Friday, July 5, 2013

Ziara ya Obama mbwa wa FBI wakagua kwa Kamanda KOVA



Ofisa mmoja wa Usalama wa Marekani (FBI), akiwa na mbwa wakati za ziara ya Obama Tanzania aliingia Makao Makuu ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kufanya ukaguzi.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi kabla ya msafara wa magari ya Marekani kupita yakitokea Ikulu kwenda Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kumlaki Rais Barack Obama.

Polisi ambaye hakutaka kutajwa alisema ofisa huyo  aliingia na mbwa hadi maeneo ya mapokezi, lakini muda mfupi walitoka.
“Walikwenda moja kwa moja mapokezi wakafanya ukaguzi,  kisha wakatoka nje ya jengo na kama hiyo haitoshi, ofisa huyo akiwa na mbwa alikwenda sehemu ya kuegesha magari yenye kesi na yale ya kawaida na kuanza kufanya ukaguzi, baada ya hapo waliondoka,” alisema polisi huyo na kuongeza:
“Licha ya mimi kutokuwa na  cheo pale, lakini hili la kutukagua na mbwa, ni kama wametudhalilisha... sisi ndiyo tunaaminika kwa usalama, leo hii wanatukagua na mbwa. Tena Kituo Kikuu.”
Hata hivyo, usalama kwenye vituo vingi ikiwamo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juliusu Nyerere, vilikuwa chini ya usimamizi na uangalizi wa makachero wa Marekani.