Tuesday, July 9, 2013

CHADEMA wasisitiza iwepo serikali tatu, Leo kutoa tamko



Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imekutana kwa dharura kujadili muundo wa serikali tatu na hatma ya Muungano wa Tanganyika na Zanziba, na leo chama hicho kinatarajia kutoa taarifa rasmi ya msimamo wake.

Halikadhalika, suala la Tume huru ya uchaguzi limejadiliwa kwa kina na wajumbe hao huku wengi wakiwa na hofu kuwa kulingana na ilivyopendekezwa kwenye rasimu hakuna uwezekano wa Tanzania kuwa na tume huru  kama ilivyo nchini Kenya.

Hayo yalisemwa jana na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed,wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu yaliyojiri kwenye mkutano huo wa dharura. 

Alisema Chadema itatoa msimamo wake leo mbele ya waandishi wa habari ili Watanzania waweze kujua kwa uwazi kuhusu masuala ambayo yameonekana kuwa mapya.

Alisema kikao hicho kilianza Julai 06, mwaka huu, na suala kubwa lilikuwa ni kujadili kipengele kwa kipengele rasimu ya Katiba, na wajumbe wengi walizungumzia kinagaubaga suala la serikali tatu na hatima ya Muungano.

“Wajumbe wengi wameonekana kulizungumzia kwa kina suala la Muungano, suala la serikali tatu ilikuwa ni moja ya mapendekezo ya Chadema kwa Tume, muundo wake ndio tunaujadili kwa kina,” alisema.

Mohamed alisema suala la tume huru ya uchaguzi limechukua nafasi kubwa katika kikao hicho na  huku wajumbe wengi wakionyesha hofu iwapo kutakuwa na Tume huru  itakayotenda haki wakati wa chaguzi.

Alisema msimamo wa Chadema ni kutaka ipatikane Katiba inayotengeneza viongozi na si watawala.

Alibainisha kuwa suala lingine ni kuanza mchakato wa uundaji Katiba ya Tanganyika kwa kuwa Zanzibar tayari kuna Katiba na itakapokamilika ya Muungano ni wazi kuwa Tanganyika itashindwa kuendesha shughuli zake.

Aidha, Mwenyekiti huyo, alisema kikao hicho pia kilijadili hali ya kisiasa nchini ikiwamo tukio la kulipuliwa kwa bomu katika kampeni za Chadema mkoani Arusha na uchaguzi katika kata 26 nchini.

Tukio la shambulio la bomu lilitokea mwezi Juni, mwaka huu, na kuua watu watatu, akiwamo kiongozi wa Chadema, na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa udiwani katika kata ya Kaloleni.


Source: Nipashe

No comments: