Saturday, November 24, 2012

Mwanamke aliyekufa na kuwekwa Mochwari arudi nyumbani

Chumba cha kuhifadhia maiti
Wakazi wa Kijiji cha  Lamadi, wilayani Busega mkoani Simiyu nchini Tanzania, juzi walifurika katika Kitongoji cha Mabulugu kumshuhudia mwanamke Ngulima Kilinga (30), aliyedaiwa kufufuka huku mwili wake ukiwa umehifadhiwa katika hospitali ya Mkula iliyopo mkoani humo.

Inadaiwa kuwa mwanamke huyo aliyefariki dunia tangu juzi, alionekana saa chache baadaye akiwa mzima wa afya na kuingia nyumbani kwake.Habari zaidi kutoka katika kitongoji hicho zinasema mwanamke huyo bado amefungiwa ndani ya nyumba yake akifanyiwa dawa za kienyeji ili arudie katika hali yake ya kawaida, kwani kwa sasa anaonekana kama zezeta.
“Bado huyu yumo ndani amefungiwa, lakini saa saba za usiku wa kuamkia leo (jana) alitaka kutoka, aling’ang’ana sana ili atoke, akapiga sana mlango...wakamfanya dawa ndipo akajaribu kutulia hadi sasa bado yumo ndani na usiku alipewa chakula akala na asubuhi amepewa uji” alisema mtu wa karibu wa mwanamke huyo.

Pia inadaiwa kuwa tayari mganga wa kienyeji amekwisha kuja kwa ajili ya kutengeneza mwanamke huyo ili aweze kurudia hali yake na kwamba amewashukuru wananzengo hao kwa kuweka maiti kwenye nyumba ya mtuhumiwa huyo, kwamba hiyo ndiyo njia sahihi.

Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Salum Msangi alithibitisha tukio hilo, lakini akabainisha hayo ni mambo ya imani za kishirikina.
Kamanda Msangi alisema polisi walipelekwa katika eneo la tukio kuhakikisha usalama wa wananchi na hadi saa 9:00 jioni jana, maiti ya mwanamke huyo iliyokuwa hospitali ilikuwa haijazikwa.
Jana umati mkubwa wa watu ulifurika katika Hospitali ya Mkula kulikohifadhiwa mwili wa mwanamke huyo kuushuhudia.

Ndugu wa mwanamke huyo akiwamo mumewe Ngitu Masisanga na mama yake mzazi, Mwashi Myeya walisema Ngulima aliugua ghafla juzi baada ya kukwama na mfupa wa samaki wakati akila chakula nyumbani kwake.
“Baada ya kuugua alipelekwa hospitali ambako alifariki ghafla na kuwekwa kwenye nyumba ya kuhiofadhiwa maiti’’ alisema.

Alisema  cha ajabu ni kwamba wakati wamelala nyumbani kwa marehemu sambamba na waombolezaji wengine, saa 7 usiku marehemu alitokea akiwa uchi.
Walisema marehemu huyo alimwita mtoto wake ampatie nguop na kuchukua albamu ambapo aliangalia picha.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa mbali na kutazama picha hizo na kutaka kupewa nguo zake, pia marehemu huyo alichukua tochi iliyokuwa ikiwaka na kuizima.
Mama mzazi wa marehemu alisema, “Kabla ya kukimbia nje tulimzuia yeye kutoka nje tulimfungia mlango na sisi ndio tukakimbilia nje, licha ya kufunga mlango alikuwa akiupiga kwa nguvu ufunguke ila na yeye aweze kutoka nje, kuna mtu amefanya dawa za kienyeji ndio tunasubiri majibu.”

Chanzo: Mwananchi