Saturday, June 1, 2013

Matokeo ya Form Six nayo yatoka, wengi wafaulu


Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA Dk. Charles Msonde
Baraza la Mitihani Nchini (Necta), limetangaza matokeo ya kidato cha sita ambapo asilimia 87.85 wamefaulu huku kundi la shule 20 za mwisho likitawaliwa na shule kongwe nchini na zile za Zanzibar.
Akitangaza matokeo hayo jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk Charles Msonde, alisema watahiniwa 50,611 walifanya mtihani huo na kati yao 44,366 sawa na asilimia 87.85, wamefaulu.
Bofya hapa kuangalia matokeo kamili ya Form Six
Mwaka 2012 wanafunzi waliofaulu mtihani huo walikuwa ni 46,658 sawa na asilimia 87.65.
Watahiniwa wa shule
Dk Msonde alisema kuwa, watahiniwa wa shule waliofaulu ni 40,242 sawa na asilimia 93.92 ya waliofanya mtihani huo.
“Wasichana waliofaulu ni 13,286 sawa na asilimia 95.80 na wavulana 26,956 sawa na asilimia 93.03,” alisema.
Mwaka 2012 watahiniwa 40,775 sawa na asilimia 92.30 walifaulu mtihani huo.
Watahiniwa wa kujitegemea
Alisema kuwa, watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo walikuwa ni 7,659 na waliofaulu ni 4,124 sawa na asilimia 53.87.
Ufaulu katika kundi hili umeshuka ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo watahiniwa waliofaulu walikuwa ni 5,883 sawa na asilimia 64.96 ya wote waliofanya mitihani hiyo.
Ufaulu kwa madaraja
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa, watahiniwa 325 sawa na asilimia 0.76 ya wote waliofanya mtihani huo walipata daraja la kwanza, kati yao wavulana wakiwa ni 188 sawa na asilimia 0.65 na wasichana 137 sawa na asilimia 0.99.
Waliopata daraja la pili ni 5,372 sawa na asilimia 12.54 wavulana wakiwa ni 3,142 sawa na asilimia 10.84 na wasichana 2,230 sawa na asilimia 16.08. Waliopata daraja la tatu ni 30,183 sawa na asilimia 70.45 wavulana wakiwa ni 20,442 sawa na asilimia 70.55 na wasichana 9,741 sawa na asilimia 70.24.
Watahiniwa waliopata daraja la nne 4,362 sawa na asilimia 10.18 ya wote waliofanya mtihani huo huku wavulana wakiwa ni 3,184 sawa na asilimia 10.99 na wasichana 1,178 sawa na asilimia 8.49.
Waliofeli ni 2,604 sawa na asilimia 6.08 wavulana wakiwa 2,021 sawa na asilimia 6.97 na wasichana 583 sawa na asilimia 4.20.
Shule za Zanzibar zaboronga
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa, shule kutoka Zanzibar zimefanya vibaya ambapo katika kundi la shule 10 za mwisho zenye watahiniwa zaidi ya 30, saba zinatoka kwenye visiwa hivyo.
Kwa upande wa shule zenye watahiniwa chini ya 30, nne zinatoka Unguja huku shule nyingine kongwe zilizokuwa zikifanya vizuri mwaka huu zimevuta mkia.
Kwa upande wa shule 10 za mwisho zenye watahiniwa zaidi ya 30 ya kwanza kutoka mwisho ni Pemba Islamic College (Pemba), Mazizini (Unguja), Bariadi (Simiyu), Hamamni (Unguja), Dunga (Unguja), Lumumba (Unguja), Osward Mang’ombe (Mara), Green Acres (Dar es Salaam), High View International (Unguja) na Mwanakwerekwe (Unguja).
Shule zilizofanya vizuri zenye watahiniwa chini ya 30, ya kwanza kutoka mwisho ni Mbarali Preparatory (Unguja), Philter Federal (Unguja), St Mary’s (Dar es Salaam, Mzizima (Dar es Salaam), Hijra Seminary (Dodoma), Tweyambe (Kagera), Mpapa (Unguja), Al-Falaah Muslim (Unguja), Presbyterian Seminary (Morogoro) na Nianjema (Morogoro).
Shule zilizofanya vizuri
Shule 10 bora katika kundi lenye watahiniwa chini ya 30, ya kwanza ni Palloti Girls (Singida), St. James Seminary, Parane na Sangiti (zote Kilimanjaro), Itamba (Njombe), Masama (Kilimanjaro), Kibara (Mara), St.Luise Mbinga Girls (Ruvuma), St. Peters Seminary (Morogoro) na Peramiho Girls (Ruvuma).
Shule 10 bora katika kundi lenye watahiniwa zaidi ya 30, ya Kwanza ni Mariani Girls (Pwani), Mzumbe (Morogoro), Feza Boys (Dar es Salaam), Iliboru na Kisimiri (zote kutoka Arusha), St Mary’s Mazinde juu (Tanga), Tabora Girls (Tabora), Igowole (Iringa), Kibaha (Pwani) na Kifungilo Girls (Tanga).

No comments: