Pro. Anna Tibaijuka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi |
Wakazi wa eneo la Chasimba Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam wamemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ashughulikie mgogoro wao wa ardhi na Kiwanda cha Saruji cha Twiga kilichopo Wazo Hill na kuhakikisha wanapata haki yao na si vinginevyo.
Walitoa kilio hicho jana mbele ya waziri huyo aliyekutana nao kuzungumzia amri ya Mahakama ya Rufani iliyowataka wananchi wanaoishi eneo hilo kuondoka kwa kuwa linamilikiwa na kiwanda hicho.
Akizungumza mbele ya Waziri, Diwani wa Kata ya
Bunju, Majisafi Sharifu alisema wamekutana na waziri kwenye kikao hicho
kutafuta suluhu lakini msimamo wao ni kwamba wananchi kwanza halafu
kiwanda baadaye.
“Tuko kwenye kikao hiki cha usuluhishi na msimamo wetu ni kwamba wananchi kwanza halafu kiwanda baadaye hivyo mheshimiwa waziri ujue hilo,” alisema na kuongeza;
“Hatutaki kwenda kinyume na Serikali lakini ni muhimu mkaliangalia hili jambo kwa umakini.”
Diwani wa Kata ya Wazo, John Moro alimwambia Tibaijuka kuwa wananchi wanateseka hivyo ni muhimu haki ikapatikana kuhusu eneo hilo na kama ikiwezekana Rais aingilie kati.
Baadhi ya wananchi ambao walifuatana na madiwani hao walisema kuwa kilichozungumzwa nao ndiyo msimamo wa wakazi wa Chasimba katika mgogoro huo.
Akijibu hoja za wakazi hao, Prof Tibaijuka alisema
mgogoro huo ni wa muda mrefu na kwa kuwa
Mahakama ya Rufani imeshatoa hukumu kuwa walioko kwenye vitalu namba 1,4 na 7 waondoke itabidi iwe hivyo na Serikali inaangalia wapi pa kuwapeleka.
Mahakama ya Rufani imeshatoa hukumu kuwa walioko kwenye vitalu namba 1,4 na 7 waondoke itabidi iwe hivyo na Serikali inaangalia wapi pa kuwapeleka.
Prof Tibaijuka alisema Serikali italipima eneo
hilo kwa kushirikiana na wananchi ili kujua mipaka ilivyo na pili
itafanyika tathmini ya kuangalia nini kilichopo na kinachotakiwa
kulipwa.
Alisema Rais hawezi kuingilia mgogoro huo na kusema wananchi waache kwa kuwa tayari mahakama imeshatoa hukumu ya kwamba wahame.
Nako huko Mkoani Arusha Wananchi wa Kijiji cha Mangola Juu, Wilayani Karatu mkoani Arusha wameitaka Serikali kuingilia kati mgogoro kati yao na mwekezaji wa Shamba la Tembotembo Coffee Estate la sivyo watajichukulia sheria mkononi kumwondoa mwekezaji huyo kwa nguvu.
Wakizungumza kwa jazba na waandishi wa habari waliotembelea kijijini hapo jana, wananchi hao kwa nyakati tofauti, walisema kwa miaka 10 sasa mwekezaji huyo, Christian Leons amekuwa akiwataka wananchi wanaoishi katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 40 sasa, kuondoka kwa madai eneo ni mali yake.
Katika moja ya madai yao, walisema mwekezaji huyo amefikia hatua mbaya ya kuwafungia wananchi barabara ya Mangola Juu kwenda Kituo cha Afya cha Makoromba jambo ambalo wananchi hao wamesema Serikali isipoingilia kati kuweka mpaka kati yao na mwekezaji huyo watajichukulia sheria mkononi.
“Nimeishi hapa kwa miaka 30 sasa na nina watoto 11 na wajukuu
katika eneo hili, leo hii mwekezaji huyu ananiambia nitoke eti eneo hili
ni lake nitaenda wapi?” alisema Loem Dagaro huku akiangua kilio.
Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho, Dominic Saghao
alisema hana imani na Serikali ya Wilaya kwani wao wako upande wa
mwekezaji huyo na Ofisi ya Ardhi Wilaya imemwekea mipaka ya wananchi
mwekezaji huyo pasipo makubaliani yoyote kati ya Serikali ya kijiji na
mwekezaji huyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Clement Berege alisema: “Ni kweli sisi kama serikali ya Wilaya tuna taarifa ya mgogoro huu na ninaahidi kutafutia ufumbuzi mapema.”
Diwani wa Kata ya Sinza Jijini Dar es salaam,
Renatus Pamba amewataka wale wote waliovamia maeneo ya wazi kuyaachia
mara moja kwani wamekiuka kanuni na taratibu zilizowekwa na Manispaa ya
Kinondoni.
Kauli hiyo inafuatia malalamiko kutoka kwa wakazi wa Sinza kudai kuwa maeneo ya wazi yameshikiliwa na watu wenye fedha na wanayamiliki kinyume na taratibu za ardhi.
Pamba aliyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Kata hiyo juzi na kusema atahakikisha anawatoa wavamizi hao na hata kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Alisema atashirikiana na Manispaa hiyo katika kutatua tatizo kwani maeneo 18 ya wazi katika Kata hiyo yamevamiwa na kujengwa.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment