuru wa kupata taarifa huku wengine wakitaka kwenda mahakamani.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema wananchi wana haki ya kufahamu kinachoendelea bungeni kutokana na kuwachagua kwenda kuwawakilisha.Juzi Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari,kauli inayokinzana na ile ambayo Spika Anne Makinda amekuwa akiitoa kwamba ni muhimu mijadala hiyo ikawa inaonyeshwa moja kwa moja.


Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kufanya hivyo ni kinyume cha utawala bora na demokrasia.Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema kufanya hivyo ni kinyume cha Katiba Ibara ya 18 ambayo inaelezea uhuru wa kutafuta, kupokea na kupata habari wakati wowote.


“Jambo la kwanza wakithubutu, sisi Chadema tutachukua hatua kali na hatutazitaja hivi sasa bali tunasubiri wafanye hilo kwanza ndiyo watajua,”alisema.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema wanataka kufanya hivyo ili wachakachue mambo yatakayokuwa yakitokea bungeni hivyo tutawashughulikia wakithubutu.


“Kauli ya Katibu wa Bunge ni ya kiutendaji tu na hawezi kufanya hivyo kwa kuwa kuna tume ya Bunge ambayo sisi wapinzani tuna nafasi, hivyo likiletwa hilo suala tutalipinga,”alisema Mnyika.


Mwenyekiti wa Twaweza, Rakesh Rajani alisema wabunge ni wawakilishi wa wananchi hivyo wanapaswa kujua kile ambacho wamekiwasilisha bungeni.
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema ni bora majadiliano ya bungeni yasionyeshwe kutokana na hali ilivyo hivi sasa.


Mrema ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo alisema pamoja na kwamba kuonyeshwa kwa Bunge ni muhimu ili wananchi wapate mrejesho,lakini hivi sasa linatia aibu hivyo ni muhimu kuidhibiti. Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema hatua hiyo inawanyima wananchi kupata taarifa za chombo ambacho wamekichagua.


“Sisi ndio tumewachagua na kuwatuma kwenda Bungeni, tuna haki ya kujua wanachokifanya huko na siyo kutunyima fursa hiyo”alisema Dk Bisimba.
Imeandikwa na Boniface Meena,Ibrahim Yamola, Aisha Ngoma na Suzan Mwillo