Tuesday, April 30, 2013

Moto mwingine Bungeni: Kinana atajwa sakata la meno ya tembo



Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Abrahaman Kinana leo amelipuliwa vikali bungeni ndani ya hotuba ya waziri kivuli  wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mchungaji Peter Msigwa kuwa kampuni yake ya uakala wa meli imehusika na kusafirisha shehena ya meno haramu ya tembo yaliyokamatwa nchini Vietinam hivi karibuni.

Mchungaji Msigwa alikuwa akisoma hotuba ya maoni ya kambi ya rasmi ya upinzani kuhusu bajeti ya wizara ya maliasili na utalii iliyowasilishwa bungeni mapema leo na Waziri wa wizara hiyo Balozi Khamis Kagasheki.

Amesema kambi ya upinzani inayo ushahidi  kuwa mmoja ya wamiliki wa kampuni hiyo (jina tunalo) ni Abrahamani Kinana ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama Tawala CCM.



Katika hatua nyingine isiyokuwa ya kawaida baada ya muda wa kuchangia hotuba hiyo kuwadia kama vile ilikuwa imepangwa Spika Anna Makinda alimkaribisha Waziri wa Mambo ya Ndani Dr. Emmanuel Nchimbi kuwa mchangiaji wa kwanza ambaye alionekana wazi wazi kumtetea Kinana kwani hakuchangia hoja nyingine zaidi ya kujibu tuhuma za Kinana kuhusika na sakata hilo, ambaye katika mchango wake hakupinga wa kukubali kuwa Kiongozi huyo mwandamizi wa Chama cha Mapinduzi anahusika na kampuni hiyo.

Katika mchango wake Dr Nchimbi alisema kuna tofauti ya majukumu kati ya kampuni ya uwakala wa meli na majukumu ya kampuni ya kushusha na kupakia mizigo bandarini Clearing and Forwarding akimaanisha kampuni ya kada huyo haihusiki na kusafirisha mizigo na hivyo haikuhusika na shehena hiyo ya meno ya tembo.

Dr Nchimbi alisema anayo taarifa kuwa kuwa watuhumiwa wa sakata hilo baadhi yao walishakamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo aliwajata baadhi ya watuhumiwa hao na kusema tayari wameshafunguliwa kesi mahakamani kwa kuhusika na sakata hilo.

Dr Nchimbi aliishutumu CHADEMA kwa madai ya kueneza uongo na kuzushia makada wa CCM tuhuma za uongo.

Habari hiyo iliwahi kuvuma mwaka 2010

Hata hivyo huenda tuhuma hizo zikawa sio jambo geni kwa kada huyo wa CCM kwani alishawahi kutolea majibu tuhuma hizo. ebu soma majibu yake hapa chini yaliyowahi kuandikwa na gazeti la Tanzania Daima.

KADA maarufu na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema hahusiki na usafirishaji wa meno ya tembo nje ya nchi, ikiwa ni siku moja tu tangu gazeti moja la wiki, lichapishe habari iliyomuelezea kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni iliyosafirisha meno hayo.

Hata hivyo, kada huyo amekiri kuwa mmiliki wa Kampuni ya uwakala wa meli ya Sharaf Shipping Agency, iliyohusika kusafirisha makontena yaliyokuwa na nyara hizo za serikali, kabla ya kukamatwa nchini China yakiwa safarini kupelekekwa Hong Kong.

Gazeti hilo lilimtaja Kinana kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo kwa kuwa na hisa 7,500 kati ya 10,000 katika kampuni hiyo, huku hisa nyingine 2,500 zikiwa zinamilikiwa na mshirika mwenzake, Rahma Hussein. Thamani ya hisa hizo ni sh 1,000 kila moja.

Kinana alitoa ufafanuzi huo katika mahojiano maalum na Tanzania Daima.

“Nimeisoma habari hiyo na kwa bahati mbaya sioni anayenilaumu wala kitu ninacholaumiwa nacho. Kwamba nina hisa katika kampuni ya wakala wa meli ya Sharaf ni kweli.

“Lakini mimi sina nafasi yoyote ya kiutendaji na wala sishughuliki na uendeshaji wa kampuni hiyo. Kwa kweli sikujua na wala sikuhusika kwa namna yoyote ile na usafirishaji wa makontena hayo na mengine yoyote,” alisema Kinana.

Alisema anachojua yeye ni kwamba, maofisa wa kampuni hiyo waliuliza na kuambiwa kuwa shehena iliyokuwa katika makontena hayo ni plastiki zilizotumika.

Alifafanua kuwa, wenye wajibu na mamlaka ya kukagua shehena zote zinazosafirishwa nje ya nchi ni mamlaka za serikali na si kampuni ya uwakala wa meli.

Alisisitiza kuwa, hana mamlaka kwa mujibu wa sheria kukagua mali inayosafirishwa japokuwa anaweza kuuliza bidhaa iliyopo katika makontena hayo.

“Ni dhahiri kabisa kwamba, habari hii imeandikwa na jina langu kutumika katika malengo ambayo siyajui. Nahisi kama jina langu limetumika kama pilipili katika kachumbari ili kunogesha habari.

“Kwa bahati mbaya pilipili imezidi katika kachumbari. Kama lengo lilikuwa kupasha habari, basi umma umedanganywa,” alisema Kinana.

Kwa mujibu wa habari hiyo, sakata la kukamatwa kwa nyara hizo za serikali liliibuliwa kwa mara ya kwanza na Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela, katika Bunge lililopita la bajeti.

Ilidaiwa kuwa, nyaraka hizo zilionyesha kuwa, kilichokuwa ndani ya makontena hayo ni plastiki zilizodurufishwa na baada ya ukaguzi kufanyika, iligundulika kuwa, kilichokuwemo ni pembe za ndovu.

Habari ya gazeti hilo hata hivyo, ilimnukuu ofisa mwandamizi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, akieleza wazi kuwa kazi ya kukagua kilichomo kwenye kontena linalosafirishwa si ya wakala wa meli kwani, wenye mamlaka na idhini ya kufanya hivyo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Source: Tanzania Daima



No comments: