Tuesday, December 4, 2012

Rufaa ya Lema leo, Mawakili ndugu ukoo wa Lissu Uso kwa Uso



 Maelfu ya wafuasi wa CHADEMA na CCM leo wanatarajiwa kumiminika mahakama ya Rufaa ya Dar es Salaam kufuatilia Rufaa ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema inayotarajiwa kuanza kusikilizwa leo na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Salum Massati, Nathalia Kimaro na Bernard Luanda.
Pamoja na mambo mengine, rufani hiyo itakayosikilizwa Dar es Salaam,  itawakutanisha wanasheria wawili ndugu; Tundu Lissu na Alute Mghway wa upande wa mashtaka na utetezi.

Lissu ambaye ni kada wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema jana kwamba atakuwapo mahakamani leo na wakili mwenzake, Method Kimomogolo wakishirikiana kumtetea mteja wao.



Wakati Lissu akimtetea Lema, Mghway ni wakili anayewatetea warufani wa (wajiburufaa) ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.

Makada hao walimfungulia Lema kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, wakipinga matokeo yaliyompa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka  2010. Hukumu ya kesi hiyo ndiyo iliyomvua ubunge Aprili 5, 2012 mwaka huu.

Baadaye Lema alikata rufaa kupinga hukumu iliyomvua ubunge, lakini ilitupiliwa mbali baada ya Mahakama kuridhika kuwa kulikuwa na dosari za kisheria, kutokana na  pingamizi lililowekwa na warufaniwa.

Hata hivyo, tofauti na hoja za wakili wa warufaniwa, Mghway kuwa kutokana na dosari hiyo, mrufani hana nafasi ya kufanya marekebisho, mahakama ilimpa Lema nafasi nyingine ya kufungua upya rufaa hiyo baada ya kusema dosari hizo zinarekebishika.
Mahakama hiyo ilimpa Lema siku 14 kufanya marekebisho na kufungua tena rufaa hiyo, kazi ambayo aliitekeleza.

Awali, rufaa hiyo ilikuwa ikisikilizwa na jopo lililoongozwa na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman akisaidiana na Jaji Salum Massati na Jaji Nathalia Kimaro, lakini sasa Jaji Mkuu, Othman hayuko katika jopo hilo na nafasi yake imechukuliwa na Jaji Luanda.

Katika rufaa yake ya awali, Lema alitoa hoja 18 za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha iliyomvua ubunge,  lakini tarehe ambayo rufaa hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa, wakili wa wajiburufaa, Mughwai aliweka pingamizi la awali.

Wajiburufaa katika pingamizi lao walitoa hoja tatu za pingamizi  wakidai kuwa kuna mkanganyiko katika vifungu vya sheria kati ya vile vilivyotumika kwenye hukumu na  vile vilivyokuwapo kwenye muhtasari wa hukumu.

Hoja nyingine walidai kuwa muhtasari wa hukumu haukuwa na mhuri wa Jaji aliyeitoa wala tarehe na hoja ya tatu ilikuwa ni utaratibu wa kuandika muhtasari huo, kwa kutokuandika maneno; “Imetolewa kwa mkono wangu na mhuri wa Mahakama.”

Kutokana na hoja hizo, Wakili Mghwai aliiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali rufaa hiyo, akidai kuwa kwa dosari hizo, mrufani hana nafasi tena ya kuzifanyia marekebisho.

Upande wa wajibu pingamizi, Wakili wa Lema, Kimomogoro na Wakili wa Serikali, Timoth Vitalis kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali walidai kuwa kasoro zote zilizotajwa hazina athari na zinaweza kurekebishika.

Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali hoja mbili za rufaa kuwa hazina msingi na ikakubaliana na hoja moja ya pingamizi kwamba kulikuwa na tofauti au kuchanganywa kwa vifungu hivyo vya sheria.
Katika uamuzi  wake wa Novemba 8, 2012,  Mahakama ilisema kuwa kisheria, hati ya muhtasari wa hukumu ni lazima ikubaliane na hukumu lakini katika shauri hilo muhtasari wa hukumu ulikuwa haukubaliani na hukumu.

“Hukumu inarejea Kifungu cha 114 (1)-(7), (Sheria ya Uchaguzi), lakini hati ya decree inarejea Kifungu cha 113 (1)- (7),” ilisema Mahakama hiyo na kuongeza:
“Decree lazima ikidhi masharti ya Amri ya XX, Kanuni ya 6 na 7, za Mwenendo wa Mashauri ya Madai, Sura ya 33. Katika shauri hili na kukiuka amri ya  XX Kanuni ya 6 na 7, dosari hiyo inaifanya hati hii isiwe halali.

Hata hivyo, mahakama ilisema kuwa inakubaliana na mawakili wa wajibu pingamizi hilo kuwa kosa hilo linawezekana limetokana na kuteleza kwa kalamu au kutokana na kosa la uchapaji.
“Kwa sababu hii linaweza kurekebishwa chini ya Kanuni ya  111ya Kanuni za Mahakama,” ilisema Mahakama na kumpa Lema siku 14 kufanya marekebisho ya dosari hizo na kufungua tena rufaa hiyo.

Source:Mwananchi

No comments: