Monday, April 29, 2013

Katiba Mpya imeiva, Mabaraza kukutana mwezi Juni - Warioba


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba (kushoto)
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kuandaa rasimu ya katiba itakayoweka mbele maslahi ya taifa na kuwaomba wananchi waijadili na kutoa maoni yao katika mabaraza ya katiba yatakayokutana kuanzia mwezi Juni mwaka huu (2013).

Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema jijini Dar es Salaam kuwa katika kuandaa rasimu hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.

“Tume haitengenezi katiba ya vikundi au vyama, tunaandaa katiba ya nchi,” amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi za Tume na kufafanua kuwa Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa  na wananchi na sio idadi ya watu waliotoa maoni.

Jaji Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya katiba ya wilaya.

Mabaraza ya Wananchi wenye ulemavu
Akizungumza kuhusu ushiriki wa walemavu katika mabaraza ya katiba, Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.

Hatua hii inafuatia ombi la Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA) waliloliwasilisha kwa Tume.

Jaji Warioba amesema Baraza moja litaundwa Tanzania Bara na jingine Zanzibar na kwamba yatashirikisha wananchi kutoka ngazi ya chini ya wilaya hadi Taifa.

“Tunaelewa kuwa watu wenye ulemavu ni karibu asilimia 10 ya watanzania wote na mchakato huu hauwezi kuwatenga katika ngazi yoyote,” amesema Jaji Warioba na kuongeza kuwa taarifa ambazo Tume yake inazo zinaonyesha baadhi ya watu wenye ulemavu wamependekezwa na mitaa, vijiji, vitongoji na shehia kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.

Chaguzi za Wajumbe Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Aidha, Jaji Warioba amezungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizofanyika nchini kote hivi karibuni za kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tathmini ya Tume inaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa viongozi na watendaji katika ngazi za vijiji, mitaa, shehia na kata walizingatia mwongozo uliotolewa na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani na utulivu.

“Kwa mfano jumla ya shehia 323 sawa na asilimia 96.4 kati ya shehia 335 kwa upande wa Zanzibar zimekamilisha vizuri mchakato huu, hali kadhalika jumla ya Kata 3,331 sawa na asilimia 99.8 kati ya Kata 3,339 kwa Tanzania Bara nazo zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa Mwongozo,” amesema Jaji Warioba.

Kuhusu hatua inayofuata baada ya chaguzi hizo, Jaji Warioba alisema Tume inaendela kupokea majina kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na ya wananchi wote waliopendekezwa kutoka katika Kata na Shehia na kazi hiyo inatarajia kukamilika ifikapo tarehe 30 Aprili mwaka huu (2013)

Changamoto
Akizungumzia kuhusu changamoto zilizojitokeza katika chaguzi hizo, Jaji Warioba amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana pia kulijitokeza changamoto kadhaa ambazo zilisabishwa na misimamo ya kisiasa na kidini

“Katika baadhi ya maeneo mikutano ya uchaguzi ngazi za vijiji, mitaa na shehia ilishindwa kufanyika kutokana na mivutano ya kisiasa na kidini zilizosababishwa na baadhi ya wananchi kufangamanisha chaguzi za Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na masuala ya kisiasa na kidini,” amesema Jaji Warioba.

Jaji Warioba ametaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kujiingiza katika vitendo vya rushwa katika chaguzi hizo ili wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza hayo ya katiba.

“Tumepokea pia malalamiko ya vitendo vya rushwa,” alisema Mwenyekiti huyo na kusema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kuongeza kuwa taasisi zenye mamlaka ya kupambana na vitendo hivyo zinapaswa kushughulikia malalamiko hayo.

 Aina na Majukumu ya Mabaraza ya Katiba
Katika mkutano huo uliofanyika katika katika Ofisi za Tume zilizopo mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti huyo pia alizungumza kuhusu aina na majukumu ya Mabaraza ya Katiba.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imetoa fursa ya kuundwa kwa mabaraza ya aina mbili ambayo ni Mabaraza yatakayoundwa, kusimamiwa na kuendeshwa na Tume katika muda na tarehe itakayopangwa na Tume.

Aina ya pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, ni Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi mbalimbali yenye malengo yanayofanana. Mabaraza haya yatajiunda, yatajisimamia na kujiendesha yenyewe na kisha kuwasilisha maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba ndani ya muda utakaopangwa na Tume.

“Kazi kubwa ya Mabaraza ya Katiba ya aina zote mbili ni kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni rasimu ya Katiba itakayokuwa imeandaliwa na Tume kutokana na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi,” alisema Jaji Warioba na kuziomba taasisi, makundi, asasi na vyama mbalimbali kutumia fursa hiyo ya kisheria kuunda mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa.

No comments: