Thursday, December 20, 2012

Rufaa ya Lema yaiva, Kesho hukumu kusukwa au kunyolewa

MAHAKAMA ya Rufani nchini, kesho inatarajia kutoa hukumu ya rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Godbles Lema, kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyotengua ubunge wake.



Hukumu hiyo inayovuta hisia za wengi nchini, inatarajiwa kuhudhuriwa na wafuasi wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mamia ya wafuasi wa Lema kutoka mjini Arusha, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa mkoa huo, Aman Gulugwa, wanatarajia kuongoza msafara wa magari kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusikiliza rufaa hiyo ya kihistoria.

Habari za kuaminika toka ndani ya Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, zilisema kuwa tayari jopo la majaji watatu; Nataria Kimaro, Salum Massati na Bernad Ruhanda, limeshamaliza kazi na kwamba uongozi wa mahakama umepanga hukumu hiyo isomwe kesho.
“Tarehe ya hukumu ya rufaa iliyofunguliwa na Lema ni kesho, hivyo mfike bila kukosa,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Desemba 4 mwaka huu, Mahakama ya Rufaa ilisikiliza sababu 18 zilizowasilishwa na mawakili wa Lema, Method Kimomogoro na Tundu Lissu kupinga hukumu iliyomvua ubunge mteja wao.

Baadhi ya hoja za mawakili wa Lema ni pamoja na madai kwamba Jaji Gabriel Rwakibalila wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, alijielekeza vibaya katika hukumu yake alivyosema kesi za uchaguzi hazitawaliwi na kanuni za sheria za Uingereza wakati kuna maamuzi ya kesi mbalimbali zilizokwishatolewa hukumu na Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu nchini na kuruhusu kesi za uchaguzi ziamuliwe kwa kanuni za sheria za Uingereza.

Mawakili wa Lema pia walidai hakuna ushahidi unaoonesha wajibu rufaa kweli ni walioandikishwa kupiga kura katika Jimbo la Arusha Mjini.

Mawakili hao pia wanadai jaji alikosea kisheria kusema kuwa mtu yeyote akiwemo mpiga kura ana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo ambalo yeye ni mpiga kura.



Kutokana na hali hiyo, wanaiomba Mahakama ya Rufaa itamke kuwa wajibu rufaa (wapiga kura wa Arusha waliofungua kesi ile), hawana haki kisheria kufungua kesi ya kupinga ubunge wa Lema kwani mwenye haki ni Dk. Batrida Buriani aliyekashifiwa.

Pia walidai hukumu ile haina hadhi ya kuitwa hukumu kwani Jaji Rwakibalila alikosea na kujielekeza vibaya kisheria katika kutoa hukumu.

Kwa upande wa mawakili wa wajibu rufaa, Aluthe Mugwai na Modest Akida na wakili wa Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis walijibu sababu zote 18 na kusisitiza kuwa hukumu iliyovua ubunge wa Lema, ilikuwa sahihi na ilikidhi matakwa ya sheria.

Aprili 15 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitoa hukumu katika kesi ya kupinga ubunge wa Lema iliyofunguliwa na wapiga kura watano wa Jimbo la Arusha Mjini.

Katika hukumu hiyo, mahakama ilimtia hatiani Lema kwa makosa ya kutoa lugha za matusi na udhalilishaji dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. Burian katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Source:Tanzania Daima

No comments: