Monday, August 19, 2013

Mashaka uraia wa Ponda, DNA ya ndugu kupimwaWAKATI Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, akiendelea kuuguza jeraha linalodaiwa kutokana na risasi katika mahabusu ya Segerea, jijini Dar es Salaam, wingu jingine la mashaka limeizunguka familia yake. 

Mashaka hayo yanatokana na kitendo cha makachero wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakiwemo wale wa Uhamiaji kudaiwa kuvamia nyumbani kwa wazazi wake, Ujiji mkoani Kigoma, kwa nia ya kuilazimisha familia yake wachukuliwe damu kwa ajili ya vipimo vya vinasaba (DNA).

Gazeti la MTANZANIA limenukuliwa kiripoti hapo jana kuwa limedokezwa kuwa kabla na baada ya tukio la sasa la Sheikh Ponda kupigwa risasi, makachero hao wamejaribu kuifikia familia hiyo ya Ponda kwa takribani mara tano bila mafanikio yoyote.

Mmoja wa wanafamilia hao ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini akihofia usalama wake, imedaiwa amelidokeza gazeti la MTANZANIA kwamba makachero hao baada ya kushindwa kuwashawishi kutoa damu, wakataka wapatiwe mate au nywele kwa ajili ya kufanyia kipimo hicho ili kutambua kama Ponda ni ndugu yao na pia ni raia wa Tanzania.

“Tulikwisha shawishiwa sana, wakati fulani walitukatia hadi tiketi za ndege ili tuje Dar es Salaam kwa ajili ya kipimo hicho pamoja na kufanya mahojiano maalumu, lakini tulikataa, kwa sababu hawa jamaa wanaogopesha,” alisema mwanafamilia huyo.

Alisema baada ya kukataa kutoa damu, ndipo walipofika kwa mara nyingine tena wakitaka kuchukua nywele za mama yake mzazi Ponda pamoja na za baadhi ya ndugu zake, lakini hilo nalo likashindikana baada ya wao kugoma.

“Tangu Sheikh Ponda aumizwe mama yake mzazi amekuwa mgonjwa, baada ya kupokea taarifa hizo kwa mshituko, hata hivyo familia kwa ujumla haina uhuru tena kwa sababu imekuwa ikifuatwafuatwa na makachero hao pamoja na watu wa Uhamiaji.

“Kwa kweli hofu imetanda katika familia yetu na hatujui nini kinafuata kutokana na kuendelea kufuatiliwa na makachero, kwa mfano ile hatua ya kupewa tiketi ili kwenda Dar es Salaam ilitufanya tushituke kwa hofu ya kwamba labda kuna mpango wa kudhuru maisha yetu, wamekwisha kuja mara nyingi, wameomba mpaka kitabu wamekitoa mpaka nakala, alichoandika Sheikh Ponda, kinaitwa ‘Tanu mkoani Kigoma mwaka 1954’,” alisema mwanafamilia huyo.

Wakati taarifa hizo zikiibuka sasa, kwa muda mrefu sasa kumekuwapo na habari za kukanganya juu ya asili ya Sheikh Ponda Issa Ponda, wengine wakidai kuwa ni raia wa nchini Burundi, taifa ambalo linapakana na mkoa wa Kigoma, sehemu inayoelezwa ndiko alikozaliwa. Hata hivyo ndugu zake wanadai kuwa wao ni raia halali wa Tanzania

Wakati huo huo, chanzo kingine cha habari kimelidokezea gazeti hili jinsi Sheikh Ponda alivyofanikiwa kuwakwepa polisi Zanzibar, baada ya kudaiwa kutoa kauli za uchochezi katika mhadhara wa Kiislamu wakati wakiwa visiwani humo.

Inadaiwa kwamba Sheikh Ponda kabla ya kuhutubia mhadhara huo alipita gerezani kumuona kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed.

Kwamba baada ya kumaliza kuhutubia mhadhara huo, alianza safari ya kuelekea katika msikiti wa Mbuyuni, ambako alihitajika kwa kuendesha mhadhara mwingine.

Chanzo hicho kinasema wakati akiwa njiani alipata taarifa kwamba Polisi wameweka mitego ya kumkamata katika maeneo mbalimbali kama bandarini na uwanja wa ndege, hivyo akashindwa kufika katika msikiti huo.

“Baada ya kubaini kuna mitego ipo kila sehemu, alikwenda bandarini kwa ajili ya kupanda boti za kwenda Dar es Salaam na hapo alionekana akiongea na watu mbalimbali, lakini baadaye alitoweka ghafla na haikujulikana mara moja alikoelekea,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo kingine cha habari kinadaiwa kililidokeza gazeti hilo la Mtanzania kuwa Sheikh Ponda alitoroka katika eneo hilo baada ya kubaini kwamba tayari alikuwa anaingia kwenye mtego wa polisi.

Baada ya kutoweka ghafla, inadaiwa kuwa Sheikh Ponda alipanda majahazi ya usiku ya kutoka visiwani humo kuelekea Bagamoyo na hivyo akafanikiwa kukwepa mitego yote iliyokuwa imewekwa na Jeshi la Polisi Zanzibar.

Sheikh Ponda ambaye kwa sasa yupo mahabusu katika gereza la Segerea, anakabiliwa na mashitaka ya uchochezi sehemu mbalimbali nchini kuanzia Juni 2 mpaka Agosti 11, mwaka huu, kwa mujibu wa shitaka alilofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Mbali na shitaka hilo, pia Sheikh Ponda anadaiwa amesababisha mkanganyiko mkubwa katika jamii, kuhusu ukweli wa jeraha analodai kwamba linatokana na risasi aliyopigwa na polisi mkoani Morogoro Jumamosi iliyopita.

Mkanganyiko huo unatokana na Hospitali aliyokuwa akitibiwa ya Muhimbili, Kitengo cha MOI kushindwa kuthibitisha kama jeraha lake limesababishwa na risasi ama la!

Pia kauli zake za uchochezi anazodaiwa kuzitoa katika mhadhara wa Kiislamu mjini Zanzibar zinatajwa kuwa nyuma ya tukio la kumwagiwa tindikali raia wawili wa Uingereza, japokuwa yeye tayari amekanusha kwa vyombo vya habari kwamba hahusiki na tukio hilo.

Source: Mtanzania

No comments: