Kikwete Amlilia Marehemu Kaboyonga
|
Rais Jakaya Kikwete |
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA),
Ndugu Irene Charles Isaka kufuatia kifo cha ghafla cha Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo, Bwana Siraju Juma Kaboyonga.
Marehemu Kaboyonga
ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini kupitia tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), amefariki ghafla usiku wa kuamkia leo tarehe 19 Desemba, 2012
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amepelekwa kwa matibabu
ya ugonjwa wa moyo.
“Nimepokea kwa
masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Bwana Siraju Juma Kaboyonga
ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta
ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambako amefanya kazi kwa muda mfupi kabla mauti
hayajamkuta”,
amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
“Nilimfahamu Marehemu
Siraju Juma Kaboyonga, enzi za uhai wake, kama Kiongozi na Mtumishi mwenye
uwezo mkubwa aliouonyesha dhahiri alipokuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo vipaji vyake alivyojaaliwa
na Mwenyezi Mungu kuwatumikia kikamilifu Wananchi wa Jimbo la Tabora Mjini na kwa
kweli Umma wa Watanzania kwa ujumla”.
Rais Kikwete amesema
ni uwezo wake huo mkubwa uliomwezesha kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambako
hakika mchango wake mkubwa unaonekana dhahiri hivi sasa.
“Kufuatia msiba huu
mkubwa, ninakutumia Salamu zangu za Rambirambi wewe Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Ndugu Irene
Charles Isaka kwa kumpoteza Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka yako. Aidha kupitia kwako, naomba unifikishie
Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu kwa
kupotelewa na Kiongozi, na kwa kweli Mhimili madhubuti wa Familia”.
Rais Kikwete amesema
anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema
peponi Roho ya Marehemu Siraju Juma Kaboyonga. Amewahakikishia wanafamilia kuwa
yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo huku akiwataka wawe
na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, kwani
yote ni mapenzi yake Mola.
No comments:
Post a Comment