Sunday, November 25, 2012

Baada ya Mawaziri kuzomewa, CCM yasema itawabana wasiowajibika

Katibu Mkuu wa CCM Abrahaman  Kinana

CHAMA Cha Mapinduzi kimesema utendaji kazi wa mawaziri wanaotokana na chama hicho utapimwa kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Chama hicho, kimesisitiza kuwa Waziri yeyote ambaye utendaji kazi wake hautakuwa wa kuridhisha atakuwa amekalia kuti kavu kwenye nafasi hiyo.

 Kauli hiyo, imetolewa na Katibu Mkuu CCM, Abdulrahaman Kinana, ambaye amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa chama hicho. Wakati Kinana akisema hayo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, ameitaka Serikali kuhakikisha inachukua hatua za kuwakamata viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Katoro mkoani Geita, ambao wanatuhumiwa kutafuna za fedha za umma Sh milioni 16.5.



Hivi karibuni mawaziri watatu walizomewa wakati walipokuwa wakikaribishwa kila mmoja kuelezea kero za wananchi wa mkoa wa Mtwara kusini mwa Tanzania. Mawaziri hao waliambatana na Katibu Mkuu wa CCM Abrahaman Kinana  katika ziara ya kujitambulisha ambapo bila hiana walizomewa mbele yake.

 Wakihutubia mikutano ya hadhara kwa nyakati tofauti mkoani Geita, viongozi hao kila mmoja alitumia nafasi hiyo kuzungumza na wanachama na kuelezea mikakati mbalimbali. Kinana akizungumzia utendaji kazi wa mawaziri, alisema kuanzia kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, watakuwa wakitoa taarifa hizo ambapo wajumbe wa NEC watawabana kwa maswali na kuhitaji ufafanuzi wa kina. Alisema kila waziri, mbunge na diwani, anayetokana na chama hicho atakuwa akipimwa utendaji wake katika kuwahudumia wananchi wa eneo husika.

 Alisema hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliye juu ya chama, bali chama kipo juu yao. “Ninapenda ifahamike sasa, CCM imejipanga katika kuwaunganisha na kuwahudumia Watanzania, hivi sasa tunaanza utaratibu mpya ambapo Mawaziri watakuwa wakitoa taarifa zao katika vikao vya NEC na kuhojiwa maswali na wajumbe.

 “Kila waziri atahojiwa utendaji wa shughuli za Serikali katika wizara yake na utekelezaji wa ilani… ikiwa kuna atakayeonekana hafai hatua stahiki zitachukuliwa. “Ninapenda hili lifahamike vizuri, hakuna aliyekuwa juu ya chama, bali chama kipo juu ya wanachama wake na kama hakuna wanachama hakuna chama, sasa kama kuna kiongozi wa aina yoyote ambaye anajiona hapimiki, ni vema akajiondoa mwenyewe kuliko kusubiri kuondolewa,” alisema Kinana, huku akishangiliwa na umati wa wananchi.

 Akizungumzia makundi ndani ya chama hicho, alisema tangu ulipomalizika uchaguzi wa ndani kuna baadhi ya viongozi walioshindwa, wamekuwa wabinafsi kwa kutochaguliwa katika nafasi za uongozi, hali inayowafanya kujiona bora kuliko wengine. Alisema kutokana na hali hiyo, kuna baadhi ya makada wa CCM wamekuwa wabinafsi huku wakiibuka na sababu mbalimbali, ikiwemo rushwa. “Watu wamekuwa wabinafsi kwa kukosa nafasi za kuchaguliwa ndani ya chama. Kama hakupita anaibuka na sababu lukuki na hata kudai aliyechaguliwa hafai bora yeye.

 “Na kama hakupita anaibuka na sababu za rushwa, kununua watu hii yote ya nini, ila napenda wana CCM wote nchini, watambue hili halifai kwa CCM ya sasa. “Uchaguzi umepita na sasa tuna kazi moja ya kukijenga chama, kwani kila eneo ambalo CCM imepoteza jimbo, kata au mtaa wapinzani ni CCM mwenyewe, sababu kubwa ni ubinafsi wa kutochaguliwa wewe. “Mchana hugeuka CCM, lakini ikifika usiku anakwenda kwa wapinzani kuwapa mikakati ya kushinda na upo mfano mzuri nimeona pale Dar es Salaam na inapotokea mwana CCM mwenzako ameshindwa dhidi ya chama kingine, wewe unakuwa wa kwanza kumpa pole, hii si sawa hata kidogo,” alisema.

 “Moja ya maazimio ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ni kuhakikisha inasimamia Serikali zake za Jamhuri na ile ya Zanzibar, hili linashuka hadi ngazi ya chini kwa halmashauri za wilaya hadi vijiji,” alisema.

No comments: