Wednesday, July 31, 2013

Mugabe na Tsvangirai 'ama zao ama zetu' wazimbabwe kuamua kwa kura


Wazimbabwe leo wanapiga kura kumchagua Rais na wabunge watakaoliongoza taifa hilo kwa miaka mitano ijayo.
Katika uchaguzi huo, Rais anayemaliza muda wake, Robert Mugabe anatetea kiti chake akichuana na mpinzani wake wa siku nyingi, Waziri Mkuu, Morgan Tsvangirai. Uchaguzi huo unafanyika huku Mugabe ambaye kupitia chama chake cha Zanu-PF akiwa ametawala kwa miaka 33, akipewa nafasi kubwa ya kumshinda Tsvangirai wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC).
Mwangalizi Mkuu wa Uchaguzi kupitia Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc), Bernard Membe alisema ana taarifa kuwa orodha ya majina ya wapiga kura haijawekwa wazi tangu juzi, ikiwa ni siku mbili kabla ya uchaguzi wa leo.
Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, alisema ameshangazwa na hatua hiyo ya kutowekwa wazi orodha ya wapigakura katika baadhi ya vituo.
Alisema orodha ya wapiga kura siyo nyaraka za siri hivyo zilipaswa kutolewa mapema ili kila mpigakura aone jina lake.
“Orodha inatakiwa itolewe ili watu waione na kuhakiki majina yao, pia kujua vituo wanavyotakiwa kupigia kura,” Membe alikaririwa na BBC Focus on Africa akisema.
Tayari MDC kimetishia kwenda mahakamani kutokana na ucheleweshaji huo unaoweza kutia doa uchaguzi. Katibu Mkuu wa MDC, Tendai Biti alisema chama hicho kitachukua hatua za kisheria dhidi ya Tume ya Uchaguzi Zimbabwe (Zec) ili kupata uhakika wa orodha hiyo. Uchaguzi wa leo huenda ukamaliza muda wa Serikali ya mseto baina ya Zanu-PF na MDC.
Mugabe ameiongoza Zimbabwe tangu ilipopata uhuru mwaka 1980. Alilazimika kuingia kwenye Serikali ya mseto baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2009 kutokana na shinikizo la Sadc ili kumaliza mzozo wa kisiasa uliokuwapo nchini humo.
Polisi 10,000
Ili kudhibiti usalama katika uchaguzi huo, zaidi ya polisi 10,000 wamesambazwa kwenye vituo mbalimbali vya kupigia kura. Redio ya Serikali ilitangaza jana jijini Harare kuwa polisi zaidi wamepelekwa Jimbo la Midlands wakiwa na silaha kadhaa zikiwamo bunduki na mabomu ya machozi. Pia ulinzi umeimarishwa katika maeneo ya katikati ya Harare, Highfield na Mbare.
Wafuasi wa Tsvangirai wameanza kushangilia katika maeneo ya wilaya mbalimbali hata kabla ya kupiga kura huku wengine wakiimba kwa kukumbuka ghasia za mwaka 2008, zilizosababisha wafuasi zaidi ya 200 wa MDC kuuawa.
Source: Mwananchi

No comments: