Monday, July 22, 2013

Vilio na majonzi miili ya wanajeshi waliokufa Darfur ilipowasili Tanzania



Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal jana aliwaongoza mamia ya waombolezaji kupokea miili saba ya wanajeshi wa Tanzania waliouawa Darfur, Sudan, Julai 13, mwaka huu.
Miili ya wanajeshi hao saba iliyowasili jana ni SajIni Shaibu Sheha Othman, Koplo Osward Paulo Chaula, Koplo Mohamed Juma Ally, Koplo Mohamed Chukilizo, Private Rodney Ndunguru, Private Peter Werema na Private Fortunatus Msofe.
Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa (Unamid), kusini mwa Darfur na walitoka katika vikosi vya, 42KJ Chabruma, Songea, 44KJ Mbeya, 36KJ Msangani, 92KJ Ngerengere, 94KJ cha Mwenge, Dar es Salaam, 41KJ Nachingwea na Makao Makuu ya JWTZ- Upanga, Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa wanajeshi hao waliuawa na kikundi cha waasi cha Janjaweed kinachoungwa mkono na serikali ya Sudan, huku wengine 19 wakijeruhiwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa walikuwa wakifuatilia magari yao yaliyokuwa yametekwa na kundi hilo.
Hali ilivyokuwa
Baada ya miili hiyo kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Jeshi saa 10:40 jioni na ndege ya Antlantis iliyotolewa na Umoja wa Mataifa(UN), mamia ya watu waliokuwapo uwanjani hapo walionekana kuingiwa na huzuni baada ya kuona miili ya marafiki, ndugu na jamaa zao ikishushwa kwenye ndege hiyo.
Baada ya ndege hiyo kuwasili, viongozi wakuu wa Serikali pamoja na wambolezaji wengine waliisogelea ndege hiyo kwa ajili ya kupokea miili ya wanajeshi hao.
Miili hiyo ilishushwa na kuingizwa kwenye magari saba ya jeshi, na kupelekwa katika Hospitali ya Jeshi la Lugalo kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Wanajeshi hao wanatarajiwa kuagwa kesho Jumatatu katika viwanja vya Makao Makuu ya Jeshi Upanga, baadaye miili hiyo itasafirishwa kwenda kuzikwa katika maeneo yaliyotengwa na familia zao.
Waombolezaji
Baadhi ya ndugu wa marehemu waliofika kwenye viwanja hivyo walisema kuwa walikuwa wakiwategemea sana ndugu zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema mara baada ya kupata taarifa za vifo hivyo, walishtuka na kutoamini kilichotokea huku wakieleza kuwa walikuwa wanawasiliana nao mara kwa mara wakati wakiwa Darfur.