Thursday, November 25, 2010
Kikwete kuunda Tume kuchunguza matatizo ya mikopo ya wanafunzi vyuo vikuu
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza kuwa ataunda Tume Maalum ya kuchunguza mfumo mzima wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na utendaji wa Bodi ya Mikopo kwa nia ya kuboresha mfumo huo na kuleta ufanisi zaidi.
Rais Kikwete ameahidi kuwa Tume hiyo itakuwa imeundwa na kuanza kazi ifikapo Januari mwakani, 2011.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ataiagiza Tume hiyo kupata mawazo ya wamiliki wa vyuo vikuu, wahadhiri na wanafunzi ili kuweza kupata ushauri uliokamilika.
Rais Kikwete ametangaza uamuzi huo leo, Alhamisi, Novemba 25, 2010, wakati alipofungua rasmi Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), chuo ambacho kitakuwa kikubwa zaidi kuliko kingine chochote nchini na ambacho kimejengwa katika miaka minne ya kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Kikwete.
Huko akishangiliwa kwa nguvu na kwa muda mrefu na wanafunzi waliojazana katika Ukumbi wa Chimwaga kwenye chuo hicho, Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria ufunguzi huo:
“Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, napenda kuwahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa tutaendelea kuongeza fedha katika mfuko huo ili wanafunzi wengi wanufaike. Tumefanya hivyo katika miaka mitano iliyopita na tutafanya hivyo siku za usoni.”
Ameongeza: “Serikali imeongeza fedha za mikopo ya wanafunzi kutoka shilingi bilioni 56.1 mwaka 2005/06 hadi kufikia shilingi bilioni 237 mwaka 2010/11. Wanafunzi waliopatiwa mikopo imeongezeka kutoka 16,345 hadi 69,921. Haya ni mafanikio makubwa na naahidi kuwa tutafanya vizuri zaidi ili tuwafikie wanafunzi wengi zaidi.”
Amesisitiza Mheshimiwa Rais: “Pia tutautazama upya mfumo mzima wa utoaji wa mikopo ikiwepo na utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo kwa nia ya kuuboresha na kuleta ufanisi zaidi. Nitaunda Tume Maalum ambayo nakusudia kuhakikisha inaanza kazi ifikapo Januari mwakani. Mawazo ya wadau wakiwemo wamiliki wa vyuo, wahadhiri na wanafunzi yatasaidia sana. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itatia maelekezo mahsusi wakati zoezi hilo likapofanyika.”
Rais ameupongeza uongozi wa UDOM kwa kutimiza ndoto yake na pia ameutaka kukitunza chuo hicho ambacho ni moja ya vyuo vizuri zaidi katika Afrika. UDOM imezaliwa kutokana na wazo binafsi la Rais Kikwete katika kutafsiri maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi wa CCM mwaka 2005 iliyotaka kupanuliwa kwa fursa katika elimu ya juu.
Pamoja na Rais Kikwete kwenye sherehe hizo alikuwa ni Mheshimiwa Benjamin Mkapa, Rais wa Tanzania wa awamu ya tatu; Mheshimiwa Dkt. Mohamed Garib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza la Chuo na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Idris Kikura. Dkt. Bilal pia alikuwa mhadhiri wa fizikia na msimamizi wa wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PHD) katika chuo hicho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment