Saturday, January 19, 2013

Mwenyekiti Tume ya Uchagazi ataka Tume iteuliwe na Bunge

Jaji Damian Lubuva

 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva ametaka wajumbe wake wasiteuliwe na rais kama ilivyo sasa, badala yake majina yao yapendekezwe na jopo maalumu, kisha yathibitishwe na Bunge kabla ya kupelekwa kwa rais.

Kadhalika, tume inataka rais asiwe na mamlaka ya kuwafukuza kazi wajumbe wake, bali jukumu hilo libaki mikononi mwa jopo.
Jaji Damian Lubuva siku alipoapishwa kuwa Mwenyekiti wa Tume

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Lubuva, alisema pia wanataka wajumbe wa tume waapishwe na jaji mkuu ili kuondoa wasiwasi wa kuwa watii kwa rais ambaye pia anakuwa mwenyekiti wa chama kinachotawala.

Katika maoni yao kwa ajili ya katiba mpya, Jaji Lubuva alisema wanataka pia wajumbe wa tume wasiteuliwe kwa kuzingatia kiwango cha elimu, bali wazingatie sifa nyingine zikiwemo za uadilifu, heshima, uwajibikaji na namna anavyokubalika katika jamii ya Watanzania.



Kufukuzwa kwa kiongozi
Katika mapendekezo yake, Tume ya Uchaguzi pia imetaka kufanyika kwa mabadiliko yatakayowawezesha viongozi wa kisiasa wanaohama, ama kufukuzwa na vyama vyao kubaki katika madaraka hadi mwisho wa muda wao wa uongozi.

Jaji Lubuva alisema iwapo mbunge au diwani atafukuzwa au kuhamia chama kingine, basi ahame na kiti chake cha uwakilishi ili kuzuia matumizi makubwa ya gharama za kufanya uchaguzi mdogo.

Kwa mujibu wa utaratibu wa sasa, kiongozi wa kuchaguliwa anapofukuzwa ama kuhama chama chake, hulazimika kuachia ngazi, hivyo kuwepo kwa uchaguzi mdogo kujaza nafasi iliyoachwa wazi.

Katika mapendekezo mengine, tume inataka kuwepo na utaratibu wa wapiga kura kuwaondoa madarakani wabunge na madiwani ambao hawatawajibika katika nafasi zao, badala ya mfumo wa sasa unaoruhu kuondolewa kwa viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji pekee.

Mahakama ya Uchaguzi
Mapendekezo mengine ya tume hiyo ni kuwepo kwa Mahakama ya Uchaguzi itakayowezesha wadau na wananchi wasiokubaliana na uamuzi wa tume kukata rufaa kabla ya kuwasilishwa kwa kesi za uchaguzi mahakamani.

Alisema kuwa mahakama hiyo itafanya kazi pale itakapohitajika, na muda wa kutekeleza majukumu yake uwe wa haraka kutokana na kazi za uchaguzi zilivyo.