. Asema Wapinzani si maadui wa CCM
. Auliza mbona wenzake wamekuwa wakikutana na CHADEMA?
Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye akiongea na Waandishi wa Habari hapo jana |
Hatimaye Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye hapo jana alijitokeza hadharani na kuzunguza na waandishi wa habari huku akikanusha vikali kukutana na viongozi wa CHADEMA kufanya mazungumzo ya kutaka kuhamia chama hicho.
Sumaye amesema hajawi kukutana na viongozi wa chama hicho wala chama chochote cha upinzani.
Hata hivyo alisema ni makosa kufikiri vyama Upinzani na viogozi wake ni maadui wa chama tawala Chama Cha Mapinduzi,CCM
Amesema kama angekutana nao asingeficha na wala asingeogopa kuweka mambo hadharani asingekuwa wa kwanza kufanya hivyo kwa sababu anafahamu hata wenzake wanaotaka kuwania urais kupitia Chama cha Mapinduzi wamekuwa wakikutana na viongozi CHADEMA kufanya nao mazungumzo.
“Mimi ningekuwa nimekutana nao ningesema tu mbona hata hao wengine wanaoutafuta urais kwa udi na uvumba huwa wanakutana nao? Amesema Sumaye.
Alisema yeye ni mwanachama mwaminifu wa CCM na kwamba alishawahi kusema kuwa hayuko kwa ajili ya cheo na wala kukosa ujumbe wa NEC na hasa kwa njia iliyotumika hakumnyimi usingizi wala hahuzuniki kugombea urais kwa tiketi ya CCM endapo ataamua kufanya hivyo.
Sumaye alisema kama ni matatizo, vyama vyote vina kasoro zake, hivyo haoni kama kuhama chama ni suluhu na kutamba kuwa kushindwa kwake kumempa nguvu zaidi na hivyo akiamua kugombea urais lazima apitie CCM.
Baada ya kupigwa mweleka katika kinyang'anyiro cha Ujumbe wa Halmashauri kuu ya CCM na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uwekezaji na Uwezeshaji ,Dr Mary Nagu huku Wilaya ha Hanang kulikuwa na taarifa zilizowahi kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari vya Tanzania kwamba alikutana na viongozi wa CHADEMA ili kuangalia uwezekano wa kuhamia Chama hicho.
Kuhusu mwenendo wa uchaguzi na hata yeye kupigwa mweleka Sumaye alitupia lawama mwenendo wa uchaguzi ndani ya CCM na kuisema uchaguzi wa Hanang’ ulighubikwa na matumizi makubwa ya rushwa, vitisho vingi, uharamia wa kuhamisha wapiga kura usiku na maovu mengineyo mengi.
“La msingi ni kuwa mimi sijakata na wala sitakata rufaa ya kupinga matokeo wala kupeleka malalamiko katika chama changu kwa sababu yaliyokuwa yakitendeka yalikuwa yanafahamika,” alisema.
Aidha Sumaye alipinga kuwa na ugomvi wa kisiasa na Mbunge wa Monduli Lowassa ambapo alikataa kwamba hajawahi kuzungumza na mtu kuhusiana na mambo hayo.
Sumaye alisema taarifa hizo zimekuwa zikisambazwa na kunukuliwa kuwa zimetoka kwenye chanzo kilicho karibu naye, lakini akafafanua kuwa hawezi kupambana na Lowassa kwa sababu hana uhasama naye.
“Nikiamua kugombea urais sitagombea kwa sababu ya mtu fulani bali nitagombea kwa sababu ya nchi na wananchi wa Tanzania,” alisema.
Akifafanua kuhusu vitendo vya rushwa ndani ya CCM, alisema kuwa nchi nyingi hasa zenye demokrasia changa kama Tanzania zimeingia katika vurugu na kuhatarisha amani na utulivu nyakati za uchaguzi.
Sumaye alisema madaraka yatakuja tu kama wananchi wapiga kura wanaona wewe ndiye utayewafaa na
wala wasirubuniwe kwa fedha au jambo lolote kwa kutumia vibaya nafasi ya umaskini wao.
“Hivi leo tunavyoongea hali ya rushwa wakati wa uchaguzi imekuwa mbaya zaidi. Katika uchaguzi wa kidemokrasia wapiga kura humchagua mwakilishi wanayemtaka kwa sababu ya uwezo wake yaani humchagua mwakilishi wao kwa ajili yao.
“Katika demokrasia iliyopondeka kwa rushwa, fedha huwachagulia watu mwakilishi kwa ajili ya waliotoa fedha. Wapiga kura ni wapiga mihuri tu,” alisema.
Sumaye bila kutaja majina ya wahusika, alisema hali imetoka kwenye kuhonga ili achaguliwe katika eneo lake na badala yake kuna rushwa za kimtandao ambapo mtu hutoa fedha katika maeneo mbalimbali nchini ili watakaochaguliwa wawe wafuasi wake mbele ya safari atakapowahitaji.
“Uchaguzi huu umeghubikwa sana na matumizi makubwa ya fedha za rushwa. Suala la rushwa katika nchi yetu na katika CCM siyo mgeni lakini sasa tatizo hilo limeota mizizi na linazidi kuwa kubwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment