Tuesday, October 23, 2012

Waziri Muhongo atema cheche:Siwaombi radhi wezi Bungeni

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameapa kuwa kamwe hataomba radhi bunge kwa madai aliyotoa dhidi ya watu aliowatuhumu kulihujumu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambao amewafananisha na wezi linaripoti gazeti la Mwananchi la Tanzania.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi juzi, Profesa Muhongo alisema yote aliyoyasema kwenye kikao cha Bunge la Bajeti kilichopita ni sahihi na ana ushahidi wa kutosha kuthibitisha tuhuma hizo.
“Kamwe sitaomba radhi kwa wezi. Subirini muone na kusikiliza kwenye kikao kijacho cha Bunge nitakachoongea kwa muda wa hizo dakika tano wanazotaka kunipa niombe radhi,” alisema Profesa Muhongo.


Alitoa kauli hiyo alipotakiwa kuzungumzia kuvuja kwa ripoti ya Kamati ya Brigedia Jenerali Mstaafu, Hassan Ngwilizi iliyoundwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda kuchunguza tuhuma za rushwa kwa wabunge zilizosababisha Kamati ya Nishati na Madini kuvunjwa.

Taarifa hizo za kuvuja kwa ripoti hiyo zinaeleza kuwa, Kamati ya Ngwilizi imependekeza Waziri aombe radhi na Katibu Mkuu wa wizara yake, Eliakim Maswi achukuliwe hatua za nidhami na mamlaka zilizo juu yake.
“Yaani watu waibie taifa, tuwagundue na kuwasema, halafu nisimame kuowaomba radhi? Sitafanya hivyo. Sitaki kuzungumza mengi, lakini Watanzania wasubiri kauli yangu siku jambo hilo litakapowekwa hadharani,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Awali, akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kikao cha Mawaziri wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuhusu mkakati wa kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme nafuu katika nchi hizo, Profesa Muhongo alisema hakuna na kamwe hautatokea tena mgawo wa umeme nchini.
Aliwataka wenye kuombea mgawo wa umeme utokee nchini kubadilisha maombi yao, kwani jambo hilo halitatokea tena kutokana na mikakati iliyowekwa na serikali kuongeza uzalishaji kupitia gesi asilia, mafuta na maji.
Alitaja vyanzo vingine vya uzalishaji umeme vinavyoendelea kufanyiwa kazi hivi sasa, kuwa ni makaa ya mawe, umeme jua, joto ardhi na mabaki ya mimea kama miwa ambayo imegundulika kuzalisha umeme.
Akitoa takwimu za uzalishaji umeme alizopokea juzi asubuhi katika utaratibu wake wa kupokea taarifa ya uzalishaji mara tatu kwa kutwa, Waziri huyo alisema zilizalishwa megawati 355.40 kwa kutumia gesi, 170
kwa mafuta na 110 kwa maji.
Alisema hadi sasa uwezo wa juu wa uzalishaji umeme nchini ni megawati 1,348 kwa siku wakati mahitaji ya ni megawati 830.

Waziri huyo alienda mbali kwa kuwataka wanaokwenda Makanisani, Misikitini au sehemu yoyote ya Ibada kuomba mgawo wa umeme utokee nchini wabadilishe maombi yao kwa sababu hayatasikilizwa.

Alitaja tatizo na changamoto pekee inayoikabili Wizara yake na Tanesco kuwa ni miundombinu ya kusambaza umeme unaozalishwa ndiyo maana nguvu kubwa sasa imeelekezwa kwenye uboreshaji wa miundombinu ili kila
Mtanzania mwenye kuhitaji umeme mijini na vijijini apate huduma hiyo.

Hivi sasa wanaopata huduma ya umeme nchini ni zaidi ya asilimia 18 ya Watanzania wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 40 milioni.

Waziri Profesa Muhongo alisema idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka mara dufu kati ya sasa hadi 2017 baada ya miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, jua, mabaki ya mimea na joto ardhi itakapokamilika.

Alisema Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuzindua mradi mkubwa wa kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Mnazi Bay-Dar es Salaam.

No comments: