Friday, May 3, 2013

Mchugaji Msigwa azidi Kumng'ang'ania Kinana


Mch Peter Msigwa

Abrahaman Kinana
Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Maliasili, ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa baada kutoa tuhuma nzito kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwamba anahusika na biashara ya meno ya tembo jana alimjia juu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kwa kitendo chake cha kumtetea Kinana badala ya kumtaka kumpa ushahidi wa tuhuma alizotoa.


“Nilitarajia Nchimbi angenitaka nimpelekee ushahidi badala yake, anamkingia kifua mtuhumiwa, lakini sishangazwi na maelezo yake kwa sababu aliweza kuitwa Dokta kabla hajapata shahada,” alisema.

Alisema badala ya wapinzani kuitwa wahuni, wabunge wa CCM walitakiwa kufanya kazi pamoja kuhakikisha wanalinda masilahi ya nchi.

Hata hivyo Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki naye alijiunga na wale wanaomkingia kifua Bwana Kinana na kusema kwamba tuhuma kwamba Kinana anajihusisha na masuala ya kusafirisha meno ya tembo baada ya meli moja  kukamatwa nchini China ikisafirisha meno hayo ambayo ina mahusiano na kampuni ya uakala wa meli mali ya Kinana si  ya sahihi.

Kagasheki alisema ni makosa kwa Kinana kutuhumiwa wakati kilichokuwa kimebebwa kwenye meli hiyo hakikuwa mali yake.
“Hivi ina maana wamiliki wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) au wale wa Precission Air ndiyo wanapaswa kutuhumiwa kwa kile kinachobebwa na abiria wao kweli?
Ndugu yangu Mchungaji Msigwa anafahamu ninamheshimu sana. Ingawa amenirushia makombora mengi sana. Lakini katika hili nadhani hata kama ni siasa nadhani ni kitu ambacho hakikubaliki kwa wastaarabu,” alisema.
Hata hivyo, Balozi Kagasheki aliahidi kuwa Serikali imepanga kufanya operesheni dhidi ya majangili wa meno ya tembo.
Alisema hawatatangaza siku ya operesheni hiyo kutokana na kuwahusisha watu wengi.