Friday, March 18, 2011

Gaddafi sasa abanwa na Umoja wa Mataifa

Waasi wamekaribisha uamuzi huo kwa furaha kuu mjini Benghazi
Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa limepitisha azimio linaloidhinisha kuchukuliwa kwa hatua za kuwalinda raia nchini Libya dhidi ya mashambulizi ya wanajeshi wa Kanali Muamar Gaddafi.

Miongoni mwake ni kutenga eneo ambalo ndege hazipaswi kupaa angani.

Lakini azimio hilo limepinga matumizi ya wanajeshi wa ardhini.

Serikali ya Ufaransa imesema hatua za kijeshi dhidi ya majeshi ya Kanali Gaddafi zitaanza wakati wowote.

Wanachama kumi wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walipiga kura kuunga mkono azimio hilo lakini wengine watano ikiwemo China, Urusi na Ujerumani walisusia kura hiyo.

Matokeo ya kura hiyo yamepokewa kwa vigelegele,vifijo na ulipuaji wa fataki katika eneo linalodhibitiwa na waasi la Benghazi, Mashariki mwa Libya.

Makundi ya waasi yalipeperusha bendera zao huku wakifyatua risasi angani mara tu habari hizo zilipowafikia.

Awali Kanali Gaddafi alikuwa aliapa kuuteka mji wa Benghazi na kusema kuwa mtu ye yote atakayepinga hatua hiyo atakabiliwa vikali.

No comments: